Kiungo mshambuliaji kutoka Zambia, Clatous Chama, amemalizana na klabu ya Singida Black Stars baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea timu hiyo katika msimu wa 2025/26.
Chama, ambaye msimu uliopita (2024/25) alikuwemo kwenye kikosi cha Yanga SC, alikuwa huru baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kumalizika. Nyota huyo awali alijiunga na Yanga akitokea Simba SC, na akawa miongoni mwa wachezaji waliotajwa kwa kishindo kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa, Singida Black Stars imemvutia Chama kwa dau nono la usajili na mshahara wa kuvutia, hali iliyomshawishi kukataa mipango ya awali iliyomhusisha na Zesco United ya Zambia pamoja na Azam FC ya Tanzania.
Nyota huyo ataungana na kiungo mkabaji raia wa Uganda, Khalid Aucho, ambaye tayari ametambulishwa ndani ya kikosi hicho. Singida Black Stars kwa sasa ipo kambini jijini Dar es Salaam kwa maandalizi ya msimu mpya na pia inatarajiwa kushiriki Kagame Cup 2025.
Mchezo wa kwanza wa maandalizi kwa Singida Black Stars utafanyika Septemba 2, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, ambapo watapambana na Ethiopian Coffee.
Related