Taharuki Kariakoo, moto ukiteketeza duka moja kati ya 100

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kariakoo leo wamekumbwa na taharuki baada ya moto kuzuka katika jengo moja lililopo katika makutano ya mitaa ya Aggrey na Sikukuu na kuharibu chumba kimoja cha duka kati ya vyumba 100 vilivyopo katika jengo hilo.
Tukio hilo limetokea leo Agosti 31, 2025 saa 5:30 asubuhi na kuwashtua wafanyabiashara na wateja waliokuwa wakiendelea na shughuli zao, huku moshi mzito ukitoka kwenye jengo hilo.

Akizungumza na Mwananchi shuhuda wa tukio hilo, Hassan Mdoe amesema waliona vumbi la mfuko wa saruji na hawakuzingatia kwa kuamini ni kawaida kwa maeneo hayo kutokea jambo hilo kutokana na ujenzi unaoendelea.

“Tulivyoona lile vumbi tukachukulia ni kawaida tukaendelea na biashara zetu lakini ghafla tukaona moshi mweusi na wamachinga wanaouza hapa chini wanakimbia na kupiga kelele za moto,” amesema Mdoe.

Amesema kesho ndiyo ilikuwa uzinduzi rasmi wa maduka hayo hivyo baadhi ya wapangaji walishaweka vitu vyao kwa ajili ya biashara.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, (SACF) Peter Mabusi, amesema moto huo umetokea saa 5 asubuhi na kuunguza chumba kimoja kilichokuwa na mali.

“Kikosi kiliwahi kufika katika eneo la tukio na kufanikiwa kuzima moto huo japokuwa chumba kimoja kilishaungua hivyo walijitahidi kuzima,” amesema Kamishna Mabusi.

Hata hivyo, Mwabusi amesema chanzo cha moto bado hakijafahamika, hivyo ameagiza timu yake ya uchunguzi kuendelea kufuatilia na kujua kilichosababisha tukio hilo.
Mabusi amewataka wafanyabiashara na wapangishaji kuepuka kutumia majengo yasiyo salama, akisema ingawa changamoto ya upatikanaji wa maduka ipo, kuendelea kufanya biashara katika mazingira hayo kunaweza kuwasababishia hasara kubwa zaidi.

Kufuati hali hiyo,  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi amesema kutokana na mfululizo wa matukio ya moto ameitisha kikao Septemba 3, 2025 cha wamiliki wa majengo ya Kariakoo, Zimamoto na Uokoaji, Tanesco na Halmashauri.

Amesema kikao hicho kinalenga kuangalia namna za kukabiliana na mwendelezo wa majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara Kariakoo.

“Kuna haja ya kufanya kikao tuone tunatokaje hapa maana inaanza kidogo kidogo mwisho wa siku litatokea kubwa, hivyo kikao hiki kitatupa tathimini tunatokaje katika eneo hili na nini kifanyike,” amesema Mushi.

Wakati Mushi akisema  hayo Mei 5, 2025 katika uwasilishaji wa wa bajeti ya wizara ya ujenzi ya mwaka 2025/26 Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega alisema wizara hiyo inatunga sheria ya majengo kwa ajili ya kusimamia sekta ndogo ya majengo nchini