JKU ya Zanzibar imeanza vizuri mashindano ya Tanzanite Pre-Season International baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mchezo huo wa Kundi C uliochezwa leo Septemba Mosi, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, mshambuliaji wa JKU, Koffy Hamza ndiye aliyepeleka kilio kwa TDS.
Hamza alianza kuifungia JKU dakika ya tano kufuatia kuwazidi ujanja walinzi wa TDS na kuuweka mpira kimiani.
TDS ambayo ni timu iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ikiibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi, ilionekana kupambana kusawazisha bao hilo, lakini juhudi hizo zikagonga mwamba.
Dakika ya 37, Hamza aliongeza bao la pili na kuifanya JKU kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Kocha wa TDS, Aggrey Moris, alikuja na mpango tofauti wa kushambulia zaidi lango la wapinzani wao, lakini vijana wake hawakufanikiwa kuuweka mpira kwenye nyavu.
Dakika 45 za kipindi cha pili cha mchezo huo ulioanza saa 7:00 mchana, zilikuwa za kushambuliana kwa zamu na hadi mwamuzi anapuliza filimbi ya mwisho, JKU ilitoka kifua mbele kwa mabao 2-0.
Michuano hiyo iliyoanza jana Agosti 31, 2025, imezinduliwa rasmi leo Septemba Mosi lilipofanyika zoezi la kutambulisha zawadi mbalimbali za washindi likiwemo kombe atakalokabidhiwa bingwa.
Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanafanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yameanza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025, yakiandaliwa na Fountain Gate FC.
Jumla ya timu 10 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A lina timu tatu za Bandari ya Kenya, Fountain Gate na Tabora United zote za Tanzania Bara.
Kundi B zipo Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union zote za Tanzania Bara wakati Kundi C kuna Namungo kutoka Tanzania Bara, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).