JKT Queens kamili kwenda kuliamsha  CECAFA

KIKOSI cha wachezaji 26 wa JKT Queens sambamba na benchi la ufundi na viongozi wengine 23 kinatarajia kuondoka nchini leo Jumatatu, Septemba Mosi, 2025, kwenda Nairobi, Kenya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Safari hiyo itaanzia Moshi, Kilimanjaro ilipokuwa kambi ya timu hiyo tangu Agosti 9, 2025, kuwahi michuano hiyo itakayopigwa kuanzia Septemba 4-16.

Historia ya Tanzania CECAFA

JKT Queens ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu uliopita 2024/25 na hii ni mara ya pili kushiriki michuano ya CECAFA.

Mwaka 2023 ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga Benki ya Biashara ya Ethiopia  (CBE FC) kwa penalti 5-4.

Mara ya kwanza michuano hii ilichezwa 2021, Kenya na wenyeji Vihiga Queens kuibuka mabingwa kwa kuichapa CBE mabao 2-1 kwenye Uwanja wa MISC Kasarani.

Tanzania imewahi kupeleka timu mara tano, ambapo Simba Queens ilishiriki 2021 na kutolewa nusu fainali, kabla ya kuchukua taji 2022 kwa kuichapa She Corporate ya Uganda bao 1-0.

Mwaka 2023, JKT Queens ilitwaa ubingwa michuano ikifanyikia Uganda, lakini ikaishia hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

JKT Queens imesajili wachezaji wapya wanne akiwemo beki Esther Maseke (Bunda Queens), straika Asha Rashid (Simba Queens), Winfrida Castor (Young Princess) na Fumukazi Ally Nguruwe (Mashujaa Queens).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 3,  Msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire amesema wameimarisha kikosi kwa ajili ya mashindano haya makubwa na kuongeza:

“Ni idadi ya wachezaji wanne tuliowaongeza ili kuongeza nguvu. Pia benchi la ufundi lina Kocha Kessy Abdallah na mshauri Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ kuhakikisha tunaleta heshima ya taifa.”

Kauli za kocha na wachezaji

Kocha mkuu wa timu hiyo, Kessy Abdallah amesema wamejiandaa vyema kwa michuano hiyo:

“Tumejiandaa vizuri na matarajio yetu ni kufanya vizuri kila mchezo. JKT Queens ni timu kubwa, tumeshaweka historia, sasa tunataka kulichukua tena kombe hili na kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Wakati huohuo Nahodha, Anastazia Katunzi amesema: “Tunaahidi tutaendeleza tulipoishia, tumejiandaa vyema kulichukua tena kombe hili. Tumecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kilimanjaro Kombaini na kushinda 14-0.”

Mshambuliaji Stumai Abdallah ameongeza: “Tutacheza vizuri na tutahakikisha tunarudi na kombe nyumbani Tanzania. Niahidi tu ubora niliouonesha Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania utakuwa mara mbili yake katika mashindano haya.”

JKT Queens ipo Kundi C pamoja na JKU Princess (Zanzibar) na Yei Joint Stars (Sudan Kusini).

Kundi A lina Police Bullets (Kenya), Denden FC (Eritrea) na Kampala Queens (Uganda), huku Kundi B likiwa na CBE (Ethiopia), Top Girls Academy (Burundi) na Rayon Sports WFC (Rwanda).

RC Kilimanjaro  akabidhi bendera

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewakabidhi bendera ya taifa wachezaji hao jana Agosti 31 katika hafla iliyofanyika Mbugani Hotel, mjini Moshi.

Amewataka kudumisha nidhamu na kuonesha ushindani wa hali ya juu: “Sasa ninyi mnakwenda kutuwakilisha Watanzania. Timu hii ni ya Jeshi la Kujenga Taifa, lazima mtufanye tuone fahari,” amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa timu za JKT Tanzania, Luteni Kanali Godfrey Mvula, ameongeza:

“Tumejipanga vyema, benchi la ufundi limefanya kazi yao na viongozi wamewajibika, sasa tunaenda kushindana.”

Hamasa na shauku ya mashabiki

Mashabiki wa soka la wanawake nchini wameonyesha hamasa kubwa kuelekea safari ya JKT Queens ambapo Asha Mbwana, shabiki kutoka Moshi, amesema:

“Tunawaamini wasichana wetu. Tuliwashuhudia wakibeba kombe mwaka 2024, safari hii tunatarajia burudani zaidi na ubingwa tena. Tutawasindikiza kwa dua na hamasa kubwa.”

Rashid Mndeme, shabiki mkongwe wa JKT, ameongeza: “Tumewaona wakiweka bidii kambini. Tunajua wapo tayari na tunatarajia matokeo makubwa. Tuna imani hii timu itarudi na taji, na Watanzania wote tunapaswa kuwa pamoja nao.”

Septemba 5, JKT Queens itaanza kuminyana na JKU Princess ya Zanzibar, kisha Septemba 9 itakabiliana na Yei Joint Stars kutoka Sudan Kusini, kabla ya kufunga hesabu za hatua ya makundi Septemba 14 dhidi ya wapinzani wake wa mwisho.