MCHEZO wa Kundi C katika michuano ya Tanzanite Pre-Season International baina ya Namungo ya Tanzania Bara na City FC Abuja kutoka Nigeria, umemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mshambuliaji wa Namungo, Heritier Makambo alifunga bao la mapema dakika ya tatu kwa ustadi mkubwa kufuatia pasi ya Abdulaziz Shahame.
Bao hilo liliwafanya wachezaji wa Namungo kucheza kwa kujiamini zaidi wakionekana kuwazidi nguvu na maarifa City FC Abuja.
Makambo alikuwa nyota hatari kwa walinzi wa City FC Abuja ambapo dakika ya 26 ilibaki kidogo aongeze bao la pili, lakini shabaha yake haikulenga vizuri lango.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga na Tabora United, aliwachambua mabeki wawili wa City FC Abuja kisha akakutana na kipa Samuel Agbana, akauinua mpira uliokwenda kugonga mwamba na kurudi uwanjani.
Tukio hilo lilimfanya Makambo kuumia na kulazimika kutolewa baada ya kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikachukuliwa na Rashid Mchelenga.
City FC Abuja ilifanya shambulizi dakika ya 30, na kumfanya kipa wa Namungo, Mussa Malika Mussa kumuangusha Ezra Maren kwenye boksi, mwamuzi akaweka mkwaju wa penalti.
Penalti hiyo iliyopigwa na Ozor Franklin kwa mtindo wa panenka, iligonga mwamba na kurudi uwanjani na kuliweka lango la Namungo salama.
Uamuzi wa benchi la ufundi la City FC Abuja chini ya kocha Richard Yamoah, dakika ya kumtoa Sadiq Aino na kuingia Uche Chidozie, ulizaa matunda kwani dakika moja tu baada ya kuingia, nyota huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto akaisawazishia timu hiyo.
Kupatikana kwa bao hilo, iliwafanya Namungo kujipanga upya na kuwapa nafasi City FC Abuja kurudisha morali ya mapambano. Hadi mapumziko matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1.
Mabadiliko ya wachezaji kadhaa katika kipindi cha pili yaliyofanywa na timu zote, hayakuwa na faida nyingine zaidi ya kutoa burudani kwa mashabiki waliofika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kushuhudia mchezo huo ambao hadi mwisho ubao ulisoma Namungo 1-1 City FC Abuja.
Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanayofanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yameanza Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025, yakiandaliwa na Fountain Gate FC.
Jumla ya timu 10 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Kundi A lina timu za Bandari FC ya Kenya, Fountain Gate na Tabora United zote za Tanzania Bara.
Kundi B zipo Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union zote za Tanzania Bara huku Kundi C kuna Namungo kutoka Tanzania Bara, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa inaibua na kukuza vipaji vya wachezaji chipukizi.