Misime: Hakuna kontena la silaha lililoingizwa nchini

Wakati tuhuma za kuingizwa kwa kontena lenye silaha zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Jeshi la Polisi Tanzania limekanusha taarifa hizo likisema ni madai yasiyo na ukweli.

Hayo yameelezwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), David Misime, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Septemba 1, 2025, jijini Dodoma.

Amesema taarifa hizo zimekuwa zikisambazwa  kwenye mitandao bila uthibitisho, jambo ambalo linaweza kuleta taharuki miongoni mwa wananchi. “Hakuna kontena lenye silaha lililokamatwa, hizo taarifa ni za uongo na hazina ukweli wowote,” amesema Kamanda Misime.

Katika mazungumzo hayo, Kamanda Misime amekwenda mbali akiwaonya wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, akisema kuna baadhi wanaitumia vibaya kwa maslahi yao binafsi. 

“Jeshi la Polisi litachukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika kusambaza taarifa za uongo zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi,” amesisitiza Misime.