Wasira awataka wanachama CCM kuacha makundi

Arusha. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho kuacha makundi yaliyotokana na mchakato wa ndani wa chama wa kura za maoni kuwapata wagombea wa ubunge na udiwani.

Amesema hayo leo Jumapili, Agosti 31, 2025, alipozungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali za CCM jimbo la Arusha Mjini na baadhi ya majimbo jirani, yakiwamo ya Monduli, Arumeru Magharibi na Arumeru Mashariki.

Wasira amesema makundi yanayotokana na kura za maoni ndani ya chama husababisha wapinzani kupita katikati ya mgawanyiko huo.

“Tatizo letu ni la makundi ambayo yametokana na mfumo wetu wenyewe, ambapo tumejiwekea kwamba tutapata mgombea wa udiwani na ubunge kwa njia ya kura za maoni. Huu ni utaratibu wetu unaoendelea, unapiga kura halafu unarudi nyumbani. Uliyempigia hakushinda, unanuna.

“Kwa hiyo, kama ulikuwa na mgombea lakini hakufanikiwa, bado wewe ni mwanachama wa CCM, huwezi kupoteza lengo kwa sababu kura ya maoni imeenda kama ilivyopangwa,” amesema.

Hivyo, amewataka wanachama wenzake kuacha makundi ya kura za maoni na sasa mwelekeo uwe kwenye uchaguzi mkuu.

Kuhusu wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani ambao kwenye majimbo na kata zao watapigiwa kura za “Ndiyo” na “Hapana,” makamu mwenyekiti  huyo ametoa tahadhari dhidi ya kubweteka, badala yake kuwahamasisha wananchi na wanachama wa CCM kujiokeza kupiga kura, Oktoba 29, 2025.

“Hata kama hukupingwa bado wewe ni mgombea wa CCM. Sasa ukisema umeachwa kuwa mbunge ukae kimya, hii si nzuri. Wote tuwahamasishe watu wajitokeze kupiga kura siku ikifika ili tupate ushindi mkubwa.

“Lazima tuhimize hili maana sheria mpya ya uchaguzi inasema hata kama hukupata mgombea wa upinzani, wananchi lazima waende kwenye vituo vya kupigia kura wapige kura za “ndiyo” au “hapana,” ili zihesabiwe na utangazwe mshindi. Tofauti na zamani.”

“Tunapojiandaa kukamata dola lazima tuhakikishe watu wanapiga kura. Tunaposema kufanya kampeni, haimaanishi Wazira au Mwenyekiti ndiye anaenda kuifanya, bali wanachama wa CCM wana wajibu wa kufanya kampeni ili hata wasiotutaka waende wapige kura,” amesema kiongozi huyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema amekuja mkoani Arusha kushirikiana na wananchi na atahakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru na haki.

Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Musa Matoroka, amesema katika mkoa huo wenye majimbo saba, Jimbo la Ngorongoro lina mgombea pekee anayetokana na CCM, huku majimbo mengine sita yakiwa na wagombea zaidi ya chama kimoja.

Amesema Jimbo la Arusha Mjini lina wagombea 16 wa ubunge, Arumeru Magharibi 12, Arumeru Mashariki 8, Longido wawili, huku katika kata zote 160 za mkoa wa Arusha, chama hicho kikisimamisha wagombea wake.