Unguja. Harakati za kusaka Ikulu ya Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitano ijayo zimeendelea kushika kasi, baada ya watiania kutoka vyama mbalimbali kujitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwania nafasi ya urais kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Leo , Agosti 31, 2025, wagombea kutoka vyama vya NCCR-Mageuzi, ACT-Wazalendo, Chama cha Kijamii (CCK), SAU, Ada Tadea na UMD waliwasili katika ofisi za tume kuchukua fomu, kila mgombea akiambatana na viongozi wa vyama vyao na wapambe, huku kila mmoja akitoa kauli za matumaini iwapo atapewa ridhaa na wananchi ya kuongoza nchi.
Kabla ya kukabidhi fomu kwa wahusika, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amewakumbusha wagombea, kuzingatia masharti ya kujaza na kurejesha fomu kwa wakati pamoja na kuambatanisha picha tatu za pasipoti na stakabadhi ya malipo ya Sh1 milioni kama dhamana, kwa mujibu wa kanuni za mwaka 2015.
“Kiasi hiki cha fedha kitarudishwa iwapo mgombea atashinda au angalau kupata asilimia 10 ya kura,” amesema Jaji Kazi huku akisisitiza tume iko tayari kutoa msaada wa kitaalamu kwa wagombea ili kuepusha makosa ya kiufundi.
Aliyekuwa wa kwanza kufika katika ofisi za ZEC leo saa 2:40 asubuhi, alikuwa Laila Rajab Khamis wa NCCR-Mageuzi.
Baada ya kukabidhiwa fomu, amesema iwapo atateuliwa na kuungwa mkono na wananchi, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kuboresha huduma za afya na kuimarisha uchumi wa vijana kupitia ajira stahiki.
“Huduma za afya bora na ajira za vijana vitakuwa msingi wa uchumi wa Zanzibar,” amesema.
Saa 3:55 asubuhi, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud, amewasili akiwa na mkewe na viongozi waandamizi wa chama.
Baada ya kupokea fomu, amesema chama chake kimejiandaa kutoa mwelekeo mpya kwa wananchi.
“Ni wakati wa mabadiliko. Wananchi wamekuwa wakinitayarisha muda mrefu, sasa ni fursa ya kutumikia Taifa,” amesema.
Othman pia amesema msimamo wa chama chake ni kupinga kura ya mapema akidai haina tija, ingawa wataendelea kushiriki kisheria.
“Tufanye kila kitu kwa amani na umoja. Ni wakati wa kuwaamsha Wazanzibari waliolala ili kupata mabadiliko,” amesema.
Mgombea wa CCK, Aisha Salum Hamad, amewasili saa 5:48 asubuhi akiongozana na viongozi wa chama chake.
Aisha amesema wanawake wana uwezo wa kuongoza na chama chake kimejiandaa kushindana kwa nguvu zote.
“Wanawake tunaweza na tutashindana kwa asilimia mia moja,” amesema, akisisitiza kuwa atawasilisha sera na mwelekeo wa chama wakati wa kampeni.
Ali Mwalim Abdalla wa SAU aliyefika katika ofisi hizo saa 6:00 mchana baada ya kukabidhiwa fomu, amesema ni haki yake ya Kikatiba kugombea, lakini vipaumbele vyake atavieleza baada ya kupitishwa na tume.
“Nimejipanga, wananchi wakae tayari kwa mambo mazuri,” amesema.
Kwa upande wa Ada Tadea, mgombea Juma Ali Khatib amesema ameingia kwenye kinyang’anyiro kwa lengo la kuwania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, lakini akishinda urais, itakuwa fahari kwake.
Amesema anataka kuendeleza kazi iliyoachwa na Dk Hussein Mwinyi, huku akisisitiza umuhimu wa elimu inayotilia mkazo matumizi ya teknolojia kuanzia shule za awali ili vijana wawe na uwezo wa kiushindani katika ajira.
Ilipofika saa 9:00 alasiri, Mohamed Omar Shaame wa UMD aliwasili kuchukua fomu huku akiahidi kwamba, iwapo atapewa ridhaa, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni kuboresha huduma za kijamii.
“Nitatangaza uniti 100 za umeme zitolewe bure kwa kila kaya, pia watu wenye ulemavu watalipwa mishahara na huduma za mawasiliano ya simu zitakuwa bure ndani ya Zanzibar,” amesema.
Shaame amesema hatua hizo zitapunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, sambamba na kupunguza gharama za maisha.