Dar es Salaam. Wazazi na walezi wamehimizwa kuzingatia umuhimu wa chanjo ya polio kwa watoto, ili kuwaepusha na madhara mbalimbali yakiwamo ulemavu wa kudumu.
Wito huo umetolewa wakati wa kampeni ya uhamasishaji inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Mwananyamala na Rotary Club mbalimbali, ikilenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za ugonjwa huo na umuhimu wa chanjo kama kinga madhubuti. Kampeni hiyo ni i sehemu ya maandalizi kuelekea Siku ya Polio Duniani inayoadhimishwa Oktoba 24 kila mwaka.
Elimu hiyo inawalenga watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ambao ndiyo waathirika wakuu wa maradhi hayo, yanayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu kwa watoto.
Akizungumza na kinamama hospitalini hapo Agosti 30, 2025, wakati wa utoaji wa elimu, mtaalamu wa masuala ya afya, Eunice Toonde, amesema wazazi wengi bado wanashindwa kutambua athari za ugonjwa wa polio, hivyo wapo wanaoshindwa kumaliza ratiba za chanjo kwa watoto wao.
“Ingawaje hatuna visa vingi vya ugonjwa wa polio hivi karibuni, sababu ya kutoa elimu ya umuhimu wa kumaliza chanjo ni kutaka kustawisha hali tuliyo nayo, kwani kutomaliza chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka mitano kunaweza kusababisha madhara mengi, yakiwemo ulemavu wa kudumu, kuharibika mfumo wa neva, kupoteza uwezo wa kutembea au kuwa na matatizo makubwa ya kudumu katika viungo vya mwili,” amesema Eunice.
“Polio inaweza pia kuathiri misuli ya kupumua, hali inayoweza kusababisha kifo kama mtoto hapati matibabu ya haraka,” ameongeza.
Eunice amesisitiza kuwa polio haina tiba, bali kinga pekee ndiyo inayoweza kuzuia maambukizi, hivyo ni muhimu kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo ya ugonjwa huo kwa watoto.
Kwa upande wake, Catherine Moshi, mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo cha KIUT anayesomea udaktari, amesema wazazi wengi hawajui kinga za aina gani watoto wao wanapewa, na hivyo wanapowaona watoto hawana dalili yoyote, hawaoni umuhimu wa kumaliza chanjo ya polio, jambo linaloweza kuwa hatari kwa afya ya mtoto.
“Kinamama wanatakiwa kuhakikisha wanawapatia watoto wao na kumaliza chanjo ya polio. Mtoto hupokea chanjo ya polio wiki ya kwanza tangu kuzaliwa, na baada ya wiki sita, kumi na nne na kumi na sita, ili kumuepusha na polio,” amesema Catherine.
Naye Rais wa Rotary Club Mikocheni, Nasibu Mahinya, amesema lengo la kutoa elimu hiyo katika Hospitali ya Mwananyamala ni kutokana na ufanisi mdogo wa kumfikia kila mjamzito na mlezi, hususan baada ya kugundua wengi hawafahamu madhara ya polio.
“Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza ugonjwa wa polio, bado wapo kinamama wengi wasiojua madhara ya polio, hivyo tukaona ni muhimu kutoa elimu hii hadi kilele cha Siku ya Polio Duniani,” amesema Mahinya.
Mahinya ameongeza kuwa kampeni za uhamasishaji zitakazofanyika kwa miezi michache ijayo, ili kuelimisha kinamama na walezi juu ya umuhimu wa kumaliza chanjo ya polio kwa watoto.
Muuguzi Mkufunzi kutoka Wizara ya Afya, Gloria Mwankenja, ametoa mfano wa mataifa kama Afghanistan na Pakistan, ambayo bado yanakumbwa na changamoto kubwa ya ugonjwa wa polio, na kusema kuwa muingiliano wa watu ni mojawapo ya sababu zinazofanya elimu hiyo kuwa muhimu zaidi.
“Kwa sasa, Tanzania imedhibiti ugonjwa wa polio, na mtoto wa mwisho kugundulika na ugonjwa huo alikuwa Mei 26, 2023 katika Manispaa ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa,” amesema Gloria.
Elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa wananchi hadi Oktoba 24, ambapo Siku ya Polio Duniani itakuwa ikiadhimishwa duniani kote, ikiwa na lengo la kutokomeza ugonjwa wa polio kabisa.