Dar es Salaam. Wakati Chama cha National League for Democracy (NLD) kikiwa kimetangaza kuzindua kampeni zake Septemba 4, 2025 mkoani Tanga, mgombea urais wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, ametoa tahadhari akidai kwamba kwa siku tatu tangu kuanza kwa kampeni, kuna viashiria vya kutokuwepo kwa usawa na heshima kwa wagombea urais.
Akizungumza leo Jumapili, Agosti 31, 2025, alipopokelewa makao makuu ya chama hicho kwa mara ya kwanza tangu alipothibitishwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa mgombea urais wa NLD, Doyo amedai kwamba kuna baadhi ya viashiria vinavyoonesha wagombea wa urais wa vyama vingine, kikiwamo chama chake, hawaheshimiwa na kunakosekana usawa.
“Kwa siku tatu hizi, NLD tumeingia woga kwa hiki kinachoendelea tangu kuzinduliwa kwa kampeni. Nalisema hili kama tahadhari, tunahitaji usawa kwenye vyombo vya habari katika kuripoti taarifa za uchaguzi.
“Vyombo vingi vya habari ni kama vinaelemea upande mmoja. NLD jana tulikuwa Zanzibar, wakati mgombea urais (alitaja moja ya vyama) akichukua fomu tume na sisi tulikuwa pale. Maana tulipangiwa tufike saa 5 asubuhi, tulipofika tukawakuta. Alipoondoka yule mgombea, askari wote nao waliondoka.
“Msafara wa mgombea urais wa NLD ukaachwa na kuingiliwa na magari ya kawaida kwenye mlango wa tume. Hili jambo limetufedhehesha. Tunaomba heshima ya wagombea urais wa vyama vyote,” amesema.
Amesema pia usawa wa kuripoti matukio ya wagombea wa urais wa vyama vyote nao unawapa wasiwasi, kutokana na namna ilivyotokea wakati mgombea urais wa NLD Zanzibar jana alipokwenda tume kuchukua fomu.
Akifafanua hilo, Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, amesema malalamiko hayo ya NLD naye ameyasikia.
Amesema tume itachukua hatua ya kuepusha changamoto kama hizo zisijirudie wakati wa kurejesha fomu, ikiwamo kupishanisha muda wa mgombea wa chama kimoja na kingine ili wasikutane kwenye ofisi hizo.
Pia watazungumza na baadhi ya taasisi nyingine ili kuwasaidia kuwaleta wagombea na kuondoa changamoto kama hizo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo amefafanua kwamba baada ya watiania wa urais wa Zanzibar kuthibitishwa Septemba 11, 2025 na kuwa wagombea urais kwenye vyama vyao, watapewa ulinzi na huduma nyingine kama hizo.
“Kwa sasa bado ni watiania, hawajathibitishwa na tume. Wakishathibitishwa na kuteuliwa, watakuwa na ulinzi na kila kitu watapatiwa,” amesema.
Akizungumzia mikakati ya chama hicho, Doyo ambaye pia ni Katibu wa NLD, amebainisha namna wanavyokwenda kufanya kampeni na namna wanavyojiandaa kushughulikia matatizo ya Watanzania endapo wataipa NLD ridhaa ya kushika dola.
“NLD tunakwenda kuzindua kampeni mkoani Tanga, Septemba 4 kuanzia saa 2 asubuhi kwenye uwanja wa Stendi ya Pangani maarufu Komesho,” amesema Doyo, akiainisha vipaumbele vya chama hicho vilivyo kwenye ilani yao.
“Kwenye ilani ya chama tumebeba mambo mazito makuu manne ambayo ni ajira, afya, elimu na miundombinu, ambavyo haya ndiyo maisha ya Watanzania,” amesema Doyo.
Akitolea mfano changamoto ya miundombinu, amesema kuna kero maeneo mengi, akigusia barabara ya Morogoro kutoka Chalinze hadi Dar es Salaam.
“Tukiwa tunatoka Dodoma, tulifika Chalinze saa 1:30 usiku, lakini Dar es Salaam tulifika saa 5:30 usiku. Hii ni sababu ya changamoto ya miundombinu. Nikiwa Rais nitapanua hiyo barabara iwe na njia nne. Kutoka Chalinze–Dar itakuwa ni dakika 45 tu,” amesema.
Amesema maboresho hayo yatafanyika pia kutoka Chalinze hadi Dodoma, mpaka Tunduma na Namanga, ambako katika kuboresha huko, ataacha eneo katikati ambalo litapandwa michikichi ili kutoa fursa ya kuvuna mawese na kutengeneza mafuta.
Doyo pia amegusia suala la rushwa akibainisha kwamba, katika vipaumbele vyake, mtu akithibitika amekula rushwa mbali na kufungwa, atatandikwa viboko hadharani na tukio litaonyeshwa mubashara kwenye televisheni ya Taifa.
“Mkinipa ridhaa, tutatunga sheria ambayo wala rushwa watakimbia nchi hii,” amesema mgombea huyo wa urais.
Amesema endapo atapewa ridhaa, ndani ya siku 90 atashughulikia kadi za bima za afya, kusiwe na kifurushi ambacho kinatoa huduma hii na ile hauipati.
“Kama mtu analipia, kwanini kwenye matibabu kuwe na limit (ukomo)? Ametoa pesa, apate huduma ya afya. Si unamwambia kiwango hiki huduma fulani hauipati. Watanzania wakinipa ridhaa, ndani ya siku 90 nitaliondoa hili.
“Kwanini watu walipishwe kwenye bima ya afya, halafu uambiwe ugonjwa huu kadi hii haikutibii? Hii si sawa. Mkinipa ridhaa, nakwenda kuondoa hili,” amesema.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani 2025 zilianza Agosti 28, 2025 tayari kwa uchaguzi mkuu ukaofanyika Oktoba 29.