Ahadi hewa mwendokasi Mbagala zakera wakazi Dar

Dar es Salaam. Baada ya huduma ya mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) katika barabara ya Mbagala kukwama kuanza leo kama ilivyoahidiwa awali na Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), wachumi na wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa malalamiko pamoja na ushauri wa nini kifanyike ili huduma hiyo ianze kutekelezwa.

Akieleza sababu ya kushindwa kutimiza ahadi hiyo, alipozungumza na Mwananchi leo, Septemba mosi, 2025, Mtendaji Mkuu wa Dart, Dk Athuman Kihamia, amesema imetokana na kutokamilika kwa miundombinu muhimu yakiwamo mageti janja na kituo cha kujazia gesi.

“Mabasi yamewasili, lakini hatutaweza kuanza kutoa huduma leo kama tulivyoahidi kwa kuwa baadhi ya miundombinu haijakamilika.

“Mageti janja kwa ajili ya ukataji wa tiketi bado hayajafungwa, na kituo cha kujazia gesi kilichopo kwenye karakana ya Mbagala nacho hakijakamilika. Hata hivyo, taarifa rasmi kuhusu maendeleo ya ujenzi huo tutaitoa baada ya wiki moja,” amesema Dk Kihamia, wakati ambao abiria wa Mbagala walikuwa wamejiandaa kuanza kupata ladha mpya ya usafiri wa umma.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mofat, Muhammad Abdallah Kassim, alipozungumza na Mwananchi wakati wakipokea mabasi hayo mwishoni mwa wiki, alisema hawatapokea fedha taslimu kwa malipo ya nauli na badala yake abiria wanapaswa kutumia kadi za Dart au za benki ambazo tayari zitafanya kazi na mfumo huo.

“Sisi hatupokei fedha taslimu. Abiria ataweka fedha kwenye kadi na kisha atatumia kusafiri. Mageti tayari yamewasili na kazi ya kuyafunga katika vituo mbalimbali inaendelea,” alisema Kassim.

Mabasi hayo 151 yaliwasili katika karakana ya Mbagala Rangi Tatu usiku wa Agosti 29, 2025, baada ya kutoka bandarani, shughuli iliyochukua takribani siku mbili.

Kampuni ya wazawa ya Mofat ndiyo iliyopewa jukumu la kuleta magari katika awamu ya kwanza ya mradi huo, ambao ni wa pili kutekelezwa ukitanguliwa na ule wa Kimara, imekabidhiwa kuleta mabasi 255 kati ya 755 yanayohitajika kwa mradi mzima.

Ahadi zilizowahi kutolewa

Wiki iliyopita, Dk Kihamia aliliambia gazeti The Citizen kwamba huduma ingeanza rasmi Septemba mosi, 2025, na kubainisha kuwa utumiaji wa tiketi ungetumika kwa mpito wakati wakisubiria mageti janja yafungwe.

Pia, Agosti 13, 2025, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokagua miundombinu hiyo aliagiza sehemu zilizobaki zikamilishwe ili huduma ianze ndani ya mwezi huo.

Hata hivyo, wakati Majaliwa akiagiza hayo, moja ya changamoto iliyokuwa imebakia ni ujenzi wa kipande cha barabara katika eneo la Kamata, ambacho bado hakijakamilika.

Mbali na changamoto za barabara, vituo vya mwendokasi navyo havikuwa na mageti ya kisasa kwa ajili ya mfumo wa kulipia kwa kadi.

Ukiacha ahadi ya Dk Kihamia na agizo la Waziri Mkuu, pia Julai 7, 2025 katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Kampuni ya Mofat, Mabrouk Masasi, alieleza kuwa mara tu magari hayo yatakapowasili nchini wangeanza kutoa huduma, hata kama yangekuwa machache kuliko idadi inayohitajika.

Walichosema wachumi, wananchi

Wakitoa maoni yao kuhusu danadana hizo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi akiwemo Profesa Humphrey Moshi, wamesema miradi inapocheleweshwa huongeza gharama.

Profesa Moshi amesema zipo sababu za kufika huko kwa kueleza kuwa kunakuwepo na mipangilio mibaya ya rasilimali fedha iliyotengwa kutekeleza mradi husika.

“Inapaswa mkishatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza jambo fulani basi lifanyike hadi likamilike, lakini kwa bahati mbaya sana fedha zinazotengwa katika miradi mikubwa kwenye nchi hii huwa watendaji wakizigawa na kuzifanyia mambo mengine, na hapo ndipo mradi unakwamia katikati.

“Hivyo, mwisho wa siku katika utekelezaji wake, badala ya kuona matokeo yake baada ya mwaka mmoja itakuchukua miaka minne hadi mitano kuyaona,” amesema Profesa huyo.

Ametolea mfano, kama unataka kuboresha elimu, unapaswa kuwa na walimu wa kutosha, vifaa na majengo, lakini si kusema mwaka huu utafanya hivi, mwakani utafanya hivi, na mwaka keshokutwa utafanya vile.

Hata hivyo, katika ushauri wake, mchambuzi huyo amesema ipo haja ya Watanzania kubadilika, ikiwemo kukamilisha miradi kabla ya wakati, jambo alilosema Taifa la China ndilo limekuwa likifanya hivi, jambo linalowasaidia kupunguza gharama.

“Kwa kuwa ni watu ambao wamekuwa wakipewa kujenga miradi mingi hapa nchini, ni vema wakaigwa,” amesema.

Mchambuzi Dk Abel Kinyondo amesema mradi kama wa Udart umepangwa ili kutatua tatizo, hivyo unapocheleweshwa ufanisi uliopangwa kuletwa unakuwa hauonekani.

“Tatizo hilo linakupa mashaka kuwa hata baadaye mradi ukija kuzinduliwa matatizo ya kiuongozi hayataisha kwa sababu mradi kama wa BRT siyo mpya kwa kuwa umekuwepo kwa muda sasa, lakini ni moja ya miradi inayoendeshwa kwa hovyo.

“Mradi wa BRT mimi nasema ni mradi pekee ambao wateja wake wako wengi, lakini biashara haina faida, biashara inakufa. Kwa hiyo, hii ni dalili ya kuwepo kwa ombwe la kiuongozi na utawala bora,” amesema Dk Kinyondo na kuongeza;

“Inabidi tujipange kwa maana ya uongozi na kiutawala bora. Isiwe tu mradi umezinduliwa, lakini yale yanayotakiwa kutokea kutokana na mradi kuwepo kwa maana ya faida zake ziwepo. Tuuache kuona sasa watu wanaacha kupanda kwenye mabasi kupitia dirishani, watu wanajazana kwenye vituo bila kuwepo magari, magari yanayopaki ni mengi kuliko yaliyoko barabarani,” ameeleza.

Amebainisha kuwa mradi wa DART ulitakiwa uwe na ufanisi kiasi kwamba mwenye gari yake aone ufahari kuliegesha gari lake na kupanda mwendokasi kuliko kuendesha kwenda ofisini au kokote kule.

“Lakini kunapokuwa na mradi kama huo halafu mtu anaona ni bora apande daladala, inavunja moyo na ukizingatia miradi iliyotekelezwa kupitia mabasi hayo imetumia fedha nyingi, na ni fedha za mlipakodi,” amesema.

Hata hivyo, ucheleweshaji huo umewavunja moyo baadhi ya wakazi wa Mbagala, akiwamo Deogratius Kisinde, aliyesema, “Tumemsikia mara kadhaa Mkurugenzi wa Dart akiahidi huduma ingeanza leo, lakini hakuna kinachoendelea. Mabasi tumeona yakiingizwa kwenye karakana tangu juzi. Ni vema mamlaka ziwe zinatoa ahadi za kitaalamu na si za kisiasa.”

Naye Alphonce John amesema anachokiona katika utoaji ahadi hewa katika miradi kama hiyo ni viongozi kuhofia vibarua vyao.

John amesema kutokana na hilo, wamekuwa wakiahidi vitu ilhali wanajua bado hawajavikamilisha, ilimradi tu kuwaridhisha wakubwa zao na kulinda vibarua vyao, jambo ambalo halileti picha nzuri wala haliwasaidii wananchi.

Mabasi hayo, yenye urefu wa mita 18, yatakayobeba abiria 160 kila moja, yanatarajiwa kusafirisha kati ya abiria 325,000 hadi 400,000 kwa siku mara huduma itakapoanza. Safari zitakuwa zikifanyika kutoka Mbagala hadi Gerezani, Kivukoni na Morocco, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.