Kigoma. Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo umefafanua kuhsu video iliyosambaa mitandaoni ikimuonesha muuguzi wa hospitali ya wilaya hiyo akitolewa kwa nguvu na mlinzi wa Suma JKT ndani ya wodi ya wajawazito, hali iliyosababisha sintofahamu miongoni mwa wananchi na wagonjwa waliokuwa wodini.
Video hiyo, iliyoanza kusambaa usiku wa kuamkia Agosti 31, 2025, ilimuonesha mhudumu wa afya akilalamika kuvamiwa na kuondolewa ghafla bila kujua kosa lake, huku ikidaiwa alikuwa akimsaidia mjamzito kujifungua na kutoa kondo la nyuma la uzazi.
Tukio hilo liliibua mjadala mtandaoni baada ya kusambazwa na watu waliodaiwa kuwa masamaria wema, ambao pia walilalamika kitendo cha muuguzi huyo kuondolewa kwa nguvu mbele ya wagonjwa wengine.
Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa Agosti 31, 2025, na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Juma Matelula, imeelezwa kuwa muuguzi huyo hakutolewa kwa sababu za kikazi, bali alikamatwa baada ya kunaswa katika mtego wa kuomba rushwa kwa mjamzito.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Agosti 28, 2025, saa 12 jioni, mama mmoja alifika hospitalini na kupatiwa huduma ya upasuaji (Cesarean Section) saa 1:40 usiku.
Ilielezwa kuwa siku iliyofuata, Agosti 29, 2025, uongozi wa hospitali ulipokea taarifa kutoka kwa wananchi waliodai muuguzi aliyemhudumia mama huyo aliomba rushwa ya Sh60,000 ili huduma hiyo itolewe. Mama huyo alishalipa Sh39,000, lakini alidaiwa kutakiwa kumalizia Sh21,000.
Baada ya kupokea malalamiko hayo, uongozi wa hospitali uliandaa mtego kwa kushirikiana na wananchi hao ili kubaini ukweli wa madai hayo. Wakati wa utekelezaji wa mtego huo, ndipo kukazuka mzozo ndani ya wodi ya wazazi ambapo muuguzi huyo alikuwa, hali iliyosababisha taharuki kwa wagonjwa na familia zao.
“Kwa lengo la kurejesha utulivu, uongozi wa hospitali uliamua kumwondoa muuguzi huyo kazini mara moja. Hata hivyo, mtumishi huyo alikaidi, jambo lililolazimu askari wa usalama kuingilia kati na kumtoa nje,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, imefafanuliwa kuwa wakati video hiyo ikirekodiwa, mgonjwa aliyedaiwa kuwa chini ya huduma ya muuguzi huyo tayari alikuwa amejifungua salama na aliruhusiwa hospitalini Agosti 30, 2025, akiwa na afya nzuri yeye na mtoto wake.
Taarifa hiyo imekanusha madai kwamba muuguzi huyo alikuwa bado anamtoa kondo la nyuma la uzazi kama ilivyodaiwa katika video hiyo.
Kwa sasa, muuguzi huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi, huku uchunguzi ukiendelea kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Uongozi wa Halmashauri umeahidi hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya mtumishi au watumishi wowote watakaobainika kuhusika katika vitendo vya rushwa.