Dar/Mikoani. Wakati Chama cha Demokrasia Makini kikizindua kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kesho Jumanne, vyama vinne vimepishana na ratiba ya uzinduzi wa kampeni zao iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kujinadi kwa wananchi.
Wakati kampeni zikiingia siku ya tano leo tangu zianze Agosti 28 mwaka huu, mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan kesho atazungumza Songwe.
Samia anaendelea kujinadi kwa wananchi baada ya kumwaga sera zake katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Akiwa mjini Morogoro, mbali na kuahidi kuendeleza miradi ya huduma za kijamii kwenye elimu, afya, maji na miundombinu, miongoni mwa ahadi zake kwa wanamorogoro wakimpa ridhaa, ni kuufanya mkoa huo kuwa wa viwanda akilenga kurejesha hadhi yake ya zamani.
Pia, ameahidi kuendeleza jitihada za kumaliza migogoro ya ardhi hasa katika Wilaya ya Kilosa kwa kutumia programu ya ‘Tutunzane’ iliyoonesha mafanikio katika Wilaya ya Mvomero kwa kuongeza maeneo ya wafugaji.
Samia alitoa ahadi nyingine alipokuwa mkoani Dodoma, akiahidi kuupa hadhi yake kama makao makuu ya nchi kabla ya kufanya kampeni zake Songwe, mkoa ambao watu wake wanajishughulisha zaidi na kilimo, biashara na uchimbaji wa madini.
Mbali na Samia, mgombea mwenza, Dk Emmanuel Nchimbi ameendelea kukinadi chama mkoani Simiyu kwa kuahidi miradi mbalimbali.
Hata hivyo, wananchi wa eneo hilo wamekitaka chama hicho kuzitekeleza kwa vitendo wakisema, kuahidi ni jambo moja na kuzitekeleza ni suala jingine.
Hivyo, mgombea urais na mgombea mwenza wanapaswa kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa ndani ya miaka mitano kama watapatiwa ridhaa ya kuendelea kuiongoza Serikali.
Katika mikutano ya kampeni ya CCM iliyofanyika Mkula, Jimbo la Busega na Dutwa, Jimbo la Bariadi Vijijini jana, mbali na kueleza kile wanachokwenda kukifanya miaka mitano ijayo iwapo watapewa dhamana, Dk Nchimbi pia amewanadi wagombea ubunge, Saimon Sangu wa Busega na Masanja Kadogosa wa Bariadi Vijijini na madiwani wa maeneo hayo.
Akiwa Dutwa kwenye mkutano uliofanyikia Uwanja wa CCM, Dk Nchimbi alisema mgombea urais Samia yupo tayari kuendelea kuwatumikia Watanzania na kinachopaswa kukifanya ni Oktoba 29, 2025 kwenda kumpigia kura nyingi.
Hata hivyo, wananchi waliohudhuria mikutano hiyo walieleza kile wanachotaka kifanyike baada ya Dk Nchimbi kueleza waliyofanya na yale wanayotarajia kwenda kuyafanya ndani ya miaka mitano ijayo.
Emmanuel Mtondo, Mkazi wa Manara Kata Bagudu, Jimbo la Busega alisema mgombea huyo aendelee kutoa taarifa za kile watakachowafanyia pindi watakapowachagua.
Mathias Busobangija, Mkazi wa Nyamkono, Busega alisema: “Waendelee kutuchapia kazi. Wafanye kazi kwa bidii na kutekeleza wanachokisema. Wasiishie kutoa ahadi pekee.”
James Mahushi, mkazi wa Maswa alisema sera ni nzuri kwa sababu zinaenda kuimarisha maisha ya wananchi, kama zitatekelezwa maisha yao yatakuwa bora zaidi.
“Mimi msisitizo wangu ni kwamba waende wakaitekeleze ilani ambayo wameahidi. Wakitekeleza wanakuwa wamefikia malengo ya wananchi, lakini wasipofanya vizuri kazi kwao,” alisema Mahushi.
Wakati CCM ikiendelea kujinadi, vyama vitatu kati ya tisa havijazindua kampeni zao, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na INEC.
Vyama hivyo ni National Reconstruction Alliance (NRA), Alliance Democratic for Change (ADC), United Democratic Party (UDP) na National League for Democracy (NLD) ambavyo kwa mujibu wa ratiba, vilipaswa kuanza kampeni tangu Agosti 28, 2025.
NRA kilipaswa kuanza kampeni Agosti 28, mjini Kigoma sanjari na ADC kilichotakiwa kuanza kampeni siku hiyo jijini Mwanza.
UDP na NLD vyenyewe vilipaswa kuanza kampeni jana jijini Mwanza na Dar es Salaam, vyote havijaanza huku baadhi vikieleza sababu za kuchelewa.
Mgombea urais wa NLD, Doyo Hassan Doyo alisema wao watazindua kampeni zao Septemba 4, jijini Tanga na ratiba ambayo wameshindwa kuitekeleza jana, wataifidia kwenye ratiba mpya itakayotoka.
“Tulipaswa kufanya kampeni Septemba mosi, Dar es Salaam, hata hivyo tumesogeza uzinduzi wetu hadi Septemba 4, hii ratiba ni ya mwezi mmoja, itakapotoka ratiba mpya, tutaona namna tutakavyoi-fix ili kufanya kampeni Dar es Salaam ambako safari hii tumeshindwa kufanya,” alisema.
Katibu wa NRA, Hassan Almas alisema kampeni bado mbichi na wao bado hawana ratiba ya kuzindua kwa sasa.
“Tutakapokuwa tayari tutasema lini tutazindua, bado kampeni ni mbichi, hivi sasa tunafanya ziara ya kuwatembelea wananchi na wagombea wetu, leo tumefanya Dar es Salaam na kesho tutakuwa Kilimanjaro, tutakapokuwa tayari kwa uzinduzi tutasema,” alisema Almasi.
Mwenyekiti wa ADC, Shaban Itutu alisema wao watazindua kampeni zao Septemba 7 mwaka huu, jijini Mwanza huku akibainisha kwamba, ratiba waliyoshindwa kuikamilisha kwa sasa wataifidia baada ya ratiba mpya kutoka.
“Hii ratiba ya sasa inaisha Septemba 28, kisha inatoka ratiba mpya, hivyo tutafidia,” alisema Itutu.
Mwananchi iliwatafuta viongozi wa Chama cha ADC kuzungumzia mkwamo wao, lakini simu zao ziliita bila majibu.
Chama cha Demokrasia Makini
Hata hivyo, kesho Jumanne, Chama cha Demokrasia Makini kitazindua kampeni zake kwenye Uwanja wa Bakhresa, Manzese jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ameir Hassan ameiambia Mwananchi kuwa moja ya ajenda yao kuu katika uzinduzi huo ni amani akibainisha kwamba, bila amani, hakuna kinachofanyika, hivyo chama chao kitazindua kampeni zake kikiwa na kauli mbiu ya ‘Amani.’
“Wananchi waje kusikia sera zetu, tunakwenda kufanya nini wakitupa ridhaa ya kushika dola, lakini kikubwa tunachokwenda kukisisitiza kwenye uzinduzi wa kampeni zetu kesho ni amani,” alisema Hassan.
Tayari vyama vya CCM, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wakulima (AAFP), Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Kijamii (CCK), vimeshazindua kampeni zao kwa mujibu wa ratiba ya INEC.
Ratiba hiyo inaonesha kesho, Chaumma kinaendelea na kampeni zake mkoani Tanga atakuwa mgombea wa urais na makamu wake mkoani Morogoro.
CUF itakuwa mkoani Mara, Chama cha Demokrasia Makini, Dar es Salaam, UDP Simiyu na ADC kitakuwa mkoani Tanga huku mgombea mwenza atakuwa mkoani Kilimanjaro.
Chama cha NLD, kitakuwa jijini Dar es Salaam wilayani Kinondoni na Ilala huku NRA kwa mujibu wa ratiba hiyo mgombea wake wa urais atakuwa mkoani Morogoro na mgombea mwenza wake atakuwa Ruvuma.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Peter Elias na Ibrahim Yamola