SINGIDA Black Stars leo usiku inaanza kampeni ya kusaka taji la kwanza msimu huu itakapovaana na Coffee ya Ethiopia katika michuano ya Kombe la Kagame, huku kocha mkuu Miguel Gamondi akiwataja mastaa watatu wa zamani wa Yanga.
Gamondi amesema uwepo kwa Khalid Aucho, Clatous Chama na Nickson Kibabage utamsaidia katika mechi kubwa za ndani na michuano ya kimataifa kutokana na uzoefu walionao sambamba na nguvu iliyopo ya mastaa wengine waliopo kikosini.
Singida iliyomaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Yanga ikipoteza kwa mabao 2-0, imepangwa Kundi A la michuano ya Kagame na pia itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kuumana na Rayon Sports ya Rwanda katika mechi za raundi ya kwanza.
Hata hivyo, licha ya kuwa na ratiba ngumu ya michuano hiyo miwili, Gamondi amesema uwepo wa majembe hayo aliyowahi kufanya nayo kazi akiwa Yanga itakuwa chachu ya kurahisisha mfumo wake, hivyo anaamini hatakuwa na kazi ngumu kwani watamsaidia kuwaunganisha nyota ambao hajafanya nao kazi.
Gamondi alisema ukiondoa uzoefu wachezaji hao wana vipaji vikubwa vya soka anaamini kuongezwa kwao kikosini ni chachu ya kuwa na timu yenye ushindani.
“Naupongeza uongozi kwa kukamiliasha usajili wa wachezaji hao ni usajili bora dirisha hili kutokana na ubora wa mchezaji mmoja mmoja, lakini uzoefu walionao nimefanya kazi nao nikiwa Yanga wamenipa matokeo mazuri na wanafahamu mifumo yangu,” alisema Gamondi.
“Naamini kuungana nao hapa watakuwa chachu ya kurahisisha mbinu zangu kwa kunisaidia wakikaa na wenzao tutarahisisha kuifanya timu iingie kwenye mfumo kwa uharaka zaidi lakini pia watakuwa chachu ya kupata matokeo tukikutana na timu kubwa na kimataifa pia.”
Gamondi alisema uwepo wa nyota hao pia ni sehemu ya kuwa na timu bora na shindani kwani tayari wameshafanya mambo makubwa katika Ligi wakiwa na timu kubwa za Simba na Yanga, hivyo inamuongezea urahisi wa kuandaa timu kwa vile ana wachezaji wakubwa wanaofahamu mbinu za wapinzani.
Akiwa Yanga, Gamondi aliipeleka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni baada ya miaka 25 tangu ilipocheza mara ya mwisho 1998 na aliiongoza hadi robo fainali na kutolewa kitatanishi na Mamalodi Sundowns ya Afrika Kusini.