Benki ya Equity imesema zaidi ya asilimia 80 ya miamala yake inafanyika kidigitali, hatua inayodhihirisha kasi ya ukuaji wa teknolojia katika sekta ya fedha,huduma hizo zinajumuisha mfumo wa uwakala ambao umeendelea kuwa njia kuu ya kuwafikishia wananchi huduma za kibenki bila kulazimika kufika kwenye matawi ya benki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Jukwaa la Mawakala, Mkuu wa Kitengo cha Malipo kutoka Equity Tanzania, Haidary Chamshama, amesema benki hiyo imejipanga kuwekeza zaidi kwenye elimu na mafunzo kwa mawakala wake,Mafunzo hayo yanahusu usimamizi bora wa fedha, ulinzi na usiri wa taarifa za wateja pamoja na njia za kuzuia utakatishaji wa fedha, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa.
Aidha Chamshama ameongeza kuwa kwa sasa Equity ina mawakala zaidi ya elfu tatu nchi nzima, na matarajio yake ni kuongeza idadi hiyo ili huduma za kibenki ziwafikie wananchi wengi zaidi,huduma zinazotolewa kupitia mawakala zinahusisha uwekaji na utoaji wa fedha, ulipaji wa bili na hata kufungua akaunti mpya, jambo linalochochea ujumuishi wa kifedha na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, mmoja wa mawakala walioshiriki katika jukwaa hilo, Chacha Magaigwa, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa mpana wa namna bora ya kumhudumia mteja na kutambua viashiria vya utakatishaji fedha,na kuongeza kuwa elimu hiyo si tu kwamba itaboresha huduma, bali pia itaongeza imani ya wateja na kuchochea ukuaji wa biashara za kifedha katika ngazi ya jamii.