Mtambo wa mabao Yanga unasukwa

NI takribani siku 17 zimebaki kuanzia leo, Agosti 31, 2025 hadi Septemba 16, 2025 itakaposhuhudiwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba kuashiria kufunguliwa kwa msimu wa 2025-26.

Wakati mchezo huo ukisubiriwa kwa hamu kubwa, huko kambini Yanga kocha mkuu wa kikosi hicho, Romain Folz amekuwa bize kuimarisha kikosi chake huku kubwa zaidi ni katika kuendeleza makali ya kucheka na nyavu.

Folz anafahamu kwamba Yanga msimu uliopita ilivuna mabao mengi katika mashindano yote rasmi matano waliyoshiriki ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Muungano.

Katika kuendeleza moto huo, ameanza kuusuka mtambo wake wa mabao kupitia mechi za kirafiki ambazo timu hiyo inacheza kwenye maandalizi yake ikiwa imepiga kambi Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo zimelidokeza Mwanaspoti kuwa hadi kufikia sasa ingawa si kwa kiwango kikubwa, lakini kuna matumaini yapo eneo la ushambuliaji.

Chanzo chetu kimebainisha kwamba, si ushambuliaji pekee, kwani hata ulinzi umeimarishwa japo kuna baadhi ya wachezaji walikosekana katika maandalizi ya awali kutokana na kuwa kwenye majukumu ya kuitumikia Taifa Stars kwenye michuano ya CHAN 2024 iliyofikia tamati Agosti 30 mwaka huu.

“Kuna vitu kocha anaonekana kuridhishwa navyo kiasi ikiwamo suala la kufunga mabao kitu ambacho ameendelea kukiwekea mkazo kwani siku zote ili upate pointi tatu kwenye mechi, lazima ufunge.

“Kocha anafahamu msimu uliopita Yanga ilikuwa imara zaidi katika kufunga mabao, hivyo hata usajili uliofanyika umezingatia kuendeleza ubora huo,” alisema mtoa taarifa huyo.

Rekodi zinaonyesha kuwa, msimu uliopita katika michuano hiyo mitano ambayo Yanga ilishiriki na kubeba makombe manne ikilikosa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoishia hatua ya makundi, ilifunga jumla ya mabao 136.

Mabao hayo 136 yalikuwa hivi; Ngao ya Jamii (5), Ligi Kuu Bara (83), Kombe la FA (22), Ligi ya Mabingwa Afrika (22) na Kombe la Muungano (4).

ECUA, BOYELI WAMPA KICHEKO FOLZ

Katika kuusuka huo mtambo wa mabao maingizo mapya Celestine Ecua na Andy Boyeli yameonekana kumfurahisha Folz kutokana na kuuwasha moto.

Nyota hao waliobebeshwa matumaini ya Yanga kufanya vizuri 2025-26, kila mmoja amefunga katika mechi nne za kirafiki walizocheza. Ecua ametokea Ligi Kuu ya Ivory Coast alipokuwa Mchezaji Bora (MVP), akifunga mabao 13 na asiti 12, wakati Boyeli alikuwa Sekhukhune United ya Afrika Kusini, alimaliza ligi na mabao sita.

Ndani ya mechi nne za kirafiki ambazo Yanga imecheza hadi sasa, timu hiyo imeshinda zote na kufunga jumla ya mabao 13, huku Ecua akipachika matatu na Boyeli mawili.

Kwa upande wa Pacome Zouzoua ambaye msimu uliopita alifunga mabao 12 katika ligi, naye anaendelea kuuwasha moto kipindi hiki akifunga mabao mawili sawa na Prince Dube, mshambuliaji aliyemaliza ligi na mabao 13.

Wengine waliofunga katika mabao hayo 13 kwenye mechi za kirafiki ni Lasine Kouma na Offen Chikola ambao ni nyota wapya, pia mabeki wa kati Bakari Mwamnyeto na Aziz Andabwile.  Pia timu hiyo imekuwa imara kwenye ulinzi ikiwa imeruhusu mabao mawili ikiwakosa mabeki wa kati Dickson Job na Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ waliokuwa wakiitumikia Taifa Stars katika CHAN.

Safu hiyo ya ulinzi imeboreshwa pia kutokana na ujio wa nahodha wa zamani wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anayecheza beki wa kushoto na Frank Assinki ambaye ni kiraka wa ulinzi.