Dar es Salaam. Wakati sekta ya utalii nchini Tanzania ikiendelea kuwa kinara katika uingizaji wa fedha za kigeni, wadau na wafanyabiashara wanaohusika kwenye sekta hiyo wamehakikishiwa ushirikiano ili kuendelea kukua kwa kasi.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zaidi ya watalii milioni 5.3 wametembelea vivutio na hifadhi mbalimbali nchini na kuingiza mapato ya zaidi ya Dola 4 bilioni za Marekani.
Hatua hiyo imeendelea kuifanya sekta hiyo kuwa miongoni mwa zinazotegemewa katika uingizaji wa fedha za kigeni barani Afrika.
Kutokana na hatua hiyo, Benki ya NMB imewahakikishia wafanyabiashara wakubwa jijini Arusha kuwa, itaendelea kushirikiana nao kwa karibu zaidi ili kukuza shughuli zao na kuongeza ufanisi wa kibiashara.

Akizungumza kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyowakutanisha zaidi ya wafanyabiashara 100 wakubwa jijini Arusha juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna amesema benki hiyo inatambua mchango mkubwa wa jiji hilo katika sekta ya utalii na biashara, hivyo imeamua kushirikiana nao kuhakikisha ustawi wa sekta hiyo unazidi kupaa.
“Moja ya jukumu letu ni kuhakikisha ustawi na uendelevu wa biashara zenu. NMB imekuwa ikibuni bidhaa na huduma za kifedha zinazolenga kuondoa changamoto, kuanzia mikopo yenye riba nafuu, teknolojia bunifu za kidijitali na mifumo rahisi ya malipo,” amesema Zaipuna.
Zaipuna amesisitiza kuwa, mchango wa sekta binafsi, hususan wafanyabiashara wa Arusha, ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo hayo.
Aidha, amewataka wafanyabiashara kuendelea kutoa mrejesho wa huduma za benki hiyo na mapendekezo ya bidhaa mpya ili NMB ibuni suluhu zinazokidhi mahitaji yao.
Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi amesema benki hiyo yenye thamani ya hisa zaidi ya Sh 4 trilioni, ina uwezo wa kumkopesha mteja mmoja hadi Sh600 bilioni.
“Hii ni ishara kuwa tumejidhatiti kikamilifu kutoa masuluhisho ya kifedha, kuanzia mikopo ya uwekezaji, malipo ya kidijitali, huduma za bima na ushauri wa kifedha,” amesema Mponzi.
Ameongeza kuwa, uimara huo umeifanya NMB kutambuliwa kama benki salama zaidi nchini kwa miaka mitatu mfululizo na kushinda mara 11 tuzo ya Benki Bora Tanzania kutoka jarida la kifedha la Euromoney katika kipindi cha miaka 13 iliyopita.
Kuhusu huduma zinazolenga kuinua na kuimarisha sekta ya utalii nchini, Mponzi amesema NMB inatoa mikopo ya kuendeleza biashara za malazi ya wageni, ujenzi wa kambi na mahema ya kifahari (luxury tents), ununuzi wa magari ya usafiri wa watalii pamoja na mikopo ya kulipia vifaa kwa awamu kwa riba nafuu.
Mmoja wa wafanyabiashara waliohudhuria, Frank Kileo ameipongeza benki hiyo kwa ubunifu na kuendelea kuwa karibu na wadau wake kibiashara.

“Tunaona benki yenu imeendelea kuwa kinara licha ya ushindani mkubwa sokoni, jambo hili linatupa imani kama wateja wenu, na kujiona tuko salama zaidi, hivyo endeleeni kujiimarisha kukabiliana na ushindani uliopo,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa NMB, Baraka Ladislaus amesema lengo la hafla hiyo ni kusikiliza changamoto za wadau hususan wafanyabiashara, kupata mrejesho wa huduma na kutoa elimu juu ya bidhaa mpya, ikiwamo teknolojia za malipo, kadi bunifu, bima za usafiri, afya, mizigo na safari.