Polisi waendelea kumsaka mganga anayedaiwa chanzo cha kifo cha mwanafunzi

Arusha. Zikiwa zimepita siku 17 tangu kufariki dunia kwa mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Qash iliyopo wilayani Babati, mkoani Manyara, Yohana Konki (17), Jeshi la Polisi mkoani Manyara limesema linaendelea kumsaka mganga wa kienyeji anayedaiwa kutoa ramli chonganishi iliyosababisha mauaji hayo.

Yohana, alifariki dunia baada ya kupigwa na wanafunzi wenzake kwa madai ya wizi wa kishkwambi, alfajiri ya Agosti 16, 2025, shuleni hapo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Septemba mosi, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, amesema jeshi hilo linaendelea kumsaka mganga huyo anayedaiwa kukimbia na familia yake baada ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa Kamanda Makarani, hadi sasa jeshi hilo linawashikilia wanafunzi 11 wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara bado linaendelea kumsaka mganga huyo anayedaiwa kuwa chanzo cha mauaji hayo kufuatia ramli chonganishi, kwani alikimbia baada ya tukio lile,” amesema.

Amesema jalada la mashtaka kuhusu tuhuma za mauaji zinazowakabili wanafunzi hao 11 bado lipo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa hatua zaidi. Ofisi hiyo ndiyo yenye jukumu la kuamua watuhumiwa washtakiwe au la, na washtakiwe kwa kosa lipi.

“Pia kuhusu wale wanafunzi 11 bado jalada liko NPS, tunasubiri uamuzi wa suala hilo,” ameongeza Kamanda Makarani.

Awali, Kamanda alidai chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo ni baadhi ya wanafunzi wenzake kumpiga kwa kumtuhumu ameiba kishkwambi cha mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, ambaye alikwenda na mwenzake kwa mganga wa kienyeji na kupiga ramli ili kumbaini mwizi.

“Walipotoka walimfuata huyo mwanafunzi na kumtuhumu wizi, kisha wakamlazimishe awarudishie. Alipokataa kuwa hakuiba, walimpiga na kusababisha kifo chake,” alidai Kamanda huyo wa Polisi.

Yohana alizikwa katika Kijiji cha Tsamas, wilayani Babati, Agosti 20 mwaka huu.