Taasisi za fedha zataja ushiriki matumizi nishati safi ya kupikia

Dar es Salaam. Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) unalenga kuhakikisha wananchi wanapata suluhisho la nishati ya kupikia isiyo na madhara kwa afya, gharama nafuu na isiyo na madhara kwa mazingira.

Hata hivyo, mabadiliko haya yanahitaji uwekezaji mkubwa wa kifedha ili kufanikisha upatikanaji wa teknolojia na huduma za kisasa. Mkakati huo unasema kwa kipindi cha miaka 10 utahitaji angalau Sh4.6 trilioni. Je, fedha hizi zinatoka wapi?

Katika muktadha huo, taasisi za kifedha, hususan benki, zina nafasi katika kuchangia kufanikisha mpito wa kitaifa kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia, kama ambavyo mkakati umetaja kuhamasisha ushirikiano wa wadau.

Moja ya changamoto kubwa kwa wananchi na wajasiriamali ni gharama kubwa za awali za vifaa vya nishati safi, kama majiko ya gesi, vifaa vya umeme au majiko ya kutumia nishati jadidifu.

Kama anavyoeleza Amani Zablon, mkazi wa Kinyerezi na mfanyabiashara wa chipsi, akisema anatumia mkaa katika mapishi kutokana na gharama ya gesi kuwa juu.

“Nina mtungi wa gesi mkubwa (kilo 30). Ni hasara kwenda kujaza kwa Sh50,000. Tungepata kwa gharama pungufu na hapo kwetu ingekuwa rahisi. Ukiangalia biashara zetu, hatuna mikopo, mitaji yetu ni midogo,” anasema.

Zablon anasema kama benki zitaunga mkono ajenda ya nishati safi na kukopesha teknolojia rahisi ya nishati kwa wananchi, mafanikio yatakuwa makubwa katika utekelezaji wa ajenda hiyo.

Katika kuwezesha ajenda ya nishati safi ya kupikia, benki zinaweza kutoa mikopo nafuu, mikopo ya muda mrefu, au mifumo ya malipo kwa awamu ili kuhakikisha kaya na biashara ndogo zinaweza kumudu gharama hizo. Hatua hii itasaidia kuongeza kasi ya upokeaji wa teknolojia safi miongoni mwa wananchi wa kipato cha chini.

Akizungumzia ushiriki wa taasisi za kifedha kwenye ajenda hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania, Tusekelege Mwaikasu, anasema taasisi za fedha zinaitikia ajenda hiyo kwa mtazamo chanya.

“Ikizingatiwa kuwa sote tunasonga mbele kuwa na mfumo wa fedha unaochangia maendeleo ya kiuchumi bila kuathiri vibaya mazingira au jamii, benki nyingi tayari yametenga bajeti mahsusi ili kuunga mkono dhamira hii,” anasema.

Katika kuthibitisha hilo, Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Benki ya NBC, Godwin Semunyu, anasema benki hiyo inasaidia wananchi katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia kupitia mkakati wa Sustainable Finance, yaani mfumo wa kifedha unaojumuisha maamuzi ya kifedha (kama vile uwekezaji, mikopo na biashara).

Anasema NBC imejipanga kuwa mshirika mkuu wa kifedha katika utekelezaji wa ajenda ya nishati safi, kwani inafadhili na kushiriki kwenye miradi yenye mchango wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja.

Mifano ya miradi hiyo, Semunyu anataja ni ufadhili wa miradi ya kijani kama Tanga UWASA Green Bond (Sh53.12 bilioni) inayoboresha huduma za maji safi, usafi wa mazingira na afya ya jamii.

“Pia mradi wa ubunifu wa bidhaa za kifedha kwa kaya na wajasiriamali, hususan wanawake, kununua majiko na teknolojia mbadala za nishati safi, mikopo nafuu kwa watoa huduma za nishati safi ili kupunguza gharama za usambazaji na kuongeza upatikanaji,” anasema.

Mbali na hilo, Semunyu anasema NBC imejiwekea sera maalumu ya kuzingatia athari za uwekezaji kwa miradi yote inayokopeshwa (environmental impact assessment) ili kujali mazingira.

Anaongeza kuwa benki hiyo hutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka kwa ajili ya msaada kwa jamii na utunzaji wa mazingira.

“Tunafadhili watoa huduma wa gesi na teknolojia mbadala ili kupunguza gharama za miundombinu na usambazaji, na tunashirikiana na sekta binafsi na serikali kuwezesha mitaji nafuu na uhamasishaji wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati salama na endelevu.

“Mfano, NBC imeingia makubaliano na kampuni kubwa ya usambazaji gesi majumbani kutoa mikopo nafuu kwa wasambazaji wake ili kuongeza upatikanaji kwa kaya nyingi zaidi,” anasema.

Hadi sasa, Semunyu anasema miongoni mwa mafanikio wanayoyaona katika kusukuma mbele ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ushirikiano na kampuni za nishati safi kama Taifa Gas, ambao umeharakisha upanuzi wa huduma na kupunguza gharama kwa watumiaji.

“Ufadhili wa miradi ya kijani kupitia hati fungani, ikiwemo Tanga UWASA Green Bond, umeboresha miundombinu na afya ya jamii, na ushiriki katika mijadala na majukwaa ya kitaifa kuhusu nishati safi na mabadiliko ya tabianchi umeongeza uelewa wa sekta ya kifedha kuhusu uwekezaji endelevu,” anasema.

Semunyu anasema ahadi ya benki hiyo kwa wananchi ni itaendelea kuwezesha fedha nafuu kwa miradi ya nishati safi, kushirikiana na serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, na kuendesha kampeni za uelimishaji na kuendeleza bidhaa za kifedha zinazochochea matumizi ya nishati safi nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Miradi na Programu za Fedha Endelevu wa Benki ya CRDB, Stanley Kinemelo, anasema benki hiyo ilizindua Green Bond (hati fungani ya kijani), ambapo fedha zinazokusanywa ni kwa ajili ya miradi rafiki kwa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Kupitia hati fungani hiyo, tutazindua huduma nyingine ambayo itajikita kwenye masuala ya nishati safi pekee. Hii itajikita hasa kwenye nishati safi ya magari, tukiangalia si tu magari kutumia mafuta, ila yawe kwenye mfumo wa kutumia umeme,” anasema.

Kinemelo anasema mbali na hatua hiyo, wanashirikiana na mashirika ya kimataifa yanayotoa mikopo kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Pia CRDB tunalenga kampuni kubwa zinazotumia nishati ya kuni kubadili mifumo yake kutumia nishati safi, ikiwemo gesi,” anasema.

Ukiwa ni muendelezo wa taasisi za kifedha kushiriki katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Januari 27, 2025, Benki ya NMB ilizindua mpango wa mikopo ya Sh100 bilioni kwa ajili ya kusaidia biashara na miradi ya kusambaza nishati safi ya kupikia nchini.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, kwenye hafla hiyo Januari mwaka huu, anasema msukumo wa benki hiyo kutenga kiasi hicho cha fedha kukopesha makundi hayo unalenga kuwezesha utunzaji wa mazingira, pia kuboresha afya na ustawi wa jamii, kukuza uchumi na kuchangia kufikiwa kwa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030.

Anasema NMB inatambua umuhimu wa kuungana na Serikali kufanikisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi.

“Benki ya NMB itatumia mpango wa NMB Kijiji Day kwa kushirikiana na kampuni ya Taifa Gas kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vijiji 2,000 mwaka 2025,” anasema.

Mradi huo wa mikopo ni hatua muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanapata nishati salama na nafuu kwa matumizi ya nyumbani. Pia utachochea maendeleo ya sekta binafsi kupitia biashara za usambazaji wa mitungi na majiko ya gesi.

“Kama mfanyabiashara ninayetumia nishati kwenye shughuli zangu, nimeona kwa macho yangu changamoto kubwa inayowakabili wananchi wengi gharama ya awali ya kununua vifaa kama majiko safi, mitungi ya gesi au mifumo ya nishati jadidifu,” anasema Peter Michael, mkazi wa Kimara Suka, Dar es Salaam.

Michael anasema watu wana hamu ya kubadilisha mfumo wao wa kupikia, lakini hawana uwezo wa kulipia kwa mara moja.

Anasisitiza mikopo nafuu kutoka benki ingeondoa kikwazo hiki na kuwawezesha familia nyingi kuanza safari ya kutumia nishati safi bila mzigo mkubwa wa kifedha.

Naye Hussein Juma, mkazi wa Tandika na mjasiriamali, anasema kwa kupewa nafasi ya mafunzo ya namna ya kuendana na ajenda hiyo, wanaweza kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi, kuajiri vijana na kuongeza kipato cha familia.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917