Rekodi ya Namungo CAF yamvutia Makambo

MSHAMBULIAJI mpya wa Namungo, Heritier Makambo amesema alichovutiwa kujiunga na Namungo ni pamoja na rekodi yao kimataifa na anatamani aandike historia nyingine akiwa na timu hiyo.

Makambo alijiunga na Namungo dirisha hili la usajili akitokea Tabora United alipofunga mabao sita na asisti nne.

Akizungumza na Mwanaspoti, Makambo amesema ukiachana na ofa nzuri aliyowekewa, lakini rekodi ya Namungo kufika makundi Kombe la Shirikisho Afrika kilimshawishi ajiunge na timu hiyo.

Ameongeza uzoefu aliokuwa nao akishirikiana na wenzake atajaribu kuipambania timu hiyo imalize nafasi nne za juu na kurejea katika michuano ya kimataifa.

“Kabla sijasaini Namungo niliuliza malengo ya timu ni nini waliponieleza nikaona wako vizuri nikajiunga nao ukiangalia wana rekodi nzuri CAF, hilo limenishawishi kwa kiasi kikubwa,” amesema Makambo na kuongeza;

“Kwa kweli kambi iko vizuri na nimeifurahia, kikubwa zaidi ni namna viongozi wanavyoelewana, wapo karibu na timu, pia kuhakikisha wachezaji wanakula kwa wakati siwezi kulinganisha  na nilipotoka ila nainjoi nikiwa hapa.”

Ameongeza, msimu uliopita hakuwa mzuri kwake, kwani akikosa muendelezo wa upachikaji mabao.

“Sikuwa na muendelezo mzuri msimu uliopita nilipoichezea Tabora United, hivyo msimu huu nataka kufanya zaidi kila ninapopata nafasi ya kufunga basi nifunge.” Amesema nyota huyo wa zamani wa Ac Horoya ya Guinea na Yanga.

Makambo kwa mara ya kwanza kucheza ligi ya Tanzania ilikuwa msimu 2018/19 akiwa na Yanga akifunga mabao 17, kisha akatimkia Horoya AC ya Guinea kabla ya kutua na kujiunga na Tabora.