Wakati upi sahihi mzazi ‘kuingilia’ ndoa ya mwanawe?

Ndoa, kwa mtazamo wa kitamaduni na kidini, mara nyingi huonekana kama muungano wa watu wawili waliovuka mipaka ya familia walizotoka.Mara mtoto anapooa au kuolewa, inakubalika kuwa rasmi anaingia katika makubaliano yanayomtenganisha na wazazi wake na kumuunganisha na mtu mwingine anayewajibika kwake.Hili linatokana na imani kwamba ndoa ni taasisi huru ambapo wazazi hawapaswi kuingilia maamuzi ya wanandoa isipokuwa wameombwa.
Hata hivyo, swali la msingi ni: Je, uhuru huu wa wanandoa kujitegemea hauna kikomo? Simulizi ya mzazi aliyefanya juhudi kumsomesha binti yake na kuishia kugeuzwa kuwa mama wa nyumbani linatuchochea kufikiri zaidi.Je, mzazi ana wajibu wa kusema au anapaswa kukaa kimya kuheshimu mipaka yake?
 Haja ya uhuruUhuru wa wanandoa kuamua mambo yao ni suala la msingi. Kwanza, unakuza uaminifu na uwajibikaji kati yao. Pili, unawapa fursa ya kujifunza kutatua migogoro yao wenyewe, jambo linaloweza kuimarisha uhusiano wao.Tatu, uhuru huu unawasaidia kujenga utambulisho wao wa pamoja kama familia mpya, tofauti na familia walizotoka.
Hata hivyo, swali linabaki:Je, ni sawa kuwaacha wanandoa kuwa na uhuru hata katika mazingira ambapo mmoja wao ananyanyasika?
Mzazi kulinda uwekezaji wake
Wazazi wengi, hasa katika jamii za Kiafrika, wamewekeza rasilimali nyingi—muda, pesa, na hata nguvu—kumsomesha mtoto wao.Mzee katika simulizi alisema wazi kwamba alijinyima mambo mengi ili binti yake apate elimu ya juu. Elimu aliyoipata binti si tu ilikuwa cheti bali zana ya kujitegemea na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nyumba yake.Je, ni sawa kumzuia mke kufanya kazi kwa hoja kwamba wajibu wake wa msingi ni kulea watoto? Hata kidogo.Katika mazingira ambayo mtu ananyimwa kutumia maarifa yake kuisaidia jamii, ni sahihi mzazi wake kupata wasiwasi na kuingilia.
Hata hivyo, kuingilia ndoa ya mwanae kunahitaji busara kubwa.Mzazi hapaswi kuingilia maisha ya ndoa kwa amri. Imeanndikwa ndoa na iheshimiwe na watu wote. Badala yake, anaweza kutoa ushauri kwa heshima, akizingatia mipaka yake.Kwa mfano, mzazi anaweza kuzungumza na mwanae moja kwa moja, akimuuliza kuhusu hisia zake na maamuzi yaliyofanywa.Ikiwa mwanae anaona kwamba maamuzi ya mume yanaingilia haki zake, mzazi anaweza kusaidia kwa kutoa ushauri usiozalisha migogoro zaidi.
 Wakati wa KuingiliaKuna hali ambazo kuingilia kwa mzazi sio tu jambo la haki bali ni wajibu. Hali hizi ni pamoja na pale ambapo kuna udhalimu wa wazi, kama vile unyanyasaji wa kimwili, kiakili, au kiuchumi.Katika kesi ya mzee, kumudu mwanamke kazi yake kunaweza kuonekana kama aina ya udhalimu wa kiuchumi, hasa ikiwa mwanamke huyo alikuwa na shauku ya kazi yake na alikuwa akichangia maisha ya familia. Mzazi ana haki ya kuingilia pale ambapo maisha au staha ya mwanae iko hatarini.
Vilevile, mzazi anaweza kuingilia pale ambapo kuna ushahidi wa wazi wa kuvunjwa haki za msingi za mwanae.              
Haki za msingi hapa zinajumuisha haki ya kufanya kazi, haki ya kuheshimiwa, na haki ya kuishi maisha yanayotimiza ndoto zake.Ikiwa mume anatumia mamlaka yake kuzuia haki hizi, mzazi anaweza kuingilia kwa kutoa ushauri au hata kusaidia mwanae kupata msaada wa nje.
 Usawa wa KijinsiaMjadala huu pia unagusa suala la usawa wa kijinsia. Kumzuia mwanamke kufanya kazi kwa sababu ya imani kwamba “heshima ya mwanamke iko katika malezi ya watoto” ni dalili ya mfumo dume unaoendelea kuwepo katika jamii yetu.Hili linadhihirisha umuhimu wa wazazi kuingilia pale ambapo maamuzi yanayofanywa yanapingana na kanuni za usawa wa kijinsia.   Mzazi anaweza kuwa na jukumu la kuelimisha jamii, ikiwa ni pamoja na mume wa mwanae, kuhusu umuhimu wa kulinda haki za wanawake za kufanya kazi na kutimiza ndoto zao.
Hata hivyo, kuingilia hakuwezi kuwa kwa njia ya jeuri.Mzazi anapaswa kutumia busara kuweka mazingira ya kuchochea uelewa wa usawa wa kijinsia. Mzazi, mathalani, anaweza kuwaalika wanandoa kwenye semina zinazojadili mada za usawa au kuwapa vitabu vinavyohusiana na mada hiyo.
 TunachojifunzaMzazi kuingilia ndoa ya mwanae ni suala nyeti linalohitaji busara. Mzazi ana haki ya kuingilia pale ambapo ndoa inaingilia haki ya mmoja wapo kufikiri kwa uhuru, kuishi ndoto zake na kuheshimiwa. Kusema mzazi hawezi kuingilia ndoa ya mwanae katika mazingira ambayo mtoto ananyanyasika ni kutokuelewa ukweli kuwa uchungu wa mwana aujuaye mzazi na kwamba mtoto kwa mzazi hakui.Mzazi ana haki ya kuuliza maswali magumu na kumsaidia mwanawe kupata haki yake. Hata hivyo, ni muhimu hili likafanyika bila kuvunja heshima ya ndoa.