Dar es Salaam. Wahitimu 50 wa kidato cha sita wamechaguliwa kupata ufadhili wa masomo nje ya nchi kupitia mpango wa ‘Samia Scholarship Extended’, unaolenga kukuza wataalamu wabobezi katika fani za Sayansi ya Data, Akili Bandia (AI) na Sayansi Shirikishi.
Akizungumza Agosti 31, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema jumla ya waombaji 96 waliwasilisha maombi kati ya 100 waliobainishwa kuwa na vigezo, wakiwemo wasichana 13. Uteuzi wa waliopata ufadhili umezingatia ufaulu wa juu katika masomo ya hisabati na fizikia.
Profesa Nombo ameeleza kuwa mchakato wa uteuzi ulifanyika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), huku majina ya waliofaulu yakiwa tayari yamewekwa kwenye tovuti za taasisi hizo.
Aidha, wahitimu waliopata ufadhili watawekwa kwenye kambi maalum ya maarifa kwa miezi 10 kuanzia Septemba 15, 2025, itakayowekwa NM-AIST, ambako watapewa mafunzo ya awali ya sayansi na teknolojia, uongozi, lugha, na utamaduni wa nchi wanazotarajia kwenda kusoma.
Kwa waliokosa nafasi hiyo, amesema bado wanaweza kupata ufadhili kusomea ndani ya nchi kupitia mpango wa awali wa Samia Scholarship. Profesa Nombo amebainisha kuwa kati ya waombaji 96, wahitimu 91 tayari wameomba udahili kwenye vyuo vya ndani.
‘’Waombaji walielekezwa kuomba pia udahili na ufadhili kwa vyuo vya ndani. Aidha, wizara imejiridhisha kuwa kati ya waombaji 96 waliowasilisha maombi yao waombaji 91 waliomba udahili katika vyuo vikuu vya Tanzania”amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Costech, Dk Amos Nungu, amesema lengo kuu la ufadhili huu ni kuhakikisha Tanzania inazalisha wataalamu wa kimataifa katika nyanja muhimu za kisayansi, huku ikiweka mkazo kwa jitihada za kuongeza ushiriki wa wasichana katika masomo ya sayansi.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha wasichana wanajitokeza na kunufaika zaidi na fursa mbalimbali zinazopatikana katika uga wa sayansi na teknolojia.
Amesema miongoni mwa jitihada hizo ni kuhamasisha wasichana kusoma masomo ya sayansi, ujenzi wa shule za wasichana pamoja na kuendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji haswa katika upande wa sayansi na teknolojia.