‘Utapeli ni tishio la ukuaji wa huduma za kifedha kimtandao’

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa kadri huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali zinavyokuwa, ndiyo utapeli na ulaghai unavyozidi kuongezeka katika eneo hilo ambalo limebadilisha mambo mengi kwa namna chanya na kurahisisha maisha ma biashara za watu.

Wataalamu wa sekta ya fedha wanasema endapo utapeli na ulaghai mtandaoni usipodhibitiwa unaweza kupunguza imani ya wananchi kwenye mifumo ya kifedha, jambo linaloweza kudhoofisha kasi ya ujumuishaji wa kifedha.

Ni kwa sababu hiyo, mawakala na watoa huduma za kifedha nchini wamehimizwa kuendelea kujiendeleza na kukumbatia teknolojia za kisasa ili kutambua mbinu mpya zinazotumiwa na matapeli wa mtandaoni na hivyo kuwalinda wateja wao.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 31, 2025 katika mkutano wa mawakala wa miamala ulioandaliwa na Benki ya Equity, Mkuu wa Kitengo cha Malipo wa benki hiyo, Haidary Chamshama amesema sekta ya kifedha inakuwa imara kama watoa huduma wa mstari wa mbele watakuwa na uelewa wa kina wa mbinu za kudhibiti utapeli.

“Matapeli wa mitandaoni wanabadilisha mbinu kila siku. Ili kuhakikisha usalama wa wateja na uthabiti wa mifumo yetu, ni lazima mawakala waendelee kupata mafunzo ya mara kwa mara ya kutambua viashiria vya utapeli mapema na kuvikabili kabla havijaathiri huduma,” amesema Chamshama.

Amebainisha kuwa mkutano huo utawajengea uwezo mawakala uwezo wa kutambua viashiria vya utakatishaji fedha na namna ya kukabiliana navyo. 

 “Miamala inayojirudia mara kwa mara bila maelezo ya msingi au inayokinzana na tabia ya kawaida ya mteja ni dalili muhimu za kuangaliwa. Tunapaswa kuwa macho zaidi,” amesema.

Chamshama amesisitiza kuwa Equity itaendelea kushirikiana na wadau wengine, ikiwamo taasisi za Serikali na vyombo vya usimamizi na kuhakikisha elimu ya usalama wa kifedha inawafikia mawakala wengi zaidi nchini akisema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya benki hiyo kujenga mazingira salama ya huduma za kifedha ili kuongeza imani ya wateja na kukuza ujumuishaji wa kifedha.

Chacha Magaigwa, mmoja wa mawakala walioshiriki, amesema elimu aliyoipata itamsaidia kuboresha huduma kwa wateja kwa njia salama zaidi.

“Sisi ndio tunakutana na wateja uso kwa uso, hivyo tukipewa elimu ya namna ya kutambua mbinu za utapeli tunakuwa nguzo ya kwanza ya ulinzi. Lakini elimu hii inapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara kwa sababu wahalifu hubadilisha mbinu kila siku,” amesema.

Takwimu zilizopo zinaonesha hivi sasa Tanzania ina zaidi ya watumiaji milioni 35 wa huduma za fedha kwa njia ya simu na idadi hiyo inaendelea kukua kwa kasi, hata hivyo, ukuaji huo umekuwa pia kivutio kikubwa kwa wahalifu wa mtandaoni wanaoangalia mianya ya kunufaika kupitia ulaghai.

Wachambuzi wa uchumi wanasema endapo vitendo vya utapeli wa mtandaoni havitadhibitiwa, vinaweza kupunguza kasi ya wananchi kuamini mifumo rasmi ya kifedha, hali itakayodhoofisha uwekezaji na ukuaji wa sekta kwa jumla.

Wanasema usalama wa kifedha ni jambo la kiuchumi na si la kiusalama pekee.