“KILIO kikubwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ni wachezaji kushindwa kutumia nafasi, hii ni kuanzia mwanzo wa mashindano ya CHAN hadi tumefikia tamati,” ndivyo anavyosema kocha wa timu hiyo ya taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alipozungumza na Mwanaspoti.
Anasema: “Timu inajaribu kutengeneza nafasi lakini haiwezi kuzitumia, lakini mpira ni mchakato sio kitu cha kukifanyia kazi mara moja. Naamini hii changamoto itakaa sawa.”
Kocha Morocco amekiri kuna uhaba wa washambuliaji kuanzia Ligi Kuu Bara akibainisha changamoto hiyo imekuwa ikizifanya timu kubwa za Simba na Yanga kusajili nyota wa kimataifa kwenye eneo la ushambuliaji.
“Hivyo ni changamoto ambayo inafanya hadi timu ya taifa inayumba. Hili ni suala la kitaifa, kinachotakiwa kufanyika ni kuandaa programu ya kuzalisha washambuliaji.”
Morocco ameandika rekodi katika fainali za CHAN 2024 akiwa kocha wa kwanza katika historia kuifikisha Tanzania robo fainali ambako ilitolewa na walioibuka mabingwa, Morocco ambao waliitambia Madagascar kwa mabao 3-2 usiku wa juzi jijini Nairobi.
Kauli ya Morocco imethibitisha hilo kutokana na matokeo ya timu hiyo kwa kuanzia mchezo wa kwanza wa ufunguzi hadi hatua ya robo ambayo imeitoa timu hiyo kwenye michuano kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Morocco.

Katika michezo sita ambayo Stars ilicheza katika hatua ya makundi na robo fainali imefunga mabao sita, ikianza vyema kwa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso, ikishinda 1-0 dhidi ya Mauritania, 2-1 dhidi ya Madagascar na kulazimishwa suluhu dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kabla ya kupoteza 1-0 dhidi ya Morocco katika robo fainali.
Licha ya Stars kuandika rekodi ya kucheza hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza ikimaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na sare moja, kilichozungumzwa na Morocco kwenye suala la ushambuliaji kiko wazi kwani kati ya mabao matano yaliyofungwa na timu hiyo ni mabao mawili pekee yaliyofungwa na mshambuliaji Clement Mzize, yote akifunga kwenye mchezo dhidi ya Madagascar.
Jingine moja lilifungwa kwa penalti na kiungo mshambuliaji Abdul Seleman ‘Sopu’ kwenye mchezo dhidi ya Burkina Faso, huu mabeki wakifunga mara mbili, ambapo beki mpya wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alifunga dhidi ya Burkina Faso na beki Shomari Kapombe wa Simba akitupia bao pekee lililoipa ushindi Stars dhidi ya Mauritania.

Ukiondoa hayo yote miaka ya hivi karibuni tangu amestaafu John Bocco kuitumikia Taifa Stars, kuna Mbwana Samatta, Kelvin John na Kibu Denis kwenye safu ya ushambuliaji ambao wamekuwa wakiitwa mara kwa mara na rekodi ya kutupia inashikiliwa na mawinga.
Mawinga ambao wanafanya vizuri ni Saimon Msuva aliyefunga mabao 23 katika michezo 93 ya timu ya taifa tangu alipokitumikia kikosi hicho rasmi mwaka 2012, huku akibakisha mawili tu kuifikia rekodi ya Mrisho Ngassa aliyefunga 25 kupitia mechi 100 alizochezea kuanzia mwaka 2006 hadi 2015 alipostaafu.
Anayefuata ni mshambuliaji Mbwana Samatta aliyeifungia timu ya taifa mabao 22 katika michezo 82, tangu alipoanza kuitumikia mwaka 2011, akifuatiwa na nyota, John Bocco mwenye mabao 16 katika michezo 84 baada ya kuitumikia kuanzia 2009.

Kwa rekodi hiyo ni wazi kauli ya kocha Morocco inathibitisha tatizo la ushambuliaji ndani ya kikosi cha taifa Stars huku wadau mbalimbali wakiungana naye.
Mchambuzi na mchezaji wa zamani, Tigana Lukinja alisema ukiachilia jukumu la makocha kuwatengeneza wafungaji, pia wachezaji wanatakiwa kujipanga na kijibidiisha.
“Suala la ushambuliaji sio kwa timu ya taifa tu ni hata kwenye ligi, tiba ya jambo hili ni kufanya mazoezi binafsi ya kufunga kutokea kwenye nafasi mbalimbali uwanjani,” anasema Tigana.
Mchezaji na kocha wa zamani aliye mchambuzi wa soka kwa sasa, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ alisema suala la washambuliaji sio Tanzania pekee, hata nchi nyingine zinapitia changamoto kama wanayopitia Taifa Stars.

“Hispania pia wamekuwa wakipambana na janga kama hilo wakimtumia Fernando Torres zama zinakwenda na kuisha zamani Tanzania kulikuwa na kina Peter Tino, Makumbi Juma, utawala huo umepita, sasa kuna changamoto,” alisema Maestro na kuongeza;
“Kila utawala unakuja na watu wapya. Tanzania ambayo inajipapatua kuendelea inatakiwa kuzalisha wachezaji katika eneo hilo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa kuchukua wachezaji kutoka shuleni.”
Aliongeza, kwa miaka ya sasa kila mchezaji anacheza nafasi ya kiungo kama si kiungo basi winga ndio maana wanakosa washambuliaji, akitolea mfano Ibrahim Hamad ‘Hilika’ kuwa licha ya kuwamo kikosini Taifa Stars, alikosa nafasi ya kucheza CHAN 2024 licha ya kwamba anategemewa katika klabu anayoitumikia, huku akiweka wazi kuwa uzoefu unamuondoa mchezoni.
“Hilika hakupata nafasi ya kucheza, lakini nafikiri sababu ni kukosa uzoefu nafikiri kungekuwa na mchezaji kama Kibu Denis angeweza kutusaidia,” alisema Maestro na kuongeza:
“Kuelekea michuano iliyo mbele yetu kitu kinachotakiwa kufanyika ni kutengeneza wachezaji kwa kutafuta njia ya kufanya scout kuanzia umri mdogo miaka tisa, saba kwa kutafuta mchezaji wa kucheza eneo hilo.”
Alisema ni muda sahihi kuanza kutafuta aina ya wachezaji hao kwa kuzingatia maumbile kwa kutumia miaka miwili hata mitatu wanaweza kufanikiwa kupata wachezaji ambao wataibeba timu ya taifa.
“Namungo ina washambuliaji wazawa lakini hawawezi kupata nafasi ya kucheza katika timu ya taifa, Simba na Yanga ndio zinatoa wachezaji wa timu ya taifa kwa sababu ya uzoefu wa michuano mingi. Nyota kutoka timu ndogo hata ukiwapeleka Simba au Yanga wanashindwa kufanya vizuri hii ni kutokana na kushindwa kujitambua.”