………….
NIRC:Nzega
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza uchimbaji wa visima 52 katika halmashauri nane za Mkoa wa Tabora. Ili kuwezesha wakulima wa maeneo hayo kuacha kulima kilimo cha mazoea ya kugemea msimu wa mvua na kujikita katika kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
Katika kijiji cha Miguwa, visima vitakavyochimbwa vitamwagilia zaidi ya ekari 1,590 na kuwafikia wakulima 1,567, ambao wengi wao wamekuwa wakitegemea mvua kwa ajili ya kilimo.
Akizungumza Katika uzinduzi wa uchimbaji wa visima katika kijiji chamiguwa kwa niaba ya waziri wa kilimo Hussein Bashe (MB) Katibu Tawala wa Nzega Mjini, Bi Winfrida Funto, ambaye alisoma risala rasmi ya Waziri. Amesema dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza kwa nguvu katika kilimo cha umwagiliaji ili kuinua uchumi wa wakulima wadogo na kuongeza usalama wa chakula nchini.
Kwa mujibu wa risala hiyo, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuchimba visima 67,500 katika halmashauri 184 nchini, ambapo zaidi ya wakulima 100,000 watanufaika moja kwa moja. Katika mwaka wa fedha 2025/26 pekee, visima 1,300 vinatarajiwa kuchimbwa, huku Mkoa wa Tabora ukipokea visima 52 katika halmashauri nane, ikiwemo Nzega Mji.
Kazi ya uchimbaji visima hivyo katika mkoa wa Tabora pekee imepangwa kutekelezwa ndani ya siku 21 na mradi huu unatarajiwa kuleta ajira za kudumu, fursa za kibiashara, na kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC aliwakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Teknolojia, Mhandisi Naomi Mcharo. Akizungumza kwa niaba ya Tume, Mhandisi Naomi amewaasa wananchi hao kulinda vifaa vinavyotumika katika uchimbaji wa visima hivyo.
Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza uzalishaji wa kilimo kwa 10% ifikapo mwaka 2030, na ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya awamu ya Sita, kuleta mageuzi ya kweli katika sekta ya kilimo, kupitia kilimo cha Umwagiliajiji.