Dar/Mikoani. Upatikanaji duni wa huduma ya maji safi na salama, migogoro ya ardhi, miundombinu, uhaba wa ajira na kipato kwa wananchi, ndizo changamoto zilizoteka vinywa vya wagombea urais wa vyama mbalimbali vya siasa ndani ya siku tano za mwanzo za kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Tayari kampeni hizo zimeshafanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Morogoro, huku baadhi ya wagombea wakitarajia kuanza katikati ya Septemba katika mikoa mbalimbali nchini.
Tangu kuanza rasmi kwa kampeni hizo Agosti 28, 2025, ni Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Wakulima (AAFP) na Chama cha Kijamii (CCK), ndivyo ambavyo tayari vimeshazindua kampeni za urais.
CCM, Chaumma na CCK vilizindua kampeni zao za wagombea urais jijini Dar es Salaam, huku CUF kikizindulia Mwanza, AAFP kikifanya hivyo katika Mkoa wa Morogoro.
Hoja kuhusu kipato kwa wananchi imeibuliwa na mgombea urais wa CCK, David Mwaijolele, aliyesema atakomesha mikopo ya “kausha damu” inayowaumiza na kuwaacha Watanzania katika umaskini.
Katika uzinduzi wa kampeni zake jijini Dar es Salaam, aliwahimiza wananchi wamchague ili akakomeshe changamoto hiyo na kuja na mikopo ya “ongeza damu” badala ya kausha damu.
Ukiacha hilo, mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, amesema miundombinu, hasa ya barabara, ni miongoni mwa mambo watakayoyashughulikia iwapo watachaguliwa kuiongoza Tanzania kwa mara nyingine.
Kwa upande wa mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, kwa nyakati tofauti akiwa kwenye mikutano yake ya kampeni, pia amezungumzia suala la kuboresha miundombinu, kumaliza migogoro ya ardhi na upatikanaji wa maji.
Mgombea urais kupitia AAFP, Kunje Ngombale-Mwiru akiwa mkoani Morogoro, alisema atahakikisha anasimamia utekelezwaji wa miradi ya barabara ili kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema miundombinu hiyo itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji, huku akigusia kutengeneza mazingira ya wananchi kupata ajira ili wainue vipato vyao.
Ramadhan Issa, mkazi wa Igoma jijini Mwanza, anasema maeneo ya pembeni ya mji yanakabiliwa zaidi na uhaba wa maji.
“Tusidanganyane, yaani kwa hapa Mwanza tatizo kubwa ni maji, haya mambo mengine kama barabara yanavumilika, lakini maji hayana mbadala,” amasema Issa.
Anaongeza: “Hasa kwa sisi wengine tunaoishi pembeni ya mji ni kero sana. Kwa hiyo hili jambo kama wataweza basi watusadie, halafu inashangaza hapa Mwanza tuko pembeni kabisa ya ziwa, halafu tunakosa maji.”
Kama alivyosema Issa, Amina Joseph, mkazi wa Luchelele jijini Mwanza, naye anasisitiza tatizo hilo la maji, akitaka lipatiwe suluhisho la kudumu kupitia sera za wagombea hao.
“Upatikanaji wa maji safi na salama bado ni tatizo kubwa kwa watu wengi wa jiji hili, mfano kukosekana kwa mabomba ya kupeleka maji maeneo ya milimani.
“Ningependa wagombea watakaoomba ridhaa ya wananchi wajumuishe suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji kwenye sera na mikakati yao, maana bado ni kilio kwa wakazi wengi, hasa sisi wa Mwanza,” anasema Amina.
Hata hivyo, upatikanaji wa huduma ya maji nchini kwa sasa ni asilimia 90 kwa maeneo ya mjini, huku vijijini ikiwa ni asilimia 79.6, kwa mujibu wa Wizara ya Maji. Ukiacha hilo, upatikanaji wa umeme kwa sasa unazalishwa zaidi ya megawati 3,000 na vijiji 12,318 vimeunganishwa na huduma hiyo.
Kwa upande wa ajira, kwa sasa ni 8,084,203, kati ya hizo asilimia 87.96 ni sekta isiyo rasmi, huku zilizosalia ni sekta rasmi.
Ukiacha maji, Soweto Kibuye, anayeishi Mabatini jijini Mwanza, anasema changamoto ni barabara za jiji hilo, ambazo zimegeuzwa kuwa maegesho ya magari.
“Barabara za Nyamagana halmashauri imezigeuza, zimekuwa parking; barabara zimekuwa nyembamba na zinaleta kero kwa watembea kwa miguu, ndiyo maana ajali za pikipiki humu ni nyingi,” anasema Kibuye.
Kwa upande wake, Mariam Amos, mkazi wa Buswelu, manispaa ya Ilemela, anasema kero ya migogoro ya ardhi na mipango miji inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Changamoto kubwa ni migogoro ya ardhi, kila sehemu kuna shida, viwanja vinauzwa mara mbili na wanaohusika wengine ni watumishi wa umma. Wakati mwingine wamekuwa wakinyang’anya watu viwanja vyao na kuviuza, pia uuzwaji huu wa viwanja na maeneo haufuati mipango miji,” anasema Mariam.
Kajuni Sebastian, mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, anasema wagombea wanapaswa kubeba ajenda ya miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha wanaboresha barabara za mitaa ambazo hazipitiki.
“Barabara limekuwa suala la miaka na miaka. Tazama barabara ya kutoka mjini mpaka Nyegezi (Kenyatta Road), ni mtihani, kuna foleni sana kwa sababu barabara ni nyembamba, msongamano umekuwa mkubwa mpaka inaleta usumbufu, hivyo kwa barabara ya Nyerere (kwenda Buzuruga) mji wetu unakuwa basi. Mabadiliko hayo yaendane na kasi ya maboresho ya miundombinu yake,” anasema Sebastian.
“Mfano hizi barabara ambazo zinatajwa, hii sio mara ya kwanza kutajwa na huwa zinawekwa hadi kwenye ilani, lakini utekelezaji hakuna; kwa kweli sina uhakika na hiki ambacho tumeahidiwa,” anasema Mirumbe Daniel, anayeishi Mara.
Nyanjiga Mafuru anasema, endapo ahadi hizo za ujenzi wa barabara zitatekelezwa kwa wakati, hali ya maisha ya wakazi wa maeneo husika kwa namna moja ama nyingine itabadilika, kwani watakuwa na fursa nyingi za kufanya shughuli za maendeleo kwa uhakika.
“Mfano, hiyo barabara ya Tarime-Mugumu inapita kwenye vijiji ambavyo wananchi wamejikita kwenye kilimo cha migomba na maparachichi; wanalima kweli, ila sasa wanashindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni, hivyo kulazimika kuuza kwa bei ya hasara kwa wafanyabiashara wanaofika kwenye vijiji hivyo,” anasema Jacob Otieno.
Jacob Otieno anasema umefika muda sasa changamoto za wananchi zisitumike kama mtaji wa kisiasa, badala yake mamlaka husika zinatakiwa kuzifanyia kazi ili wananchi waweze kuwa na maisha bora.
“CCM hawakutakiwa kusema watashughulika na changamoto kama za barabara, wao walitakiwa waje waseme watafanya nini zaidi, kwa maana kuwa hizo changamoto zilipaswa ziwe zimeshughulikiwa kitambo. Niwaombe tu, wakifanikiwa kushika dola tena wahakikishe wananchi tunakuwa na maisha mazuri,” anasema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Ramadhan Manyeko, anasema kwa mgombea anayemaliza muda wake ndiye anayetakiwa kueleza zaidi alikwamia wapi, kwa sababu changamoto zilikuwepo.
“Kwa sababu alikuwa madarakani, huyu anapaswa kusema alikwamishwa na nini hadi kushindwa kuzimaliza kero hizo, ingawa ameshaahidi namna ya kuzitatua,” anasema.
Anasema kwa wanaoomba ridhaa kwa wananchi, wanapaswa kujikita kufafanua watakachokifanya ili kufanikisha utatuzi wa kero hizo.
“Hawa wanaoomba kwa kuwa hawakuwa madarakani, wafafanue watatumia mbinu gani kuhakikisha wanamaliza changamoto hizo,” anasema.
Akizungumzia hilo, Mkazi wa Dar es Salaam, Malinzi Nunu, anasema iwapo matatizo yao yatatatuliwa kwa ahadi zinazotolewa, malengo yasudiwa yatafikiwa.
“Barabara, maji na umeme ndizo changamoto zinazowaumiza zaidi wananchi, huku akiwasihi wanasiasa kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao. Sisi tunasumbuliwa zaidi na changamoto ya miundombinu, umeme na maji tunachoomba ahadi, zinazotolewa zitekelezwe,” anasema.
Mwananchi mwingine wa Morogoro, Salum Dimoso, anasema migogoro ya ardhi ndilo tatizo kubwa zaidi kwa wakazi wa eneo hilo na mara nyingi limesababisha mapigano ya wakulima na wafugaji.
Anaeleza viongozi wa Serikali za Vijiji ndio chanzo cha migogoro hiyo, kwani wanauza ardhi kiholela na wakati mwingine wanasimamia uuzaji kinyume na taratibu.
Mbali na hilo, anasema wanakwenda mbali zaidi hadi kufikia hatua ya kuwatetea wale wanaoshiriki kufanya makosa, ikiwemo wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Pamoja na hilo, anasema suala la uhaba wa ajira, hasa kwa vijana, ni changamoto nyingine inayowakabili wakazi wa eneo hilo na kwamba unahitaji mkakati madhubuti kukomesha hilo.
“Vijana hatuna ajira, tunaambiwa habari za kujiajiri wakati hatujatengenezewa mazingira ya kujiajiri. Kilimo cha jembe la mkono sio ajira; ni mateso. Wagombea wahakikishe wanakuja na mikakati ya kutuongezea ajira na kila kijana asibaki holela,” anasema.
Imeandikwa na: Juma Issihaka, Bakari Kiango (Dar), Beldina Nyakeke (Mara) na Daniel Masyenene (Mwanza)