WAKATI Simba ikitamba kuwa jezi zao mpya zinazozinduliwa leo Agosti 31, 2025 zitakuwa za ubora wa hali ya juu, mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu amewataka mashabiki na wanachama kuilinda chapa yao.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo unaofanyika leo katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki jijini Dar, Mangungu amesema kuwa jezi zao ni za hadhi ya juu na hadhi ya klabu imezingatiwa.
“Tangu awali tuliweka ahadi kwamba tunakwenda kusaini mkataba na mkandarasi wa kutafuta chapa ya kimataifa.
“Tumezingatia sana maoni, mapendekezo ya mashabiki wetu lakini sisi ni klabu inayoheshimu sana mikataba. Mimi nimshukuru sana Jayrutty na wenzako. Utaratibu sisi bodi ya wakurugenzi hatuna mkono wetu katika utengenezaji wa jezi.
“Nawaomba sana, jukumu la kuilinda chapa ya Simba sio la Mwenyekiti wa Klabu ya Simba au Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, ni jukumu la Wanasimba wote. Ninaamini kabisa bidhaa tunazitoa zitakuwa za kiwango cha kimataifa,” amesema Mangungu.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru amesema kuwa wametengeneza bidhaa bora itakayowapa thamani.
“Dhamira hii tunaenda kuionyesha kupitia jezi yetu. Kutoka kushona jezi mpaka kuvaa jezi ambayo imekidhi viwango vya ubora, Wanasimba tuna la kujivunia.
“Simba na Jayrutty tunakwenda kuonyesha moja ya bidhaa bora Afrika,” amesema Sakuru.