‘X-Factor’ ya Fadlu ni hii!

KATI ya vitu ambavyo kocha wa Simba, Fadlu Davids vinampasua kichwa ikiwa ni siku chache tu kabla ya kuanza msimu mpya wa 2025/26 ni pamoja na mchezaji mwenye sifa ya kuamua mchezo, ambapo katika mahojiano yake kabla ya kurejea Dar alitumia neno la Kiingereza ‘X-Factor’.

Mwanaspoti linajua kwamba mchezaji anayemtaka Fadlu ni mtu anatakayecheza pale kwenye eneo la kiungo mshambuliaji akiwa na uwezo wa kuvunja ngome ya wapinzani na kuamua matokeo hasa kwenye mechi kubwa na ngumu na hilo ndilo lililoiangusha Simba msimu uliopita ikiwemo katika mechi mbili dhidi ya Yanga.

Msimu uliopita dhidi ya watani zake hao Simba ilianza kwa kupoteza kwa bao 1-0 kwenye Ngao ya Jamii na kwenye ligi ikalala kwa jumla mabao 3-0, kwani katika mechi ya kwanza ilipoteza kwa bao 1-0 na kisha 2-0 ile ya mzunguko wa pili.

Katika kuhakikisha anafanikiwa kupata staa atakayekuwa na uwezo wa kuamua mchezo, kocha huyo kwa sasa anapambana na wale waliopo, kwani licha ya dirisha la usajili nchini kuwa wazi, lakini uwezekano wa kupata nyota mwenye sifa hizo kutoka katika timu za Ligi Kuu Bara ni mdogo.

Lakini, anapambana kupata suluhu kutoka miongoni mwa wachezaji alionao na tayari ana uhakika na huduma ya Neo Maema aliyesajiliwa kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kwa sasa kocha huyo anaangalia namna gani Maema anaweza kutumika kwenye kikosi hicho kwa kushirikiana na Charles Jean Ahoua ambaye msimu uliopita ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akimaliza na mabao 16 huku akiwa na asisti tisa.

“Tumekuwa na wakati mzuri wa maandalizi, lakini bado kazi haijamalizika. Tuna siku chache hapa na tuna mambo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi… hatupo mbali na kule ambako tunahitaji kuwa,” alisema na kuongeza:

“Wote (Maema na Ahoua) ni wachezaji wazuri. Tunachohitaji ni ufanisi zaidi kwenye maeneo yote, hivyo tutaangalia kama kuna uwezekano wa kucheza wote kwa pamoja. Tutaona itakavyokuwa na kadri ambavyo wataendelea kuzoeana. Nina imani na ubora wao, ila tunachohitaji ni vile ushirikiano wao unaweza kuwa na matunda.”

Ndani ya wiki chache zilizosalia kwa Simba kabla ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Fadlu anapambana kuona kama anaweza kuwatumia nyota hao kwa wakati mmoja ili kuwa na ufanisi zaidi kwenye eneo la kiungo cha ushambuliaji.

Lakini, hilo alisema litategemea na uwiano wa timu kwani msimu uliopita Simba ilitumia viungo wakabaji wawili ambao ni Fabrice Ngoma aliyeondoka na sasa yupo Alassane Kante aliyesajiliwa kutoka CA Bizertin ya Tunisia, Yusuph Kagoma huku juu yao akicheza Ahoua kama namba 10.

Fadlu anaamini ubora wa viungo hao washambuliaji utakuwa na nafasi kubwa ya kuongeza makali zaidi katika safu ya ushambuliaji ambayo ina washambuliaji wapya wawili – Jonathan Sowah aliyefunga mabao 13 msimu uliopita akiwa na Singida Black Stars pamoja Seleman Mwalimu aliyetua akitokea Wydad Casablanca ya Morocco. Nyota hao wanaungana na Steven Mukwala ambaye msimu uliopita aliifungia Simba mabao 13 kwenye ligi.

Septemba 10, Simba itacheza mechi ya mwisho ya kirafiki kwenye tamasha la Simba Day dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kabla ya mechi ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii – siku sita baadaye na baada ya hapo itasafiri kwenda Botswana kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya awali dhidi ya Gaborone United.