Mwihambi kurejesha majeshi Mtibwa Sugar

BEKI wa kati, Vedastus Mwihambi yupo mbioni kurejea Mtibwa Sugar, baada ya mkataba wake na Tanzania Prisons kumalizika, ambapo mazungumzo baina ya pande zote mbili yapo katika hatua nzuri zaidi.

Nyota huyo anarejea Mtibwa Sugar ikiwa ni misimu miwili imepita tangu aondoke ndani ya kikosi hicho msimu wa 2022-23 na kujiunga na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, kisha baadaye kuondoka na kujiunga na maafande wa Prisons.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema wanaendelea na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao na tayari wapo wachezaji wanaofanya pia mazungumzo nao, hivyo muda utakapofika watawaweka wazi.

“Baadhi ya wachezaji tuliokamilisha taratibu zote za kuwasajili tumeshawatangaza na tunaendelea na wengine ambao bado tupo katika mazungumzo nao, dirisha la usajili halijafungwa hivyo, mashabiki zetu watarajie makubwa,” alisema.

Kifaru aliongeza hawezi kusema kama mchezaji huyo wamekamilisha taratibu zote za kumsajili, japo ni kweli wapo waliofikia makubaliano ya kukichezea kikosi hicho kwa msimu wa 2025-2026 ili kuleta ushindani tofauti na ukimya wao unaozungumzwa.

Licha ya kauli ya Kifaru, Mwanaspoti linatambua Mwihambi amekamilisha dili hilo na muda wowote atatangazwa kwa lengo la kuichezea timu hiyo, akiungana na nyota mwenzake kiungo, Ezekia Mwashilindi aliyetokea pia kwa maafande wa Prisons.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu msimu wa 2022-2023, imerejea tena Ligi Kuu ikiwa ndio mabingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa kinara kwa pointi zake 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea pia kufuatia kushuka daraja.