Tido akumbuka rekodi ya Bayi, akitaja riadha ilivyoibeba nchi

Mwandishi wa habari nguli, Tido Mhando ameeleza kumbukumbu ya miaka 52 ya nguli wa riadha, Filbert Bayi akibainisha namna alivyoibeba nchi enzi zake.

Tido amebainisha hayo jana Agosti 30, katika mahafali ya Shule ya Msingi na Sekondari za Filbert Bayi, yaliyofanyika kwenye ‘Campus’ ya Kibaha.

Tido aliyekuwa mgeni rasmi,  alishuhudia utoaji wa tuzo mbalimbali za kitaaluma na michezo zilizotolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri wa shule hizo.

“Sina shaka na taaluma ya shule, sababu historia ya matokeo yake inathibitisha hilo, katika michezo pia ni shule ambayo inatoa fursa kwa vipaji, imejidhatiti kama ilivyokuwa kwa muasisi wake,” amesema Tido.

Akisimulia namna alivyokutana na Bayi, Tido amesema ilikuwa mwaka1973, yeye (Tido) akiwa mwandishi wa habari na kwenda Kibaha kuangalia mazoezi ya wanariadha.

TID 01

“Nilikuta kijana mmoja anakimbia sana , nikaambiwa ndio Bayi, alikwenda katika mashindano ya Afrika na kufanya vizuri, wakati huo riadha ndiyo ilikuwa ikitamba sana, katika soka Simba na Yanga zilikuwepo lakini wanariadha ndio walituletea heshima sana.

“Mwaka1974 nilipewa nafasi kwenda na timu ya Tanzania katika michezo ya Jumuiya ya Madola, Newzealand, katika michezo ile mbio za 1500 zilikuwa zikizungumzwa sana.

“Ushindani ulikuwa mkali wakitajwa mwenyeji,

John Walker aliyeshikilia rekodi dunia na Mkenya John Jipcho, siku ya fainali sikupata usingizi hadi asubuhi, nilikuwa na hamasa kuliko hata Bayi mwenyewe.”

Amesema wakati mbio inaanza, Bayi alichomoka moja kwa moja.

TID 02

“Kwa muda ule nilipata taharuki,  sikuwa na uwezo wa kusema naweza kuona nini, Bayi alishinda tena kwa kuvunja rekodi ya dunia.

“Baada ya ushindi ule, waandishi wa habari wa nchi tofauti  walimzunguka, lakini Bayi alinitafuta mimi kwanza na kutoa salamu kwa Watanzania, aliipa heshima Tanzania na hadi sasa anaiendeleza kwa watoto wa Kitanzania ambao anawapa ofa za kimasomo wale wenye vipaji shuleni kwake,” amesema Tido.

Akizungumzia hilo, Bayi amesema, Tido ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati  ya Waandishi wa Habari akiwa mwandishi wa habari, yeye ndipo aliweka rekodi ya dunia, akiishuhudia.

“Wakati huo ni kweli riadha ilikuwa ikifanya vizuri kimataifa, kutokana na maandalizi tuliyopewa kama nchi, nataka kuirejesha rekodi hiyo kupitia vipaji vilivyopo shuleni hapa,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi za Filbert Bayi, Elizabeth Mjema amesema mahafali hayo yamehusisha wanafunzi wa Shule ya Msingi  Filbert Bayi za Kibaha, Pwani na Kimara Dar es Dar es Salaam,  sanjari na Sekondari.

TID 03

Amesema shule hiyo mbali na kufanya vizuri kitaaluma, pia inaprogramu za michezo na vijana wake wamekuwa wakifanya vizuri kitaifa (Umisseta) na kimataifa (Feassa) wakiiwakilisha nchi vema.

Katika mahafali hayo, ilifanyika programu ya soka kwa wanafunzi kuwa na timu mbili za wapenzi wa Yanga na Simba na kuchuana ambako upande wa Yanga uliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na mchezaji aliyejitambulisha kwa jina la utani la Prince Dube.