NAHODHA na nyota wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga, Le Havre ya Ufaransa, Mbwana Samatta na mshambuliaji mpya wa Simba, Seleman Mwalimu ‘Gomes’ ni miongoni mwa wachezaji waliotwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichotangazwa rasmi leo Jumapili.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amekitaja kikosi hicho kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Congo Brazzaville na Niger.
Stars iliyoishia robo fainali katika michuano ya CHAN 2024 iliyofikia tamati usiku wa jana ikiwa ni ya pili kufanyika Afrika Mashariki baada ya ile ya mwaka 2016, itaanza kambi hiyo Jumanne Septemba 2, 2025, ikiwa na nyota 23 huku wanne tu wakiwa ndio wanaocheza soka la kulipwa nje.
Katika kikosi hicho, nyota wa muda mrefu Mbwana Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), Saimon Msuva (Al-Talaba SC, Iraq) wapo kuhakikisha safu ya ushambuliaji inabaki na makali yake.
Pia, chipukizi Antony Remmy kutoka Azam FC U20 amepewa nafasi ya kujumuika na wenzake, jambo ambalo linaashiria mkakati wa kujenga kizazi kipya cha wachezaji wa Stars.
“Tunapaswa kuandaa timu yenye uwiano wa uzoefu na vipaji vipya. Hii sio safari fupi, ni mwendelezo wa maandalizi ya kuhakikisha tunakuwa na kikosi chenye ushindani kila eneo. Vijana wapya watapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wakongwe kama Samatta na Msuva,” alisema kocha Morocco anayekuwa mzawa wa kwanza kuipeleka Stars CHAN na Afcon kwa mpigo.
Safu ya ulinzi inaendelea kuwa na wachezaji waliothibitisha ubora wao kwa muda mrefu kama vile Shomari Kapombe (Simba), Mohamed Hussein, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wote kutoka Yanga.
Katika eneo la kiungo kuna majina ya Mudathir Yahya, Feisal Salum na Yahya Zaid yamejumuishwa, huku kocha Morocco akibainisha wamejitahidi kufanya machaguo ya wachezaji kulingana na mipango ya mechi hizo.
“Tumekuwa tukiangalia wachezaji ambao wanaweza kutusaidia kulingana na mpango wa mechi ambazo zipo mbele yetu,” alisema Morocco, nyota wa zamani wa Coastal Union.
Katika kikosi hicho pia amejumuishwa mshambuliaji hatari wa Yanga, Clement Mzize ambaye alifunga mabao mawili katika mashindano ya CHAN.
Kwa mujibu wa benchi la ufundi, Stars itaingia kambini mapema ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa na muda mzuri wa kuzoeana na kuimarisha mbinu za uchezaji. Mechi hizo mbili dhidi ya Congo Brazzaville na Niger zinatarajiwa kuwa na umuhimu mkubwa katika mstari wa Tanzania kufuzu kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia zitakazopigwa kati ya Septemba 5 na 9.
Taifa Stars ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi E sawa na Niger ambayo ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita, kundi hilo linaongozwa na Morocco yenye pointi 15.
Kikosi kamili kilichoitwa: Makipa, Yakoub Suleiman (Simba), Hussein Masalanga (Singida BS) na Antony Remmy (Azam FC U20).
Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Wilson Nangu (Simba), Mohamed Hussein (Yanga), Pascal Msindo (Azam), Ibrahim Bacca (Yanga) na Dickson Job (Yanga).
Viungo ni Yusuph Kagoma (Simba), Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Yahya Zaid (Azam), Mudathir Yahya (Yanga), Feisal Salum (Azam FC).
Washambuliaji ni Edmund John (Yanga), Charles M’Mombwa (Floriana FC), Clement Mzize (Yanga), Abdul Hamis (Azam), Mbwana Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), Saimon Msuva (Al-Talaba SC, Iraq), Iddy Selemani (Azam) na Selemani Mwalimu (Simba).