Dar es Salaam. “Mtoto wa leo ndiye kiongozi na mchapakazi wa kesho. Ili kumjenga, tunahitaji uwekezaji wa muda, upendo na malezi yenye mwelekeo sahihi.”
Hii ni kauli ya mtaalamu mmoja wa malezi, Chrinstom Haule aliyoniambia wakati nazungumza naye juu ya hoja hii.
Haule aliniambia kuwa si lazima iwe na gharama kubwa, bali moyo wa kujitoa na maadili yanayowekwa nyumbani na shuleni, ndiyo mwongozo mkuu kwa mtoto.
Anasema kama wazazi watajitoa kumjenga mtoto katika bidii, nidhamu, ujasiri na mshikamano, watakuwa wanaunda kizazi kitakachoweza kusimamia mabadiliko ya kesho kwa busara na uadilifu.
Hapa nikajifunza jambo kuwa, uongozi bora na uchapakazi si vipaji vya kuzaliwa navyo pekee; ni matokeo ya malezi na mazingira tunayoandaa leo kwa ajili ya watoto wetu.
Katika ulimwengu wa leo unaobadilika kwa kasi, suala la malezi limekuwa na uzito mkubwa kuliko wakati mwingine wowote. Dunia inahitaji watu wenye nidhamu ya kazi, maadili na ujuzi wa uongozi unaoheshimu utu wa kila mmoja. Hivyo basi, jukumu la mzazi au mlezi haliko tu katika kumlisha na kumvalisha mtoto, bali pia katika kumwandaa awe raia mwema, mchapakazi na kiongozi wa baadaye mwenye dira na uthubutu.
Siku zote tunelezwa kuwa watoto ni kioo cha maisha ya wazazi wao. Wanachokiona ndicho wanachokichukua kama somo la maisha. Mzazi au mlezi anapodhihirisha tabia ya uchapakazi, uadilifu na uwajibikaji, mtoto naye hujenga hulka hiyo.
Mtoto anayemwona mzazi wake akiheshimu muda wa kazi, akitimiza ahadi na kuonyesha bidii katika shughuli zake, anajifunza kuwa bidii na uthubutu ni njia ya kawaida ya maisha. Hali kadhalika, uongozi huanzia nyumbani.
Mzazi anaposhirikisha familia katika uamuzi mdogo, akisikiliza maoni ya watoto, au kuonyesha ustahimilivu katika changamoto, anamfundisha mtoto kwa vitendo maana halisi ya uongozi.
Hivyo tabia ya kuwa mchapakazi haiji ghafla mtu akiwa mtu mzima la hasha; hilo ni zao la malezi ya muda mrefu.
Njia bora ya kumjenga mtoto ni kuanza kwa kumpatia majukumu madogo anapokuwa mdogo.
Kwa mfano, mtoto anaweza kufundishwa kupangilia vitabu vyake, kufagia chumba au kusafisha meza baada ya kula chakula. Ingawa majukumu haya huonekana madogo, huchangia kumfanya aelewe mapema kuwa kazi ni sehemu ya maisha na kila mtu ana wajibu.
Kadri anavyokua, anaweza kupewa majukumu makubwa zaidi yanayolingana na umri wake na hatua kwa hatua anajengeka katika msingi wa uwajibikaji.
Hakuna uchapakazi bila nidhamu. Nidhamu ndiyo msingi unaomfanya mtu kufuata ratiba, kutimiza majukumu kwa wakati na kutoahirisha kazi.
Watoto wanapofundishwa kupanga muda wao, kusoma kwa wakati, kucheza kwa wakati na kupumzika ipasavyo, wanajifunza kuendesha maisha yenye uwiano.
Mzazi anaweza kumsaidia mtoto kuandaa ratiba ya kila siku na kumfuatilia, si kwa hofu bali kwa maelekezo. Nidhamu hii si tu inamfanya mtoto awe mchapakazi, bali pia humwezesha kukabiliana na changamoto kwa ustadi na bila kukata tamaa.
Kwa sababu tunaambiwa kiongozi wa kweli si yule anayefuata maelekezo pekee, bali anayethubutu kufanya uamuzi na kusimamia msimamo wake.
Ili mtoto ajenge ujasiri huu, ni muhimu apewe nafasi ya kujieleza na kutoa maoni yake nyumbani au shuleni. Kwa mfano, mzazi anaweza kumuuliza mtoto maoni yake kuhusu chakula cha familia, ratiba ya michezo au namna ya kutatua changamoto ndogo.
Hata kama uamuzi wake hautafuatwa kila mara, kitendo cha kusikilizwa, humjengea kujiamini na kumwandaa kuwa kiongozi anayejua kusimamia anachokiamini.
Uongozi bora hauhusiani na mamlaka ya kutawala, bali uwezo wa kushirikiana na kuheshimu wengine. Watoto wanaposhirikishwa katika michezo ya kikundi, kazi za pamoja nyumbani au kushiriki miradi ya kijamii, wanajifunza kuwa mafanikio makubwa hupatikana kwa mshikamano.
Wanafundishwa kuzingatia maoni ya wenzao, kusaidia wenye uhitaji na kushirikiana kwa heshima.
Hizi ndizo stadi zinazowaandaa kuwa viongozi wanaothamini mshikamano wa kijamii badala ya nguvu za mamlaka.
Historia ya viongozi wengi wakubwa duniani imejaa changamoto na kushindwa kwao mara nyingi kabla ya kufanikiwa. Somo hili ni muhimu kwa watoto.
Mzazi anapaswa kumfundisha mtoto wake kwamba, kushindwa si ishara ya kutokuwa na uwezo, bali ni darasa la kujifunza na fursa ya kujaribu tena.
Kwa kumweleza simulizi za watu mashuhuri waliopitia changamoto kubwa lakini hawakukata tamaa, mtoto hujengeka katika moyo wa uvumilivu na bidii. Hii humsaidia kukua akiwa mtu asiyeogopa changamoto bali anayeona fursa ndani yake.
Na hata kama malezi ya nyumbani ni mazuri, mazingira ya mtoto kwa ujumla pia yanahitajika kumjenga. Elimu bora, vitabu vya kusoma, muda wa kucheza na kuchunguza, pamoja na malezi ya kimaadili ni nyenzo za msingi.
Mzazi anapohakikisha mtoto yuko kwenye mazingira salama, yenye changamoto chanya na yenye fursa za kujifunza, anamwezesha kukua akiwa mbunifu, mwenye fikra pevu na mwenye uwezo wa kufikiri kimkakati ambazo ni sifa kuu za kiongozi na mchapakazi wa kesho.
Methali ya Kiswahili inasema, “Mtoto hulelewa, hajilelei.” Hii ina maana kuwa malezi ya mtoto si jukumu la mzazi pekee, bali ni jukumu la familia, walimu na jamii yote.
Wakati jamii inapoonesha mshikamano katika malezi ya mtoto, husaidia kila mmoja kuwajibika kumjenga katika misingi ya maadili, uchapakazi na uongozi.
Shule zinaposhirikiana na wazazi kuwafundisha nidhamu na bidii, jamii nzima hunufaika kwa kuandaa kizazi cha kesho kilicho imara zaidi.