BAADA ya mshambuliaji wa Mashujaa, Ismail Mgunda kurejea kucheza Ligi Kuu Bara amesema anatamani kutajwa katika orodha ya wafungaji wenye mabao mengi msimu unaoanza Septemba 17.
Mgunda katikati ya msimu uliyopita aliondoka Mashujaa akiwa amefunga mabao mawili kwenda kujiunga na AS Vita ya DR Congo ambako hata hivyo hakufanikiwa kutimiza ndoto kwa kile alichokitaja ni masilahi.
Alisema baada ya kurejea nchini alikuwa anafuatilia Ligi Kuu aliona ushindani mkali hasa kwa washambuliaji, hivyo akawa anafanya mazoezi ya kujipanga kuhakikisha anarejea akiwa fiti.
“Sikufanikisha lengo langu la kucheza kwa mafanikio nikiwa nje ambako ni tofauti na hapa nchini, mapro wanalipiwa nyumba wakati mwingine wanaishi kambini, kule kila kitu unajilipia mwenyewe, sasa pata picha ukiwa hulipwi mshahara kwa wakati,” alisema Mgunda na kuongeza:
“Kocha Youssouph Dabo ndiye aliyenisajili naye aliondoka kwa changamoto hiyo, hata nilipomshirikisha hilo akasema nifanye uamuzi wenye manufaa na mimi. Ndiyo maana nikaamua kurejea nchini.
“Natamani msimu unaoanza Septemba 17 uwe wa mafanikio kwangu pamoja na timu ya Mashujaa iliyosajili wachezaji wazuri kama Salum Kihimbwa akiwa Fountain Gate alimaliza na mabao manne na asisti tano, Selemani Bwenzi akiwa KenGold alimaliza na mabao matano, jambo litakaloniongezea ushindani na siyo kubweteka.”