Dube afichua siri ya kambi, amtaja Folz

KAMBI ya Yanga inayojiandaa na msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2025-26, imezidi kunoga kwa kocha Romain Folz kuendelea kuwapika mastaa wa timu hiyo, huku akikomalia mechi za kirafiki kujenga utimamu wa wachezaji wake, lakini nyota wa kikosi hicho Prince Dube amevunja ukimya na kuzungumzia vita ya namba kutokana na ongezeko la wachezaji wapya.

Dube amekiri ongezeko la wachezaji wapya katika eneo la ushambuliaji analotumika yeye kwa sasa limeongeza ushindani, licha ya kutamba kuwa hana presha, isipokuwa kunamuongezea ubora zaidi.

Hadi sasa Yanga imeshacheza mechi mbili za kirafiki tangu ilipotoka Rwanda kucheza na Rayon Sports na kuifunga mabao 3-1, kwa kuinyuka Fountain Gate kwa mabao 2-1, yaliyowekwa wavuni na Prince Dube na Aziz Andambwile na juzi imeifunga Tabora United 4-0, mabao yakifungwa na Pacome Zouzoua, Prince Dube na Celestin Ecua aliyetupia mbili.

Dube ambaye msimu uliopita alifunga mabao 13 ya Ligi Kuu akiwa nyuma ya Clement Mzize aliyefunga 14, hadi sasa katika mechi za kutesti mitambo akiwa ameshatupia mawili, aliliambia Mwanaspoti, hana presha juu ya ujio wa wachezaji wapya katika eneo analocheza na badala yake anafanya kazi yake kwa kuhakikisha anaonyesha uzoefu wa ligi na uwezo alionao.

Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Yanga akitokea Azam FC, akiwa tayari ametwaa mataji matano msimu uliopita, alisema ujio wa washambuliaji ni faida kwa klabu na imeongeza ushindani mkubwa, lakini kwake pia kwani anapambana kuhakikisha anafanya kilicho bora zaidi msimu ujao.

“Kuongezewa changamoto inaweza kukujenga na kukuangusha pia lakini naweza kusema nimeshakuwa mkomavu kwenye mpira, siwezi kuwa na presha, zaidi napambana kuonyesha uwezo ili kujihakikishia nafasi niliyonayo ndani ya timu,” alisema straika huyo raia wa Zimbabwe aliyeongeza;

“Nimeangalia usajili uliofanywa, kuna wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa. Ni nafasi yangu kuendelea nilipoishia kwa kuipambania timu na mimi binafsi sio rahisi kutokana na uwepo wa kocha mpya, mchezaji yeyote anaweza kupata namba kulingana na namna atakavyoonyesha kwenye uwanja wa mazoezi.”

Dube alisema anajua kuzembea kidogo katika kuwania namba kutamfanya akalie benchi kitu ambacho hakuna mchezaji anayependa kimtokee hasa mwenye kiu ya kufanya makubwa kikosini.

Mshambuliaji huyo alisema Yanga ilimuamini ana kitu cha ziada cha kuisaidia timu na hilo ndilo jukumu la kwanza atakalofanya kwa kuipigania iwe katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako anajua wanachama na mashabiki wana kiu ya kuona inafika mbali zaidi.

Wakati Dube akiyasema hayo, kocha Folz ameendelea kugawa dozi kwa wachezaji, huku akikomaa zaidi na safu ya ushambuliaji ambayo ndio inaonyesha makali zaidi kwa kutupia mabao kambani na ametoa nafasi kwa washambuliaji wote waliopata nafasi ya kufunga ikiwa ni pamoja na Andy Boyeli aliyetupia akiwa Rwanda pamoja na Pacome walipoifunga Rayon Sports 3-1. Bao jingine la tatu lilifungwa na nahodha, Bakar Mwamnyeto.

Inadaiwa kocha huyo muumini mkubwa wa kutumia nafasi kila inayotengenezwa na tayari uongozi wa klabu hiyo umefanya usajili wa maana eneo hilo ambalo tayari lilikuwa na Dube, Clement Mzize na sasa wameongezewa nguvu kwa kuongezwa Andy Boyeli na Celestin Ecua.

Yanga inaendelea kujifua tayari kwa mechi ya kirafiki ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi itakayofanyika Septemba 12, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kucheza na Bandari Kenya itakayotumika kutambulisha kikosi kipya cha msimu wa 2025-26.

Baada ya hapo Yanga itacheza na Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii siku ya Septemba 16 kisha kusafiri hadi Angola kuifuata Wiliete Banguela katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa kati ya Septemba 19 na kurudiana jijini Dar Septemba 27.