Mgaza aiokoa Dodoma Jiji dakika za jioni

WAKATI Tanzania Prisons ikiwa na matumaini ya kuondoka na pointi tatu, mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Yassin Mgaza dakika ya mwisho akaiokoa timu hiyo na kichapo katika mechi ya kwanza wa mashindano ya Tanzanite Pre-Season International.

Mchezo huo ulioanza kupigwa  saa 7:00 mchana leo Agosti 31, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, kipindi cha kwanza kilimalizika bila ya timu hizo kufungana.

Kipindi cha pili dakika ya 65, Haruna Chanongo aliitanguliza Tanzania Prisons akiunganisha kwa kichwa krosi ya Kabona Never.

Hata hivyo, Yassin Mgaza, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Anuary Jabir, aliisawazishia Dodoma Jiji dakika ya 90+4 kwa mkwaju wa penalti.

Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanafanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yameanza leo Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025.

Jumla ya timu 10 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A lina timu za Bandari FC ya Kenya, Fountain Gate na Tabora United zote za Tanzania Bara.

Kundi B zipo Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union zote za Tanzania Bara huku Kundi C kuna Namungo kutoka Tanzania Bara, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).