Ajibu ajifunga mwaka mmoja KMC

KIKOSI cha KMC kinachonolewa kwa sasa na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Yanga, Marcio Maximo, kimezidi kuimarishwa katika eneo la ushambuliaji baada ya kumsajili kwa mkataba wa mwaka mmoja, Ibrahim Ajibu aliyekuwa akiitumikia Dododma Jiji.

Kiungo mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, Yanga, Azam na Singida Big Stars kwa msimu uliopita akiwa na Dodoma Jiji alifunga bao moja tu, lakini mabosi wa KMC hawakuona tatizo kumpa mkataba wa mwaka mmoja ili aungane na wenzake wanaoendelea kujifua chini ya Mbrazili Maximo.

Katika nafasi anayocheza Ajibu atakwenda kukutana na ushindani wa wachezaji wakiwamo Redemtus Mussa, Oscar Paulo na Baraka Majogoro ambaye msimu uliopita hakuwa na timu baada ya kutoka Chippa United ya Afrika Kusini 2023/24.

Ajibu aliyewahi kuitumikia pia Coastal Union aliyoifungia mabao mawili msimu wa 2023-24 atakuwa na kibarua kizito na kufanya kazi ya ziada kuwaweka benchini Oscar aliyemaliza na mabao matano na Mussa aliyefunga manne msimu uliopita.

Chanzo cha ndani kutoka KMC kilisema: “Tumemsajili Ajibu kutokana na uzoefu alionao katika Ligi Kuu, japo data zake sio kubwa, ila ana uwezo wa kufanya vizuri.”

Chanzo hicho kiliongeza: “Mchezaji mwingine ambaye tumeona anaweza akaisaidia timu chini ya kocha mpya Mbrazil Marcio Máximo ni Majogoro. Uzoefu wake utakuwa msaada mkubwa katika timu.”

Msimu uliyopita KMC ilimaliza katika nafasi ya 10 kwa pointi 35, jambo ambalo chanzo hicho kilisema ligi ijayo ya 2025-26 klabu hiyo inalenga kupambana ili kumaliza katika nafasi za juu na siyo kujikwamua kuepuka kushuka daraja.