WALIMU WA NGUMI 29 KUTOKA TANZANIA WAFAULU MAFUNZO YA KIMATAIFA YA NYOTA MOJA


30-08-2025, Dar es salaam.
WALIMU  wa mchezo wa ngumi 29 kutoka Tanzania wamefaulu mafunzo ya kimataifa ya Ualimu ya IBA nyota 1 katika mafunzo yaliyofanyika kuanzia tarehe 28-07-2025 mpaka 06-08-2025.
Ni historia kubwa katika tansia ya mchezo wa ngumi nchini Tanzania kwa kupata idadi kubwa ya wahitimu wa kimataifa kwa wakati mmoja toka nchi kupata uhuru, yote yakitokea chini ya uongozi dhabiti wa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) Ndg. Lukelo Willilo (kwenye picha)
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na mkufunzi mkuu wa IBA na Chama cha ngumi bara la Ulaya (EUBC) Dr. Gabriel Martelli yalishirikisha jumla ya walimu wa ngumi 36 kutoka mataifa matano (5) huku Tanzania ikiwakilishwa na walimu wa kutoka ngumi za ridhaa na za kulipwa kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania pamoja na nchi zingine za Malawi (1), Comoros (1), Ethiopia (3) na Bangladesh (1).
“Ni jambo la kujivunia sana kwangu na wasaidizi wangu wote katika Shirikisho kwa hatua kubwa tunazoendelea kuzifanya za kuleta maendeleo katika michezo nchini Tanzania, lakini hasa katika kutekeleza ahadi zetu kwa vitendo na maelekezo ya Serikali yetu ya awamu ya sita iliyo chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kuhakikisha tunawaendeleza wataalumu wa michezo hasa katika ngazi za Kimataifa” alinukuliwa Rais wa BFT Ndg. Lukelo Willilo.
Hii ni mara ya pili katika kipindi kifupi baada ya kufanyika kwa mara ya kwanza nchini mafunzo mengine ya Kimataifa ya Waamuzi na Majaji (R&Js) yaliyofanyika Dar es salaam August, 2024 ambapo jumla ya Watanzania 26 walifanikiwa kuhitimu na kufaulu ngazi ya nyota 1 ya Kimataifa.
Hafla maalumu ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu itafanyika hapo baadae.