Daraja jipya laibua kicheko kwa wasafiri, madereva

Kibaha. Wananchi, madereva na wasafirishaji waliokuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya usafiri kila msimu wa mvua eneo la bonde la maji, Ruvu, Kibaha mkoani Pwani, sasa wamefurahi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja jipya la mita tano lenye thamani ya Sh1.5 bilioni.

Kwa miaka mingi, eneo hilo lilikuwa kikwazo kikubwa kwa usafiri, kwa sababu maji yalipozidi, yalifunika barabara na kusababisha magari kusimama kwa saa kadhaa, mengine kusombwa na maji.

Akizungumza leo Jumatatu, Septemba Mosi, 2025 akiwa eneo hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Pwani, Baraka Mwambage amesema ujenzi wa daraja hilo umekamilika ndani ya miezi 10 kwa kuzingatia masharti ya mkataba.

“Kwa muda mrefu eneo hili lilikuwa kero kubwa hasa nyakati za mvua. Abiria na wasafirishaji walilazimika kusubiri maji yapungue ndipo waendelee na safari na magari na hata binadamu walishuhudiwa wakisombwa,” amesema Mwambange.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo sasa, kunaondoa changamoto hiyo na shughuli za usafiri na usafirishaji zitafanyika bila usumbufu.

Mwambage amesema barabara hiyo ni moja ya njia kuu za kimkakati nchini, ikipitisha wastani wa magari 19,000 kwa siku, huku zaidi ya magari 740 yakipita kwa kila saa.

 Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi Tanzania (Wamata), Majura Kafumu akizungumzia ahueni hiyo, amesema daraja hilo limekuwa suluhisho la matatizo waliyokuwa wakiyapata kwa muda mrefu.

“Kila msimu wa mvua tulikuwa tukipata adha kubwa; safari zilisimama, foleni zilikuwa kero na abiria walilalamika sana. Sasa tunaamini usafirishaji utakuwa wa uhakika bila hofu ya maji,” amesema Kafumu.

Madereva wa magari ya abiria na mizigo waliozungumza na Mwananchi wameelezea furaha yao, akiwamo Madua Rashid aliyesema daraja hilo limeondoa mzigo wa kiakili uliokuwa ukiwasumbua kila mvua inaponyesha.

“Tulikuwa tukiendesha kwa shaka, tukijua mvua ikinyesha barabara inakatika. Lakini sasa tunasafiri bila wasiwasi. Hii ni faraja kubwa kwetu,” amesema Rashid.

Athumani Alfani, dereva mwingine, amesema; “Hii ni neema kubwa. Kila tulipopata changamoto eneo la Ruvu tulichelewa kufikisha mizigo na abiria. Hali hiyo ilisababisha hasara na malalamiko. Sasa tumepata tumaini jipya.”