Dodoma. Viongozi wastaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali wamemwelezea mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kama chaguo bora katika nafasi hiyo, huku wakiwataka wananchi kwenda kumpigia kura, ili aendelee kuliongoza taifa.
CCM kinaendelea na kampeni katika maeneo mbalimbali, na tangu kilipozindua kampeni zake Agosti 28, tayari mgombea huyo urais amefanya kampeni katika mikoa ya Morogoro na Dodoma, huku akitarajiwa kuendelea na kampeni mkoani Songwe.
Wakati huohuo, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi, amefanya mikutano ya kampeni katika mikoa ya Mwanza na Mara, lengo likiwa kuinadi ilani ya CCM na kuwashawishi wananchi kukipigia kura chama hicho.
Leo, Samia amefanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Chamwino, Chemba, Kondoa na kumalizia Dodoma Mjini, ambako maelfu ya wananchi wamejitokeza kumsikiliza.
Katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Tambukareli jijini Dodoma, viongozi wastaafu walipopewa nafasi ya kuzungumza, wamemuimbea kura mgombea huyo wa urais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Philip Mangula, amewataka wananchi wa Dodoma kwenda kumpigia kura Samia, kwa sababu tayari ana uzoefu wa kutosha katika miaka minne iliyopita na kazi aliyofanya imeonekana.

“…mgombea wetu analipenda Taifa hili, ameonyesha uwezo wake. Hao wengine (wagombea wa vyama vya upinzani) mmh, hatuwezi kufanya majaribio. Mkampigie kura Samia, anayafanikisha yote yaliyowekwa kwenye ilani,” amesema Mangula.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, amesema katika historia ya chaguzi za Tanzania, mikoa miwili imekuwa na rekodi nzuri ya kutoa kura nyingi kwa CCM ambayo ni Iringa na Dodoma.
Amewahamasisha wananchi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kwenda kumpigia kura mgombea huyo wa CCM ili aendelee kuliongoza Taifa kwa miaka mitano ijayo.
“Ninawaomba wana Dodoma wenzangu, wote tukampe kura zetu Samia ili aendelee kutuongoza. Tukawapigie kura wabunge na madiwani wa CCM,” amesema Malecela.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Dk Bashiru Ally, amesema amepokea kazi waliyopewa na mwenyekiti ya kuweka wagombea bora, kuielezea ilani kwa wananchi na kukitafutia kura chama hicho kwenye uchaguzi ujao.
“Twendeni tukakitafutie kura chama chetu ili kiendelee kuiongoza Serikali kwa mustakabali wa Taifa hili,” amesema Dk Bashiru kwenye mkutano huo ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Samia, amesema chama chake kimejipanga kumaliza changamoto ya maji katika mkoa huo ili uendane na hadhi yake ya kuwa makao makuu ya nchi.
“Dodoma ni makao makuu ya nchi, si vema kuwa na tatizo la maji. Tutamaliza tatizo hilo kupitia mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria. Pia, ujenzi wa bwawa la Fakwa ukikamilika, utapunguza tatizo la maji katika mkoa huu,” amesema mgombea huyo.
Kwa upande wa nishati ya umeme, amesema wanakwenda kujenga kituo cha kupoza umeme wenye msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma. Amesema wanaamini mkoa huo utakuwa na umeme wa uhakika.
“Tunakwenda kumalizia ujenzi wa Uwanja wa Msalato. Ni matumaini yetu kwamba ifikapo mwaka 2027, wale wanaokuja kwenye mashindano ya Afcon waje kufanya mazoezi kwenye uwanja huo,” amesema Samia.
Ameongeza kuwa wanakwenda kuongeza kasi ya usajili wa ardhi ili kumaliza migogoro ambayo imekuwa ikijitokeza. Pia, amesema wanakwenda kuvutia uwekezaji kwenye kongani za viwanda mkoani humo.