“Nani ameleta taarifa hizo?”
“Ni mwenyekiti wa mtaa huo.”
“Polisi wameshakwenda?”
“Wanajiandaa kuondoka.”
“Kwaminchi ni kubwa, hilo tukio limetokea sehemu gani?”
“Ametupa jina la mtaa na namba ya nyumba.”
“Ni mtaa gani?”
Polisi huyo alikuwa na kipande cha karatasi mkononi, akanisomea jina la mtaa huo na namba ya nyumba.
“Hebu nipe hicho kikaratasi.”
Polisi huyo akanipa kipande hicho cha karatasi. Baada ya kukisoma nilimwambia:
“Polisi wanaokwenda waende, nitafika muda si mrefu.”
Polisi huyo akatoka. Nilitaka kuendelea kuandika maelezo yangu, lakini tayari kihoro kilikuwa kimenishika, nikaacha kuandika, nikatoka ofisini.
Niliwakuta polisi wakijipakia kwenye gari na kuondoka, na mimi nikapanda gari ninalolitumia na kuelekea huko Kwaminchi. Dakika chache baadaye nikalisimamisha gari mbele ya nyumba moja iliyokuwa katika mtaa niliyoelekezwa.
Barazani mwa nyumba hiyo, ambayo nilihisi tukio hilo limetokea, kulikuwa na watu wengi walioonekana kuwa na shauku ya kujua kilichotokea. Gari la polisi lililonitangulia nalo lilikuwa limeshawasili.
Baada ya kusimamisha gari nilishuka. Watu waliokuwa hapo barazani walinipisha wenyewe, nikaingia ndani ya nyumba hiyo. Ukumbini nilikuta watu kadhaa. Nikakisia chumba kilichotokea tukio.
Kilikuwa chumba cha pili mkono wa kushoto. Kwenye mlango kulikuwa na watu waliosimama wakitazama ndani ya chumba hicho ambacho mlango wake ulikuwa umeachwa wazi. Nikachungulia ndani. Niliuona mwili uliokuwa ukining’inia kwenye kitanzi huku polisi wakiupiga picha.
Niliingia katika chumba hicho na kusaidiana na polisi hao kuuondoa mwili huo na kuulaza chini. Nikashituka nilipokiona kipande cha karatasi kwenye shingo ya mtu huyo. Nikakichukua na kukitazama.
Kilikuwa na maandishi ya wino mwekundu yaliyosomeka:
HUYU NI WA MWISHO
Chini yake kulikuwa na sahihi na alama ya dole. Sikuwa na shaka yoyote kwamba mtu huyo alikuwa amenyongwa katika mfululizo ule ule wa kina Unyeke. Nikashuku kwamba huyo alikuwa ni Chinga, ambaye nilifahamishwa na Husna.
Nikampekua mifukoni. Nikakuta simu, leseni ya kuendesha na pochi iliyokuwa na pesa. Niliitazama ile leseni, nikakuta ilikuwa na picha ya marehemu na jina lake liliandikwa Pascal Laizzer.
Ilituchukua kama nusu saa kukamilisha uchunguzi wetu katika chumba hicho, ikiwa ni pamoja na kuchukua alama za vidole za marehemu. Nikawaagiza polisi wautoe mwili huo na kuupakia kwenye gari.
“Hapa yuko mkazi wa humu ndani?” nikawauliza wananchi waliokuwa wakitutazama.
“Wakazi wapo,” mwanamke mmoja akaniambia.
“Na wewe ni nani?”
“Mimi ni mwenyekiti wa mtaa huu.”
“Wewe ndiye uliyetoa taarifa polisi?”
“Ndiyo mimi.”
“Sawa. Wakazi wa humu ndani wako wapi?”
“Hawa hapa.”
Mwenyekiti huyo alinionesha watu watatu waliokuwa mle chumbani.
“Marehemu anaitwa nani?” nikawauliza.
“Anaitwa Pascal,” alijibu mtu mmoja miongoni mwa wale watu watatu.
“Mnaweza kunieleza nini kimetokea?”
“Hatujui kilichotokea, ila tulimkuta ameshajinyonga.”
“Amejinyonga au amenyongwa?”
“Hatuna uhakika.”
“Nani alikuwa wa kwanza kumuona?”
“Ni mimi,” alijibu yule yule niliyekuwa ninazungumza naye.
“Ilikuwaje?”
“Huyu marehemu ni mpangaji mwenzetu ndani ya nyumba hii. Nilikuwa nimemgongea aniazime chaja yake. Chaja yake inakubaliana na simu yangu. Nilipomgongea hakujibu, nikajaribu mlango kuona kama alikuwepo. Mlango ukafunguka. Nikatupa macho, nikamuona ananing’inia kwenye kitanzi. Nikawafahamisha wenzangu tunaoishi humu ndani, halafu tukatoa taarifa kwa mwenyekiti…”
“Kuna aliyemuona marehemu hii leo kabla ya kujinyonga au kunyongwa?”
“Mimi binafsi nilionana naye asubuhi. Asubuhi alitoka, halafu alirudi akiwa amefuatana na jamaa mmoja ambaye simfahamu, wakaingia chumbani. Sasa baada ya hapo sikushughulika naye tena.”
“Alikuwa amefuatana na jamaa mmoja ambaye aliingia naye chumbani?”
“Ndiyo.”
“Humfahamu?”
“Simfahamu.”
“Je, ukimuona tena huyo jamaa au ukioneshwa picha yake unaweza kumfahamu?”
“Mmh! Naweza nimfahamu au nisimfahamu kwa sababu nimemuona mara moja tu, sikumkariri.”
“Marehemu ana ndugu mnaowafahamu?”
“Kusema kweli hatuwafahamu ndugu zake.”
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Sele Mgosi.”
Niliandika jina hilo kwenye notibuku yangu, kisha nikamwambia:
“Nipatie namba yako ya simu.”
Akanitajia namba ya simu yake. Nikaiandika, kisha nikairudisha notibuku yangu mfukoni.
“Sawa. Nitakapokuhitaji nitakupigia simu.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya hapo nilitoka katika kile chumba. Polisi walikuwa wameshaupakia ule mwili kwenye gari tayari kuupeleka hospitali. Na mimi nikapanda kwenye gari na kuondoka.
Nilikwenda makao ya polisi, nikamfahamisha afisa upelelezi kuhusu tukio la mtu aliyenyongwa eneo la Kwaminchi.
“Umekwenda kumshuhudia?” afisa upelelezi akaniuliza.
“Nimekwenda na nimesharudi. Mwili wake umepelekwa hospitali.”
“Ni nani?”
“Nafikiri ni yule mtu ambaye alitajwa na yule msichana tuliyezungumza naye. Aliniambia anaitwa Chinga, lakini leseni yake ina jina la Pascal Laizzer.”
Niliitoa ile leseni na kumuonesha afisa upelelezi. Afisa upelelezi aliitazama, kisha akaniuliza:
“Huyu ndiye aliyenyongwa?”
“Ndiye yeye.”
“Umethibitishaje kuwa yeye ndiye Chinga?”
“Lazima atakuwa ni Chinga. Tumekuta kipande cha karatasi kwenye shingo yake, kama ambavyo tulikikuta kwa wenzake. Kimeandikwa: ‘Huyu ni wa mwisho.’”
Nilikitoa kipande hicho cha karatasi kutoka mfukoni mwangu na kumuonesha. Afisa upelelezi alikitazama, kisha akaniambia:
“Mnyongaji ni yule yule. Hapa anatuthibitishia kwamba amemaliza kazi. Sasa tutakuwa na kazi moja tu ya kumtafuta yeye.”
“Shuhuda mmoja anayeishi nyumba aliyokuwa akikaa marehemu Pascal ameniambia amemuona mtu aliyekuwa pamoja na marehemu muda mchache kabla ya kukutwa amenyongwa. Nina shaka kwamba yeye ndiye aliyewanyonga wote.”
“Amekueleza muonekano wake?” afisa upelelezi akaniuliza.
“Baada ya kuniambia hivyo sikumhoji mengi. Nitamuita baadaye ofisini na nitamuonesha picha ya mtu ambaye tunamshuku. Kama atathibitishia ndiye yeye, muuaji tutakuwa tuko naye mikononi. Wakati wowote tunaweza kumtia mbaroni.”
“Sasa hilo si la kusubiri baadaye. Nenda ofisini, kampigie simu aje ofisini kwako. Nataka hili suala likifika kwa wakubwa tuwe na majibu ya kuwapa.”
“Sawa afande, acha niende.”
Nikainuka na kutoka. Kabla ya kupanda gari nilimpigia simu Sele Mgosi, shuhuda aliyekuwa akiishi katika nyumba iliyotokea tukio la mtu aliyenyongwa.
“Unazungumza na Inspekta Fadhil wa kituo cha polisi cha Chumbageni,” nikamwambia Mgosi mara tu alipopokea simu.
“Nazungumza na nani?” Mgosi akaniuliza kwa sauti ya hofu kidogo.
“Inspekta Fadhil. Tuliongea dakika chache zilizopita hapo Kwaminchi nikachukua namba yako.”
“Ndiyo inspekta, unasemaje?”
“Ninakuhitaji ufike kituo cha polisi cha Chumbageni sasa hivi. Ukifika, taja jina langu, utaletwa ofisini kwangu. Sawa?”
“Sawa. Nitafika.”
Nikakata simu na nikapanda gari. Nilifika kituo cha polisi, nikashuka kwenye gari na kuingia ofisini kwangu. Nikiwa nimekaa kwa dakika chache mlango wa ofisi yangu ukabishwa.
“Pita ndani,” nikasema.
Mlango ukafunguliwa. Nikamuona Sele Mgosi akiingia.
“Karibu kiti,” nikamwambia.
Mara tu alipokaa, kitu cha kwanza nilimtolea picha ya Thomas Christopher, mtu ambaye tulikuwa tunamtafuta kuhusiana na mauaji ya watu wote watatu waliokuwa wamenyongwa. Picha yake niliipata kutoka ofisi za kampuni ya simu baada ya kuwapelekea namba ya simu yake niliyoipata kutoka katika simu ya mtu wa kwanza kunyongwa.
“Huyo mtu ambaye ulimuona leo amefuatana na marehemu, ndiye huyo hapo?” nikamuuliza Mgosi baada ya kumpa ile picha.
Mgosi hakunijibu kwa haraka, aliendelea kuitazama picha hiyo kisha akaniambia:
“Sina uhakika sana kwamba ndiye au siye. Mtu mwenyewe nilimuona mara moja tu, halafu mtu aliyeko katika hii picha anaonekana kuwa kijana sana kuliko niliyemuona.”
“Tunachohitaji ni kufanana, si ujana au uzee. Mtu unaweza kutumia picha uliyopiga zamani ukiwa kijana.”
Mgosi akatikisa kichwa.
“Siwezi kusema ndiye au siye, labda kama nitamuona yeye mwenyewe.”
“Tunamtafuta. Tukimpata tutakuita umtambue, anaweza akawa tofauti na hii picha.”
“Mimi nasubiri akamatwe nije nimtambue,” Mgosi akaniambia huku akinirudishia picha hiyo.
“Na wewe ukimuona tena mitaani tafadhali nipigie simu unijulishe.”
“Sawa. Nitafanya hivyo.”
Baada ya Mgosi kuondoka ofisini kwangu, na mimi nikatoka. Nikapanda gari na kuelekea Chuda. Dakika chache baadaye nikalisimamisha gari mbele ya geti la jumba moja la kifahari, ambalo namba yake ndiyo iliyoandikwa katika usajili wa namba ya simu ya Thomas Christopher.
Nilishuka kwenye gari nikaenda kubisha geti. Sekunde chache baadaye geti likafunguliwa na msichana yule yule ambaye niliongea naye siku ya kwanza nilipofika katika jumba hilo.
“Hali yako?” nikamsalimia.