MPANGO maalumu wa kuwawezesha vijana kujifunza mchezo wa kikapu umezinduliwa wikiendi kwa ushirikiano baina ya Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Vodacom Tanzania sambamba na Shirika la Salesian of Donbosco Kanda ya Tanzania.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye viwanja vya Donbosco Oysterbay, jijini Dar es Salaam ukishuhudiwa na viongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD) pamoja na Shirikisho la mchezo huo nchini (TBF).
Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom, Zuweina Farah alisema mpango huo umeangazia dhamira ya kampuni hiyo katika kuwawezesha vijana, kujiendeleza kielimu na michezo, kwa lengo la kukuza vipaji vya ndani na kuimarisha maendeleo ya jamii.
Kama sehemu ya mpango huo, kampuni hiyo imekarabati Uwanja wa Kikapu wa Don Bosco Oysterbay na kutengeneza mazingira salama na ya kisasa kwa wanamichezo chipukizi kujifunza na kushindana.
“Uwekezaji wetu ni zaidi ya katika michezo, tumejikita katika kukuza uwezo wa vijana kupitia elimu na ushirikiano wa kijamii,” alisema Zuweina aliyeongeza;
“Tunajivunia kuiunga mkono BDL na kuchangia katika ukuaji wa mpira wa kikapu nchini Tanzania. Ushirikiano huu unaakisi dhamira yetu pana ya kuleta athari chanya katika jamii na kujenga uhusiano wa kudumu na vijana wa Kitanzania.”
Kwa upande wa Padri Emilius Salema, Mkuu wa Shirika la Salesian of Don Bosco, Kanda ya Tanzania, aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo.
“Tunatoa shukrani za dhati kwa Vodacom Tanzania kwa mchango wao mkubwa. Ukarabati wa uwanja wetu wa kikapu na ufadhili wa masomo uliotolewa utakuwa na matokeo chanya ya muda mrefu kwa wanafunzi wetu na jamii kwa ujumla,” alisema Padri huyo.
Rais wa BD, Shendu Mwagalla alitoa shukrani fupi kwa kusema; “Tunaishukuru Vodacom Tanzania kwa udhamini na msaada wao. Ushirikiano huu utaikuza Ligi ya Mkoa (BDL), kuendeleza wachezaji na kuhamasisha mpira wa kikapu kote Dar es Salaam. Tunatarajia msimu wenye mafanikio na ushirikiano endelevu.”