Dar es Salaam. Tabia yake ya kujibu jumbe za wananchi kwenye mitandao ya kijamii inamfanya kuwa miongoni mwa viongozi wachache wanaoonekana na kukubalika zaidi mitandaoni.
Sifa hii anaipata si tu kwa kujibu hoja na kutoa ufafanuzi wa mambo kadha wa kadha yanayohusu sekta yake kama wengine, bali yeye anakwenda mbele zaidi kwa kujibu jumbe za mwananchi mmoja mmoja kulingana na alichokiandika.
Kwa kifupi, utakavyokuja kwenye ukurasa wake ndivyo atakavyokupokea, ukija na hoja, ataijibu; ukiwa na changamoto, atakushauri na kukuonesha wapi unaweza kupata msaada; ukileta mzaha, naye atajibu mzaha. Kwa kifupi, unaweza kumuita mama wa mitandaoni.
Huyu ni Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, ambaye amedumu kwenye nafasi hiyo kwa takribani miaka mitatu tangu kuteuliwa kwake.
Safari yake ya kisiasa ilianza Desemba 5, 2020, alipoteuliwa na Rais John Magufuli (hayati) kuwa mbunge, kisha kumteua kuwa Waziri wa Afya. Kabla ya nafasi hiyo, Dk Gwajima alikuwa akihudumu kama Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tamisemi (Afya).
Alidumu kwenye wizara hiyo kwa takribani miaka miwili kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kumuhamishia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, anayohudumu hadi sasa.
Hata hivyo, siku za karibuni umeibuka mjadala wa uwezekano wa mama huyu kutoendelea kuwepo kwenye wizara hiyo kutokana na kutokuwa miongoni mwa wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za ubunge.
Jina la Dk Gwajima halikuonekana kwenye orodha ya watiania wa majimbo wala viti maalumu, hali inayosababisha wananchi wengi mitandaoni kudhani huenda asiwepo kwenye wizara hiyo ambayo anaonekana kuitendea haki.
Suala hilo limeonekana kuumiza vichwa vya wananchi, hasa wanaochangamana na mama huyu kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii, ambako amekugeuza kama moja ya ofisi yake.
“Hivi kwa nini hukugombea ubunge mama? Natamani urudi bungeni, lakini je, usipopata uteuzi katika vile viti 10, itakuwaje? Ukweli ni kwamba tutakuwa tumepoteza waziri jembe, nani atatutetea wanaume?” ameandika Star-Lamaa wakati akitoa maoni kwenye ukurasa wa Dk Gwajima.
Maoni yanayofanana na hayo yametolewa pia na Maria Florah: “Mpendwa Rais Samia, tunaomba huyu mama mtuachie, amekuwa zaidi ya faraja kwa jamii ya Watanzania.”
“Ukitaka kuwa kiongozi bora, jichanganye na watu, mfurahi ujue maoni yao. Kiukweli, waziri Gwajima anajua mengi na uongozi. Mimi nimemfuatilia kwa muda mchache, nimeona mengi. Kwa kifupi, mama, huna haja ya walinzi, Watanzania tuko tayari kukulinda,” ameandika Jumanne Kimolo.
Naye Jovitha Mlay ameandika: “Mmoja wa viongozi wanawake ninaowapenda sana katika siasa. Asante kwa kuwa chachu ya hamasa kwa wasichana na wanawake wengi hapa Tanzania. Huduma unazotupatia nina kila sababu ya kusema wewe ni kiongozi wa pekee na mfano wa kuigwa.”
“Ninavyokupenda wewe, mama, natamani usingekuwa na chama chochote, uendelee kututumikia Watanzania,” ameandika Dodolima.
Kwa upande wale, Mandiko Mathew ameandika: “Waziri wetu uko vizuri kwa kweli. Mawaziri wote wangekuwa kama wewe, kusingekuwa na lugha za ajabu zinazoelekezwa kwa kiongozi wetu wa juu. Naomba ubaki kwenye wizara hii.”
Mbali na tabia ya kujibu jumbe za wananchi, Dk Gwajima amekuwa akionesha kwa mfano namna ya kuwa mke na mama wa familia. Licha ya nafasi yake ya uongozi, mara kadhaa amekuwa akionesha maisha yake na mumewe, na wote kwa pamoja wamekuwa kielelezo cha kuhamasisha upendo kwa wanandoa.
Hili pia limekuwa kivutio kwa wengi, hasa wanaume, ambao mara kadhaa wamekuwa wakimpongeza kwa namna anavyosimama katika nafasi yake kama mwanamke kwenye nyumba, licha ya kuwa na madaraka ya kitaifa.
“Mama, unalolifanya unafundisha vijana wajue mapenzi na ndoa. Mungu akutangulie urudi tena kwenye wizara hii maana maisha unayoishi ni ya kijamii,” ameandika Lesamilaf.
Naye Salehe Sultan amedika: “Kama wanawake wote wangekuwa na upendo na mfumo wa maisha kama wa waziri Gwajima kwa mume wake, basi ndoa nyingi zingekuwa na furaha na amani pia.”
“Huyu mama namkubali sana, kwa wale wenye kiburi kwa sababu wana pesa na wanashindwa kuwaheshimu waume zao, wana kitu cha kujifunza kwa waziri Gwajima. Mbele ya mume wake anaweka uheshimiwa mbali, ni mnyenyekevu na mwenye heshima,” ameandika Bynassakaka.
Kwa upande wake, George Giz ameandika: “Nyie wenzetu mnatumia dawa gani, pamoja na cheo ulichonacho bado unaonesha heshima kwa mumeo. Wengine huku tumeoa mtendaji wa kijiji, tumdomo anarefusha, hataki amani. Ndoa inakuwa chungu, ndani haieleweki mwanaume nani, mwanamke nani. Lakini huyu waziri anamheshimu mume wake bila kujali cheo chake.”
Akizungumzia hilo, mwanasaikolojia Jacob Kilimba amesema kinachotokea kwa waziri huyo ni matokeo ya tabia yake ya asili ya kupenda kujichanganya na watu.
“Kisaikolojia, kuna aina ya watu wanapenda kujichanganya na wengine wanakuwa wa kujitenga. Sasa huyu mama, kwa uhalisia wake, anaonekana ni mtu wa kujichanganya. Ukimsikia anavyoongea, utajua huyu ni mtu mwenye haiba ya kujichanganya na watu.
“Kuna wakati anakuwa kama mama, na hii inamsaidia kwenye wizara yake hata watu kuwa huru kuwasilisha changamoto walizonazo, hasa matukio ya ukatili, ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakifichwa lakini sasa yanaripotiwa na wanaona hatua zinachukuliwa,” amesema.
Kilimba amebainisha kuwa kwa kawaida watu wanapenda kuwa karibu na viongozi wao, ikitokea na yeye anawapa nafasi hiyo, ndiyo sababu amekuwa kivutio cha watu.
“Viongozi wengine wangechukua mfano huo ili kujua hali ilivyo kwa jamii. Kwa wizara ile, akikosekana Gwajima, naamini Serikali itapoteza uhusiano wake na jamii na kupata taarifa zinazohusu matatizo ya watu.”
Mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto, Rhoda Mmari, amesema anachokifanya waziri huyo kinachochea ushiriki wa wananchi katika masuala mbalimbali yanayohusu jamii, ikiwemo kuibua changamoto, hasa zinazohusu matukio ya ukatili.
Amesema waziri huyo amekuwa pia akitumia mitandao kuhamasisha jamii, hususan wanawake na vijana, kuhusu haki zao, fursa za kiuchumi na masuala ya kijamii.
“Kupitia mitandao ya kijamii, wananchi wanaweza kutoa maoni yao, malalamiko au mapendekezo moja kwa moja, na anapoyafanyia kazi inawapa hisia kwamba mawazo yao yanathaminiwa na kwamba wana nafasi ya kushiriki katika utawala.
“Mitandao ya kijamii humsaidia yeye kama waziri kutambua matatizo haraka katika jamii. Malalamiko yanayoibuliwa na wananchi hupata majibu ya haraka au kufikishwa kwa mamlaka husika kwa ufuatiliaji, hivyo kuboresha utoaji wa huduma.”
Akizungumzia hilo, Wakili Bashir Yakub amesema kiongozi yeyote wa umma anapaswa kuwa karibu na watu, jambo ambalo Dk Gwajima analifanya kwa ufanisi wa hali ya juu.
“Namna ya kuufikia umma kwa wepesi katika mazingira ya sasa ni mitandao ya kijamii. Moja ya malengo ya mitandao ni kuwaleta watu karibu.
“Tabia yake inamuweka karibu na watu anaowaongoza, hii inamfanya kujua changamoto zao, na wao wanajisikia salama kueleza yanayowasibu,” amesema na kuongeza:
“Sio kwamba viongozi wengine hawatumii mitandao, ukweli ni kwamba hawataki kujihusisha na watu, na hawatumii mitandao kutatua kero za wananchi kama anavyofanya Dk Gwajima. Kiongozi wa umma ni lazima uwe mnyenyekevu kwa umma.”
Amesema kupitia tabia hiyo ya waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya jamii, mitandaoni mambo mengi yanaibuliwa na amekuwa akiyafuatilia, na hatua zinachukuliwa.
“Kupitia yeye, matukio mengi ya ukatili mitaani yameibuliwa na anaonesha kufanyia kazi taarifa anazopata hadi hatua zinachukuliwa, hii inafanya watu wengi kujenga imani dhidi yake, na ndicho kinachotakiwa kwa kiongozi wa umma,” amesema.
Mfano wa matukio ni yale ambayo Dk Gwajima ameonesha kuchukua hatua pindi yalipoibuliwa mitandaoni, ni lile linalomhusu binti wa Yombo, ambaye alifanyiwa ukatili na kundi la vijana wanaodaiwa kutumwa na afande.
Baada ya taarifa hiyo kufikishwa kwa jeshi la polisi, vijana hao walitafutwa, kupatikana, wakafunguliwa mashtaka na kufikishwa mahakamani.
Tukio lingine lililoibuliwa mitandaoni na kuchukuliwa hatua na mama huyo ni lile linalowahusu mabinti wa chuo waliomfanyia ukatili na udhalilishaji mwenzao kwa kile kilichodaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume wa mwenzake.
Kama ilivyo ada yake, waziri alipopata habari kuhusu tukio hilo, alitoa taarifa rasmi ya wizara kukemea kitendo hicho na kuliagiza jeshi la polisi kuchukua hatua stahiki. Mabinti hao walipatikana na wakafikishwa mahakamani.
Amefanya hivyo pia hivi karibuni baada ya kupata malalamiko ya Neema Nairot, ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram alilalamikia kufanyiwa ukatili na mchumba wake kwa ushirikiano na familia yake.