Mbeya. Waendesha pikipiki ‘bodaboda’ jijini Mbeya wamesema ili kupunguza wimbi la ajali za mara kwa mara barabarani ni kuwapo mikataba rasmi na mikopo isiyoumiza.
Wamesema chanzo cha wao kutajwa kuwa chanzo cha ajali za barabarani ni kuwahi abiria ili kukusanya marejesho ya waajiri wao na kukamilisha mikopo waliyonayo.
Wakizungumza katika hafla fupi ya maadhimisho ya mwaka mmoja wa mauzo ya pikipiki aina ya TVS 250, jijini hapa, baadhi ya waendesha bodaboda wamesema chanzo cha ajali ni kukimbizana na marejesho ya waajiri wao.
Eliah Richard ambaye ni mwendesha bodaboda Kanda ya Kabwe jijini hapa, amesema kwa sasa kumekuwapo na utulivu kwa madereva hao kutokana na mafunzo na elimu wanayopewa kutoka Jeshi la Polisi.
Amesema pamoja na juhudi hizo, lakini changamoto kubwa ni mikataba isiyo rasmi ambayo muda mwingine wamiliki wa vyombo vya moto huamua kumnyang’anya dereva chombo anapokosa au kuchelewesha marejesho ya siku.
“Wamiliki wa vyombo hivi wawe na mikataba rafiki, marejesho kuwapo uvumilivu ili kuondoa presha kwa madereva na kupoteza umakini barabarani,lakini hata mikopo hii iwe rafiki,” amesema Richard ambaye ni makamu katibu wa chama cha waendesha bodaboda.
Naye Alexander Bugogo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodaboda Kanda ya Kabwe, amesema mikataba mingi wanayoingia na wamiliki haina manufaa zaidi ya kukandamiza madereva, hali inayowapa hofu.
Amesema kwa sasa wamejishika na Jeshi la Polisi kujifunza sheria za barabarani, akieleza kuwa wamiliki wengi wa vyombo vya moto wamekuwa wakiongeza muda wa mikataba tofauti na makubaliano.
“Tumeanza mafunzo ya wiki mbili, changamoto kubwa ilikuwa kwa baadhi ya wamiliki kuongeza siku katika mikataba na kutishia kutunyang’anya kifaa, sasa hali hiyo inaondoa utulivu kwa dereva barabarani,”amesema Bugogo.
Kwa upande mdau wa usafirishaji na Mkurugenzi wa Kampuni ya Utu Haki, Godwine Jumbe amesema kupitia pikipiki wameamsha uchumi wa wananchi na kusaidia maisha ya wengi katika shughuli zao za kila siku.
“Pikipiki haibebi tu mtu au mzigo bali kufikisha uaminifu, kuokoa na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja, familia, kundi hadi Taifa, huu ni mnyororo kuanzia anayezalisha, anayeuza hadi mtumiaji.
“Hadi sasa kuna watu maisha yao yanategemea zaidi pikipiki, ndio maana leo tumekusanyika hapa kufurahia pamoja mafanikio ya mwaka mmoja wa TVS Gia 5 ya 125,” amesema Jumbe.
Meneja wa TVS Mkoa wa Mbeya, Fadhili Nangale amesema wanajivunia mafanikio ya bidhaa hiyo kwa kuwa, tangu wameingia sokoni watumiaji wamekuwa na matumizi bora na ya faida kiuchumi.
“Tuwashukuru wateja wetu, tunaahidi kuendelea kuzalisha kilicho bora kwa manufaa ya walaji, tumeona namna wakazi wa Mbeya walivyotupokea na ndio maana tukaamua kukutana nao kwa ajili ya hafla fupi,”amesema Nangale