Dk Nchimbi awaahidi makubwa Simiyu, wananchi wataka utekelezaji

Busega. Wakati mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi akiwaahidi wana Busega, mkoani Simiyu miradi mbalimbali, wananchi nao wamekitaka chama hicho kuzitekeleza kwa vitendo.

Wamesema kuahidi ni jambo moja na kuzitekeleza ni suala jingine, hivyo mgombea Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wanapaswa kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa ndani ya miaka mitano na si vinginevyo.

Wamesema hayo leo Jumatatu, Septemba 1, 2025 katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Mkula, Jimbo la Busega na Dutwa, Jimbo la Bariadi Vijijini.

Mbali na kueleza kile wanakwenda kukifanya miaka mitano ijayo iwapo watapewa dhamana, Dk Nchimbi amewanadi wagombea ubunge, Saimon Sangu wa Busega na Masanja Kadogosa wa Bariadi Vijijini. Madiwani nao wa maeneo hayo amewaombea kura.

Akiwa Mkula, Dk Nchimbi amesema miaka mitano iliyopita wamejenga vituo vya afya vinne, hospitali moja ya wilaya, zahanati saba, shule za sekondari tisa, madarasa yalikuwa 1,043 sasa yamefika 1,342.

Ameendelea kubainisha mafanikio kuwa miradi ya maji mipya 15 zaidi ya Sh15 bilioni zimetumika ukiwamo mradi mkubwa wa maji Lamadi- Mkula ambao umesababisha watu asilimia 73 kupata majisafi.

Amesema kutokana na mbegu bora na ruzuku imechagiza kilimo kupiga hatua, choroko kilo moja ilikuwa Sh2,700 sasa ni Sh3,200, alizeti ilizalishwa tani 1.2 hadi sasa ni tani 5.7, kwenye mifugo majosho matano yamejengwa.

Amebainisha wanachokwenda kufanya miaka mitano ijayo, Dk Nchimbi kuwa wanakusudia kujenga vituo vipya vya afya vinne, zahanati mpya nne, sekondari mpya tano, shule za msingi mpya mbili na madarasa 76 kwenye shule zote.

Akiwa Dutwa kwenye mkutano uliofanyikia Uwanja wa CCM, Dk Nchimbi amesema Samia yupo tayari kuendelea kuwatumikia Watanzania na kinachopaswa kukifanya ni Oktoba 29, 2025 kwenda kumpigia kura nyingi.

Mwananchi imezungumza na wananchi waliohudhuria mikutano hiyo, Mkula na Dutwa na kueleza kile ambacho wanataka kifanyike baada ya Dk Nchimbi kueleza waliyofanya na yake wanayotarajia kwenda kufanya miaka mitano ijayo.

Emmanuel Mtondo, mkazi wa Manara  Kata Bagudu, Jimbo la Busega amesema mgombea huyo aendelee kutoa taarifa za kile wanachokwenda kuwafanyia pindi watakapowachagua.

“Mama Samia hizo ahadi alizotoa azikamilishe kwelikweli, isije kuwa ahadi hewa. Sisi tutaaendelea kuwa pamoja naye katika kumpa kura,” amesema Mtondo.

Mathias Busobangija, mkazi wa Nyamkono, Busega amesema waendelee kutuchapia kazi.

“Wafanye kazi kwa bidii na kutekeleza wanachokisema. Wasiishie kutoa ahadi pekee.”

James Mahushi, mkazi wa Maswa amesema sera ni nzuri kwa kuwa, zinakwenda kuimarisha maisha ya wananchi, kama kweli zitatekelezeka maisha yao yatakuwa bora zaidi.

“Mimi msisitizo wangu ni kwamba waende wakaitekeleze Ilani ambayo wameahidi. Kwani wakitekeleza wanakuwa wamefikia malengo ya wananchi lakini wasipofanya vizuri kazi kwao,” amesema Mahushi.

Catherine John, mkazi wa Guriati, Bariadi Vijijini amesema kwa kuwa watakuwa wameapa kutekeleza, hivyo wanapaswa kutenda kwa vitendo.

“Hajadanganya wananchi, amemdanganya Mungu, kwa hiyo ni wao wenyewe kutekeleza waliotuahidi,” amesema Catherine.

Catherine amesema eneo ambalo wanapaswa kulitizama kwa ukaribu kwani ni changamoto ambayo tutakutana nayo.

Nanai, Dk Chegeni waitwa jukwaani

Katika mkutano wa Mkula, Dk Nchimbi amewaita jukwaani Dk Raphael Chegeni na Francis Nania akisema: “Hapa nina marafiki zangu, Nanai na Chegeni, sasa kama hawapo na wameniambia ni nyumbani kwao nitashangaa.”

Nanai na Dk Chegeni walikuwapo, wakasogea jukwaani na kila mmoja akapata wasaa wa kuzungumza kwenye mkutano huo mkubwa wa kampeni. Wawili hao walikuwa miongoni mwa watiania wa ubunge wa Busega.

Nanai aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), ameanza kwa kusema: “Sikujua kama kutakuwa na protokali hii,  lakini Mungu ni mwema, kila wakati.”

“Balozi Nchimbi, tumeshiriki kura za maoni vizuri, lakini kikubwa chama kimeteua. Tunakipenda chama chetu.

“Sisi ambao hatukupata fursa za kugombea ubunge hatuna nongwa, mimi namuunga mkono ndugu yangu na mdogo wangu Songe,” amesema Nanai.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa zamani wa Mwananchi Communications Limited (MCL) huku akishangiliwa amesema: “Niwaombe Watanzania wote, wana CCM wote, tumevunja makundi, kambi zote na kambi yetu ni moja tu ya CCM. Tuhakikishe Samia, wabunge na madiwani wanashinda kwa kishindo.”

Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa Busega, Dk Raphael Chegeni amesema CCM imemteua wagombea safi wa madiwani, wabunge na urais: “Na kutokana na hilo, hatuna shaka kabisa na ushindi wa kishindo tarehe 29 Oktoba.”

“CCM imetekeleza ilani vizuri sana na haya ni matokeo mazuri, tunasema Samia … mitano tena,” amesema.

Dk Chegeni amesema uchaguzi umekwisha: “Kwenye CCM huwa tunapambana sana lakini baada ya kumalizika tunasema chama kwanza, mtu baadaye. Namuunga mkono mgombea wetu wa ubunge, Simon Songe. Katika hili CCM huwa tunakuwa pamoja.”