Mwanza. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho kimemteua mgombea urais thabiti ambaye ni kiboko na atakitetemesha Chama cha Mapinduzi (CCM).
CUF inawakilishwa na mgombea urais, Gombo Samandito Gombo na mgombea mwenza, Husna Mohamed Abdallah.
Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumapili Agosti 31, 2025 wakati akiwatambulisha wagombea hao kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela, jijini Mwanza.

Amesema wagombea hao wanazijua shida za Watanzania na wanataka kuhakikisha wananchi wanapata hali sawa na rasilimali za nchi zinanufaisha Watanzania wote.
”CCM wataanza kupata joto kwamba CUF wanatuletea mgombea thabiti mwenye uwezo wa kupambana; na chukua chako mapema. Nchi yetu iko njia panda ufisadi na rushwa vimekithiri,” amesema Profesa Lipumba.
Amesema chama hicho kilimshauri Rais Samia Suluhu Hassan kupambana na rushwa na ufisadi lakini ushauri wao ukatupwa kapuni, jambo ambalo limesababisha vilio vya wananchi kila kona ya nchi, huku akiahidi kwamba CUF itapambana na rushwa na ufisadi ambao umekithiri nchini.
”Ndugu zangu CCM hawafai, tunawaletea mgombea ameshashika jembe kwenda kulima, ameshachunga ng’ombe, ameshavua samaki. Mgombea wetu anajua matatizo ya Watanzania wa kawaida,” amesema mwenyekiti huyo.

“CCM haizungumzii utawala bora wala kupambana na ufisadi, tunawaletea mgombea atakayepambana kuleta maisha bora.”
Akimzungumzia mgombea mwenza, Husna Mohamed Abdallah ambaye hakufika uwanjani hapo kutokana na dharura, Profesa Lipumba amesema: “Tunaye mgombea mwenza, Bi Husna yeye ni mwalimu kwa taaluma, ana msimamo thabiti wa kuitetea Tanzania, anajua matatizo yanayotukabili.”
”Kwa hiyo tunawaletea timu ambayo itafanya kazi pamoja kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote,” amesisitiza Profesa Lipumba.