KAMA ulidhani Yanga inapiga porojo katika ujenzi wa Uwanja pale Jangwani, tulia kwanza, kwani kuna mambo mazito yameshaanza na habari mpya ni rasmi mchakato wa kuongezewa eneo unakamilika leo Septemba Mosi.
Kuanzia kesho Jumanne (Septemba 2), Yanga itakuwa inamiliki eneo la mita za mraba 37,500 pale Jangwani ikiwa ni baada ya kukamilisha eneo ambalo waliliomba kwa serikali.
Yanga ilikuwa inataka kujenga uwanja wake katika eneo hilo la Jangwani ambalo awali kulikuwa na Uwanja wa Kaunda kabla ya kubomolewa, lakini sasa kwa mujibu wa ramani yao, eneo limeongezeka na uwanja utachukua mashabiki wasiozidi 30,000.
Kwa mujibu wa uongozi wa Yanga, eneo ambalo klabu hiyo inalimiliki halikuwa linatosha ndipo ikawasilisha maombi kwa serikali kuongezewa eneo la chini kidogo na uwanja wa zamani wa Kaunda.
Juni 9, 2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa akizungumza mbele ya wanachama wa klabu hiyo katika Mkutano Mkuu wa klabu hiyo aliithibitishia klabu hiyo kuwa maombi yao yatatekelezwa.
Kauli hiyo ya Mchengerwa imekwenda kwa vitendo baada ya kuongezwa kwa eneo la mita za mraba 2000 ambalo klabu hiyo ililiomba kwa serikali.
Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba leo Jumatatu, uongozi wa Yanga utakwenda kukamilisha umiliki wa eneo hilo kwa kulipia kodi stahiki kwa serikali.
Taratibu hizo zinatokana na kupitishwa kwa taratibu hizo za malipo na kikao cha Kamati ya Utendaji cha klabu hiyo kilichofanyika wiki iliyopita, makao makuu ya Yanga.
Baada ya malipo hayo Yanga itaweka mawe ya alama za umiliki wa eneo hilo, ambapo baada ya hapo zitabaki taratibu za ndani ya klabu hiyo kuanza mchakato wa ujenzi.
“Kila kitu kipo sawa, kuna malipo ambayo yatafanyika Jumatatu (leo), yakishafanyika hayo sasa tutakuwa tunamiliki rasmi eneo la ukubwa wa skwea mita 37,500 ambalo sasa litatutosha kabisa kwa ujenzi,” alisema bosi huyo wa juu ndani ya Yanga na kuongeza;
“Nadhani kila kitu baada ya malipo hayo kitatangazwa katika mkutano mkuu ambao utafanyika wikiendi ijayo.”
Yanga itakuwa na Mkutano Mkuu, Septemba 7 utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere ambao utakuwa na ajenda 10 tofauti.
Iko hivi. Katika uwanja huo, Yanga itashirikiana na mfadhili na mdhamini wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ ambaye Mwanaspoti linafahamu yuko tayari kutoa bajeti kubwa ya ujenzi wa uwanja huo.
Tayari Yanga imeshakamilisha michoro ya uwanja huo ambayo ilishawasilishwa kwa serikali kisha kupitishwa, hatua ambayo itabakiza kupatikana kwa mkandarasi atakayeanza ujenzi wa mradi huo.