*Ampa siku mbili katibu mkuu akanushe, baada ya hapo asilaumiwe
Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mwenezi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Joseph Ndala, amepinga vikali taarifa inayoenezwa mitandaoni inayodai kuwa amevuliwa uanachama wa chama hicho, akisisitiza kuwa yeye ni mwanachama halali na mmoja wa waanzilishi wa ACT.
Ndala amesema hatua hiyo ni kielelezo cha udhaifu wa kiuongozi ndani ya chama, kwani imekiuka Katiba na kanuni za ACT-Wazalendo.
Amesema barua inayodai kumvua uanachama imetokana na tawi la Mafiga mkoani Iringa, wakati yeye ni kiongozi na mwanachama hai wa chama hicho jijini Dar es Salaam. “Hata Mwanasheria Mkuu wa chama alishawahi kuthibitisha rasmi kuwa mimi si mwanachama wa tawi la Mafiga bali natokea Dar es Salaam. Aidha ushiriki wangu katika vikao na mikutano ya kitaifa umekuwa ukitambulika kupitia Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Ndala.
Ameongeza kuwa hata kama angekuwa mwanachama wa Tawi la Mafiga, hatua ya kumvua uanachama ilipaswa kufuata taratibu za kikatiba, ikiwemo kuandikiwa barua rasmi, kupewa sababu na nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kabla ya maamuzi yoyote. Ndala pia ameitaka Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama kujitokeza hadharani ndani ya siku mbili na kukanusha barua hiyo. “Wasipofanya hivyo, tusilaumiane,” ameonya.
Katika taarifa yake, amewataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutoachishwa mjadala wa msingi ndani ya chama, akibainisha kuwa hoja kubwa kwa sasa ni uamuzi tata wa viongozi waliompitisha Luhaga Mpina kuwa mgombea urais kwa kukiuka kanuni na taratibu za chama.
Amesisitiza kuwa tukio la kuenezwa kwa taarifa hiyo ni jitihada za kumdhoofisha mtu anayepigania heshima ya Katiba na misingi ya demokrasia ndani ya chama.