Dar es Salaam. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimetangaza ajenda kuu zitakazotekelezwa iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza Tanzania, kikisisitiza nia yake ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania kupitia sera zinazolenga kuboresha maisha, kupambana na ufisadi na kuinua uchumi wa wananchi wa kawaida.
Pia, kimeahidi kudhibiti ufisadi na kuongeza uwajibikaji serikalini kwa kuhakikisha utawala bora unaojali maslahi ya umma na kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma hadi Sh800,000 baada ya makato.
Hayo yameelezwa kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika kwenye viwanja vya Biafra, Kinondoni, Dar es Salaam leo Jumapili, Agosti 31, 2025.
Uzinduzi huo umeshuhudiwa na wananchi waliojitokeza kusikiliza sera na ahadi za chama hicho, huku wagombea wa chama hicho, Salum Mwalimu (mgombea urais) na Devotha Minja (mgombea mwenza) wakitambulishwa rasmi.
Akizungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho, Salum Mwalimu amesema uchaguzi wa mwaka huu ni wa uamuzi mgumu wa wananchi kuendelea kuchagua ahadi hewa, umaskini au kuanza safari mpya ya matumaini.
Mwalimu amesema kupitia ilani ya chama hicho wameipa kipaumbele sekta ya habari kwa kuufanya mhimili sawa na Mahakama na Bunge, akisisitiza mhimili wa habari ndio kiunganishi kati ya Bunge, Serikali na Mahakama.
“Tumeamua kuweka habari nafasi ya juu kwani ndio itahabarisha kasoro za Serikali na mapendekezo ya Watanzania ndiyo yatapitia huko. Tutasimamia kuwa mhimili rasmi wa dola nchini, kwani Serikali inayojificha kuonwa ndiyo yenye mambo mengi ovu. Hivyo, Serikali nitakayounda hakutakuwa na hofu ya kumulikwa ndani au nje,” amesema.
Mwalimu amesema kupitia ilani ya chama hicho wamelenga kukuza uchumi jumuishi katika sekta zote, kuboresha uongozi, kujenga maadili na kuhakikisha mafisadi wanakomeshwa, kwani wanatumia rasilimali za Taifa kwa maslahi binafsi.
Kwa eneo la utumishi na utawala, Mwalimu amesema wanatambua changamoto nyingi zinazowakabili watumishi wa umma zipo za makusudi na pia bahati mbaya.
“Tunaomba ridhaa tukatetee maslahi ya watumishi. Ndani ya miaka mitano ya uongozi wetu, kima cha chini cha mshahara ni Sh800,000 baada ya kodi,” amesema.
Pamoja na hayo, amesema wanapokwenda kuongeza maslahi hayo, lazima watumishi nao watambue fedha wanazolipwa zinatokana na kodi za Watanzania, hivyo lazima wafanye kazi kwa kujituma na Serikali ya Chaumma haipo tayari kuwaona wakifanya Serikali shamba la bibi.
Suala la wastaafu nalo ameligusia akisema, mafao ya wastaafu ndani ya siku 100 wakiwa madarakani watawasilisha muswada wa sheria kurejesha kikokotoo cha zamani ili wastaafu wanapolipwa wapewe fedha zao zote kwa wakati mmoja.
Kwa eneo la bunge, Mwalimu amesema ndani ya uongozi wa Chaumma mhimili huo utajitegemea na hautatumiwa kulinda Serikali.
“Bunge lazima lisimame kukemea na kudhibiti Serikali. Sina sababu yeyote ya kulindwa, sina ndugu ambaye ni mtumishi wa umma, kwa hiyo naingia Ikulu nikiwa msafi kwenda kuwatumikia Watanzania,” amesema.
Mwalimu amesema pamoja na Mahakama kuwa yenye mamlaka ya mwisho ya kutoa haki, amesisitiza mambo ya kurekebishwa ikiwemo bajeti yake kutolewa kwa wakati.
“Suala la bajeti lisitumike kama fimbo ya kuichapa Mahakama, bali kibembelezi chake. Tutahakikisha bajeti inatengwa na inatoka kama ilivyo,” amesema.
Pia, amesema maisha ya majaji ni magumu na wanaishi maisha ya upweke, hivyo lazima Serikali ifidie upweke huo na kwamba kupitia Chaumma, majaji hao watakwenda kuishi kwa raha.
Kwa eneo la maadili ya uongozi, Mwalimu amesema wanaamini uongozi si nafasi ya kujinufaisha bali kuhudumia umma.
“Hatuhitaji kuimba tu utawala wa sheria, tunataka uongozi ambao hakuna kiongozi atakayekuwa juu ya sheria. Ndiyo maana nimesema nitaipa uwezo Mahakama iweze kunihukumu pale ambapo sitendi haki,” amesema.
Mwalimu amesema watahakikisha wanadhibiti upotevu wa maji unaotokana na ubovu wa miundombinu, akisisitiza miradi ya maji imekuwa shamba la bibi kwani mingi huzinduliwa lakini haitoi maji.
“Kwa eneo la vyakula, Chaumma itafuta kodi zote za vyakula ili vipatikane kwa bei rahisi. Hakuna sababu ya wananchi kutozwa kwenye vyakula kwani Taifa lenye njaa halina ustahimilivu. Kucheza na chakula ni kutengeneza bomu ambalo likilipuka hakuna wa kulizima,” amesema.
Amesema wakishika dola wataanzisha sera ya ubwabwa kwa wote ili Watanzania wapate lishe kwa wakati wote bila kujali vipato vyao.
“Kwa wajawazito, suala la kwenda hospitali kujifungua kama unavyoenda kuanza kidato cha kwanza bweni, unalazimika kubeba vyandarua, beseni, maji, mto na foronya. Sisi hatutaki kuwasababishia kinamama msongo wa mawazo,” amesema.
Mgombea huyo wa urais amesema kwenye eneo la makazi watahakikisha wanapunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi na kutoa motisha kwa wauzaji wa vifaa vya ujenzi.
“Tutaondoa tozo ya maendeleo ya viwanda ili kuwezesha wananchi kujenga majengo kwa gharama nafuu. Pia, tutapunguza kodi ya ongezeko la thamani kutoka asilimia 18 hadi 12,” amesema.
Awali, akiwahutubia wananchi, Minja amesema watawekeza katika kilimo na ajira kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana.
“Kuboresha huduma za afya na elimu ili wananchi wote wapate huduma bora bila ubaguzi. Tunataka kuongeza vipato vya wananchi,” amesema.
Minja, aliyehutubia kwa hisia kali, amesisitiza kuwa ni wakati wa kuipumzisha CCM baada ya miaka 60 ya kushindwa kutatua changamoto za msingi.