Tanzania ya pili Kombe la Dunia la vijana wa mazingira magumu

Timu ya Tanzania ya Wanawake kutoka kituo cha Future Stars Academy cha jijini Arusha, imeshika nafasi ya pili katika michuano ya vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu (Homeless World Cup) yaliyofanyika kati ya Agosti 22-30 jijini Oslo, Norway, yakishirikisha timu 60 kutoka mataifa 48.

Future Stars Academy imetwaa nafasi hiyo baada ya kushinda mchezo wa fainali ya daraja la pili la michuano hiyo dhidi ya Austria kwa mabao 5-4. Mabao ya Tanzania yalifungwa na Loyce Dismas, Susan Michael, Varian Issa na Sarah Jacob. 

Mshindi wa kwanza wa jumla kwa timu za wanawake ilikuwa Uganda iliyoshinda fainali ya daraja la kwanza dhidi ya Romania. 
Kenya ilimaliza ya tatu baada ya kushinda fainali dhidi ya Mexico katika daraja la tatu la michuano hiyo. 

Kwa upande wa timu za wanaume, Misri ilichukua ubingwa wa jumla huku Ureno ikishinda l daraja la pili na Poland katika daraja la tatu. Tanzania haikuwakilishwa na timu ya wanaume. 

Michuano hiyo ya timu za wachezaji wanne-wanne huanza kwa raundi ya kwanza katika makundi ambapo washindi wa kwanza huingia raundi ya pili ya makundi katika daraja la kwanza; washindi wa pili huingia kwenye makundi ya daraja la pili na washindi wa tatu kwenye makundi ya daraja la tatu. 

Katika raundi ya pili timu huchuana tena hadi kufikia fainali ya kila daraja ambapo mshindi wa daraja la kwanza hutangazwa bingwa wa jumla; mshindi wa daraja la pili huwa mshindi wa pili wa jumla na mshindi wa daraja la tatu huwa mshindi wa tatu wa jumla. Tanzania imeshinda kwenye fainali ya daraja la pili.

Mashindano haya huandaliwa kila mwaka na taasisi ya Homeless World Cup yenye makao yake makuu nchini Uholanzi ikishirikiana na shirika la Salvation Army. 

Balozi wa Tanzania anayewakilisha katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, Mobhare Matinyi, aliwapongeza vijana hao kwa ushindi walioupata na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa walikuja wanne tu bila mchezaji wa akiba hata mmoja.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu timu ya Tanzania kushiriki mashindano haya ambayo mwakani yatafanyikia nchini Mexico.