Katika maisha ya ndoa, hakuna jambo zuri kama kuwa na mwenza unayependana naye kwa dhati, lakini pia hakuna changamoto kubwa kama kushughulika na watu wasiokutakia mema uhusiano huo.
Watu hawa, mara nyingi huingia katika maisha ya wanandoa kama marafiki, ndugu, au hata majirani, lakini lengo lao si jema. Ni muhimu sana kutambua na kujua dalili za watu hao ili kulinda ndoa yako isiathiriwe au kuharibiwa kabisa.
Watu wasioitakia mema ndoa yako si lazima waonyeshe uovu wao waziwazi. Mara nyingi hujificha nyuma ya tabasamu, maneno ya busara, au hata msaada wa hapa na pale. Wanajua jinsi ya kujifanya wana nia njema ilhali wanachofanya ni kuchochea migogoro, kueneza fitina au kuingiza chuki kati yako na mwenza wako.
Kujua madhara ya uhasidi, hii hapa simulizi ya Furaha Hatuna, mkazi wa jijini Mwanza, anayeelezea namna rafiki yake alivyomfanyia hasadi katika ndoa yake hadi kufikia hatua ya kuachwa na mumewe.
“Nilifunga ndoa na mume wangu tulipendana na kushirikiana kwa karibu. Hata hivyo, hali hiyo ilianza kubadilika baada ya Amina aliyekuwa rafiki yangu wa karibu kuanza mazoea na mume wangu pamoja na kujihusisha sana na familia yetu.
Amina alianza kunitembelea mara kwa mara, akijifanya rafiki mwaminifu kumbe nyuma ya pazia, alikuwa akimweleza Ali (mumewe) maneno ya kunichonganisha naye.
Mara kadhaa alimwambia nimekuwa nikizungumza na wanaume wengi sokoni na kwamba ana siri nyingi za mabwana zangu. Mimi sikujua chochote na nilikuwa nikimshirikisha mtu niliyedhani rafiki yangu changamoto ndogondogo za ndoa nikitarajia kupata faraja.
Lakini ushauri nilioupokea ulikuwa wa kuvunja siyo kujenga, bahati mbaya nilikuja kujua baada ya ndoa yangu kuvunjika.
“Amina alikuwa ananiambia kwamba mume wangu ana mwanamke mwingine na kuwa ni bora nijifanye mgumu na kuonyesha hasira. Alijua wazi kuwa maneno hayo yangewasha moto ndani ya ndoa, lakini alinishauri.
Kwa maneno ya uongo yaliyosambazwa na Amina, ndoa yangu ilianza kuyumba. Mume wangu alianza kunituhumu kwa mambo ambayo hayakuwepo, huku na mimi nikianza kudhani ana uhusiano wa nje. Ugomvi wa mara kwa mara ukawa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Amina alijua kila kitu kilichotokea nyumbani kwangu kwa sababu nilimuamini kama dada. Lakini kumbe alikuwa akitumia siri hizo kuniharibia,”
Baada ya miezi kadhaa ya migogoro mikali, Ali alifikia hatua ya kunipa talaka. Wiki chache tu baada ya talaka hiyo, taarifa zilisambaa kwamba ameoa tena na mke mpya si mwingine bali ni rafiki yangu niliyejuwa ni ziadi ya ndugu kwangu. Niliumia sana sitoweza kumsamehe.”
Kutambua watu hawa mapema ni silaha muhimu ya kulinda amani na uhusiano wa ndoa yako.
Dalili moja kuu ya watu hawa ni kuingilia uamuzi wa ndoa yako bila kuombwa ushauri.
Kwa mfano, rafiki au ndugu anayejaribu kila mara kumpotosha mwenza wako au kukupotosha wewe kuhusu mwenza wako, hasa kwa kutumia maneno kama, “Mimi siingilii ndoa ya mtu, lakini…” ni lazima umchunguze kwa makini.
Mara nyingi huanza kwa ushauri mdogo lakini baadaye wanageuka kuwa chanzo cha migogoro mikubwa. Hawa ni watu wanaotaka kuonekana kuwa na maarifa kuhusu ndoa yako kuliko hata mke au mume wako mwenyewe.
Wengine ni wale wanaoshabikia migogoro yenu badala ya kuwatuliza au kuwaombea suluhisho. Kwa mfano, mtu anayefurahia unapoeleza matatizo ya ndoa yako, na kisha anakuongezea hasira badala ya kukushauri kutafuta suluhu, huyo hana nia njema. .
Mtu wa aina hii anaweza kukuambia, “Huyo si mtu sahihi kwako,” au “Kama angekupenda kweli asingekufanyia hivyo,” bila hata kujua upande wa pili wa hadithi. Hawa ni watu wanaopanda mbegu ya talaka kwa njia ya maneno mepesi lakini yenye sumu kali.
Wengine hujificha kama marafiki wa karibu sana. Kwa mfano, rafiki wa kike au wa kiume wa zamani wa mwenza wako ambaye anajifanya hana hisia zozote, lakini mara kwa mara anawasiliana, anatoa zawadi, au hata kukaribisha mazungumzo ya faragha na mwenza wako, huyo pia anaweza kuwa hatari kwa ndoa yako.
Watu hawa hutumia urafiki wa zamani kama kivuli cha kuingilia ndoa yenu. Wanapandikiza hisia, mashaka, au hata vishawishi vya kimapenzi vinavyoweza kuivuruga ndoa.
Pia, kuna wale wanaotumia mitandao ya kijamii kuingilia ndoa ya mtu. Wanaweza kuwa marafiki wa mtandaoni wanaojifanya kutoa maoni ya kawaida lakini kwa lengo la kumvutia mwenza wako.
Kwa mfano, mtu anayemwandikia mwenza wako ujumbe wa mapenzi au kumsifia kupita kiasi mbele ya macho yako au kwa siri, huo ni uhasidi wa moja kwa moja.
Kuna tofauti kati ya sifa ya kawaida na ile yenye nia ya kumvuta mtu kutoka kwenye ndoa yake.
Mahasidi wengine wanajificha katika familia au ukoo. Hawa ni hatari zaidi kwa sababu ni vigumu kuwaepuka. Wanaweza kuwa mama, baba, au ndugu wa karibu wanaoamini kuwa huchangia sana kwenye uamuzi wa ndoa yako. Mtu wa familia anayesema, “Mimi ndiye niliyekulea, usiache mume/mke wako akubadilishe,” anaweza kuleta mgawanyiko mkubwa.
Ingawa nia yao inaweza kuonekana kuwa ya kusaidia, mara nyingi huchochea hisia za ubaguzi au mapendeleo ambayo huleta uhasama kati ya wanandoa.
Namna nyingine ya kuwatambua ni kwa kuona jinsi wanavyojibu habari njema kuhusu ndoa yako. Mtu ambaye haonyeshi furaha unapofanikisha jambo na mwenza wako, au ambaye anabeza mafanikio yenu kama wanandoa, huyo ni lazima umchunguze. Watu hawa mara nyingi huzungumza kwa kejeli au kusambaza uvumi unaodhoofisha hadhi ya mwenza wako au ndoa yenu kwa ujumla.
Njia mojawapo ya kujikinga dhidi ya watu hawa ni kuweka mipaka ya mawasiliano na ushirikiano. Sio kila mtu anatakiwa kujua hali ya ndoa yako, changamoto zenu, au mafanikio yenu.
Weka siri zako ndani ya ndoa, zungumza na mwenza wako moja kwa moja, na tafuta msaada wa kitaalamu endapo kutakuwa na changamoto kubwa. Marafiki au ndugu wasio waaminifu wanaweza kutumia taarifa zako kwa ajili ya uharibifu.
Zaidi ya yote, maombi na maarifa ya kiroho ni silaha kuu dhidi ya mahasidi wa ndoa. Wengine ni wa kiroho, hutumwa na nguvu za giza ili kuharibu misingi ya ndoa za watu.
Maombi ya pamoja kama wanandoa, pamoja na imani madhubuti kwa Mungu, husaidia kuweka ulinzi dhidi ya nguvu hizi.
Pia ni muhimu kuwa na marafiki wa ndoa, yaani wanandoa wengine wanaotamani mema na ambao ni mfano mzuri wa ndoa zenye afya.
Kama mume au mke, ni muhimu kuwa na mawasiliano ya wazi, uaminifu, na upendo wa dhati kwa kila mmoja. Ukiona mwenza wako anaanza kushawishika na maneno ya watu wa nje, usimshambulie bali zungumza naye kwa upole na mueleweshe hatari ya kushirikisha watu wasiowafaa.
Ndoa ni uwanja wa kazi ya pamoja, na kila mmoja anapaswa kujua kuwa kuna watu hawatafurahia mafanikio yenu.
Ni muhimu kuelewa kuwa mahasidi wa ndoa hawavai sare za uadui. Mara nyingi huja kama marafiki, washauri, au hata watoa msaada.
Lakini kwa jicho la ndani, na kwa kutumia hekima, unaweza kuwajua.
Ni jukumu lako kama mwenza kuwa mlinzi wa ndoa yako na kuhakikisha kuwa unazuia kila chembe ya sumu ya uhasidi kabla haijaota mizizi.
Ndoa ni safari, na kama safari nyingine yoyote, kuna vikwazo, vishawishi, na maadui wa mafanikio. Lakini kwa upendo, busara, na imani, kila kikwazo kinaweza kushughulikiwa na kufutwa.
Unadhani ni nani kwenye maisha yako ambaye amewahi kuonyesha tabia ya namna hii?